Afcon yamponza Rais wa Soka Zambia

Muktasari:

  • Kamanga (56) anashikiliwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha zilizokusanywa na serikali kwa kuwasafirisha na kuwagharamia rafiki yake na mtu wa familia yake kwenye safari ya kwenda kwenye Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) zilizofanyika Januari 2023 nchini Ivory Coast.

RAIS wa Shirikisho la Soka Zambia (Faz), Andrew Kamanga anashikiliwa na mamlaka za nchini humo kwa tuhuma za utakatishaji fedha.

Kamanga (56) anashikiliwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya fedha zilizokusanywa na serikali kwa kuwasafirisha na kuwagharamia rafiki yake na mtu wa familia yake kwenye safari ya kwenda kwenye Fainali za Mataifa Afrika (Afcon) zilizofanyika Januari 2023 nchini Ivory Coast.

Rais huyo wa Faz aliyemadarakani kuanzia mwaka 2016 anashikiliwa pamoja na katibu mkuu wa Shirikisho hilo Reuben Kamanga kwa makosa hayohayo.

Taarifa iliyotolewa na tume ya kuzuia na kupambana na dawa ya kulevya na makosa ya utakatishaji wa fedha (DEC) imesema Kamanga anashikiliwa kwa kuwasafirisha Madalitso Kamanga na Jairous Siame kwenda nchini Ivory Coast akitumia kiasi cha Kwacha ya Zambia 99,980 (Sh9.9 milioni) ambao hawakuwa maafisa wa Faz.

Taarifa hiyo ya kushikiliwa kwa Kamanga inakuja zikiwa zimesalia siku chache kabla ya kufanyika kwa mkutano mkuu wa Faz utakafanyika wikiendi hii jijini Lusaka.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa na Faz inasema hatua ya kushikiliwa kwa Kamanga hakuna tishio lolote la kumuondoa madarakani na kwamba hizo ni tuhuma ambazo zitahitaji kufanyiwa kazi mahakamani.