Mambo hadharani Ligi Kuu England

New Content Item (1)
New Content Item (1)

LONDON, ENGLAND. MECHI za wikiendi iliyopita ziliweka mambo hadharani ya yale yanayoweza kwenda kutokea msimu huu kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England.

Kwa sasa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England si za timu tatu tena, zimebaki kuwa za timu mbili tu, Arsenal na Manchester City.

Liverpool imejiondoa kwenye vita hiyo ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu baada ya kuangusha pointi zaidi kwa kutoka sare na West Ham United, huku ikiwa imetoka kuchapwa na Everton.

Aston Villa sasa kila kitu kimebaki kwenye mikono yao kuamua hatima yao ya kumaliza msimu kwenye Top Four na kukamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati mambo yamekuwa mabaya zaidi kwa Sheffield United, kwamba msimu ujao watakuwa kwenye Championship.

Makala haya yanahusu uchumbuzi wa namna mambo yalivyokuwa kwenye wikiendi iliyopita katika mikikimikiki ya Ligi Kuu England.


Liverpool yarusha taulo mbio za ubingwa
Wiki chache zilizopita, Liverpool ilikuwa kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England. Lakini, ghafla tu kiwango chao uwanjani kimeshuka na kujikuta ikipata ushindi mmoja kwenye mechi nne zilizopita na hivyo kuondoka kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Na kitu kibaya ni kwamba ilikuwa na wasiwasi hata kwenye mchakamchaka wa kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. Kama matokeo yangekuwa ya kuchapwa dhidi ya West Ham basi Top Four pia ingekuwa kwenye shaka kubwa kutokana na kuchuana na wapinzani Aston Villa na Tottenham Hotspur wakisaka nafasi hiyo ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Na mbaya zaidi, mechi zake tatu zilizobaki, mbili itakabiliana na wapinzani wake hao.

Itaanza kwa kukipiga na Spurs kwenye Uwanja wa Anfield, kisha itakwenda kukipiga na Aston Villa huko Villa Park kabla ya kumalizana na Wolves katika mchezo wao wa mwisho kwenye ligi msimu huu.

Kwa kiwango cha Liverpool cha sasa kuna wasiwasi kama itaweza kushinda mechi hizo zilizobaki, lakini kitu kizuri ni kwamba pointi ilizokusanya, zimetosha kuwahakikishia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Sheffield United yashuka daraja

Ilipata bao la kuongoza mapema tu dhidi ya Newcastle United uwanjani St James’ Park, lakini ghafla mambo yalibadilika na kujikuta ikipoteza mechi ya nne mfululizo kwenye Ligi Kuu England. Kipigo hicho kimehitimisha zama za Sheffield United kucheza kwenye Ligi Kuu England na kwamba itakuwa kwenye Championship msimu ujao.

Kikosi hicho cha kocha Chris Wilder kilitibua mambo kwenye kipindi cha pili na kuchapwa mabao 5-1. Kwenye kipindi cha kwanza ubao wa matokeo ulisomeka 1-1 baada ya Alexander Isak kuisawazishia Newcastle baada ya bao la kuongoza la Sheffield United lililofungwa na Anel Ahmedhodzic.

Kipindi cha kwanza Sheffield United ilionekana kuwa na ubora na kupoteza nafasi kibao za kufunga, lakini iliruhusu mabao matatu ndani ya dakika 11 kwenye kipindi cha pili na hicho kilimaliza kila kitu, kabla ya Callum Wilson kufunga bao la tano kwenye dakika ya 72.
Newcastle ilitengeneza nafasi nne kubwa kwenye mchezo huo na zote ilizozitumia kutumbukiza mipira nyavuni.

Kasheshe kubwa uwanjani Villa Park  
Aston Villa ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Villa Park ilifunga bao la mapema kabisa dhidi ya Chelsea baada ya beki Marc Cucurella kujifunga. Morgan Rogers aliendelea kuonyesha kiwango chake bora kabisa akiwa na chama lake la Aston Villa baada ya kufunga bao la pili kabla ya filimbi ya mapumziko.

Staa huyo aliyesajiliwa kwenye dirisha la Januari, sasa amefunga mabao matatu na kuasisti mara moja katika mechi zake tano alizocheza kwenye Ligi Kuu England tangu alipojiunga na miamba hiyo ya Villa Park.

Chelsea ilijibu mapigo kwenye kipindi cha pili na kutawala mchezo. Ilikuwa na umiliki wa mpira kwa asilimia 69 na ilipiga mashuti 13 dhidi ya manne tu iliyopiga Aston Villa kwenye kipindi cha pili. Na namna ilivyocheza kwenye kipindi cha pili, mambo yalikuwa mazuri kwa The Blues, ilipofunga mara mbili na kufanya ubao wa matokeo usomeke 2-2.

Noni Madueke na Conor Gallagher walifunga mabao kwenye kikosi hicho cha kocha Mauricio Pochettino na ilifunga bao la tatu kupitia kwa Axel Disasi, lakini VAR ilikataa bao hilo kwa kuwa kulifanyika madhambi kabla ya bao hilo kufungwa.
Aston Villa sasa inaweza kuona imepoteza pointi mbili tu kwenye mechi hiyo, lakini madhara yake ni makubwa kwenye vita yao ya kufukuzia nafasi kwenye Top Four ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Wapinzani wao kwenye vita hiyo ni Spurs, ambao walikubali kipigo cha mabao 3-2 nyumbani dhidi ya Arsenal, huku Manchester United ikijiweka mbalimbali kabisa baada ya kutoka sare dhidi ya Burnley uwanjani Old Trafford.
Kinachotishia Amani kwa Aston Villa ni kwamba wapinzani wao Spurs bado wana mechi mbili mkononi.

North London derby ilikuwa burudani

Ilikuwa mechi ya kugawana vipindi kati ya mahasimu wawili, Tottenham Hotspur na Arsenal walipomalizana na kuonyesha ubabe kwenye North London derby. Katika mechi hiyo, Arsenal iliongoza mabao 3-0 hadi mapumziko dhidi ya mahasimu wao hao, huku Bukayo Saka na Kai Havertz wakionyesha kiwango bora kabisa kwa upande wa kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta.

Hata hivyo, mabao hayo hayakuwa yameonyesha taswira halisi ya mchezo huo. Spurs ilifunga bao, likakataliwa kwa madai ya mfungaji alikuwa ameotea na hapo ilionekana kama mechi hiyo bado haijakwisha. Spurs pia ilinyimwa penalti kuonyesha kwamba kuna kitu timu hiyo ilikuwa inakifanya ndani ya uwanja kupambana kwenye mechi ya mahasimu wawili wa jiji la London.

Kwenye kipindi cha pili, Arsenal ilirudisha timu nyuma na kuwapa nguvu Spurs ya kupeleka mashambuli, wakifanikiwa kufunga kupitia kwa Cristian Romero baada ya makosa ya kipa David Raya, kabla ya Heung-Min Son kufunga kwa mkwaju wa penalti katika dakika tatu za mwisho.

Mabao hayo mawili yaliamsha mizuka ya Spurs na kuanza kuishambulia Arsenal kwa nguvu zote jambo lililowafanya wababe hao wanaonolewa na Mikel Arteta kuwa kwenye shaka nzito ya kuharibu mipango yao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England.
 
Mabingwa watetezi wazidisha presha
Manchester City ndiyo iliyocheza mechi ya mwisho kabisa kwa wikiendi iliyopita wakati mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England kuwashusha daraja Nottingham Forest. Kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kilifahamu wazi kinachokwenda kufanya kwenye mechi hiyo baada ya wapinzani wao kwenye mbio za ubingwa huo, Arsenal kushinda kwenye mchezo wao wa mapema.

Ushindi wa Arsenal iliweka pengo la pointi kufikia nne, hivyo Man City ilihitaji ushindi ili kufanya ibaki pointi moja baina yao, huku wao wakiwa na faida ya kuwa na mchezo mmoja mkononi, ambao kama watashinda, basi watapanda kileleni na kuongoza kwa tofauti ya pointi mbili. Kiungo mchezeshaji, Kevin De Bruyne aliendelea kuonyesha umahiri wake kwenye mchezo huo kwa kuisaidia Man City kushinda 2-0 na hivyo kufikisha pointi 79, zinazowafanya kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo, kwa tofauti ya pointi moja tu dhidi ya Arsenal, yenye pointi 80.

Nottingham Forest ingeweza kuiweka Man City kwenye wakati mgumu endapo kama mshambuliaji wao Chris Wood angetumia nafasi zake alizopata vizuri na kufunga mabao. Lakini, viwango vya mchezaji mmoja mmoja ndivyo vilivyoleta tofauti katika mechi hiyo iliyopigwa City Ground juzi Jumapili.