JIWE LA SIKU: Klopp, Mourinho wote sio chaguo la kwanza, wametoboa

Muktasari:

  • Wakati Liverpool inaachana na Brendan Rodgers chaguo lao la kwanza la kocha waliyekuwa wakimhitaji alikuwa Carlo Ancelotti. Fenway Sports Group, kampuni inayomiliki klabu ya Liverpool ilikuwa ikimfukuzia Mtaliano huyo akapige kazi Anfield. Kipindi hicho, Klopp hakuwa kabisa kwenye mipango.

LIVERPOOL, ENGLAND

XABI Alonso. Ni jina linatamba kwenye soka la kisasa huko Ulaya.

Kwa kile anachokifanya Bayer Leverkusen, amekuwa kwenye rada za timu nyingi zinazohitaji huduma yake.

Liverpool iliweka jina lake ubaoni, walitaka aje kuchukua mikoba ya Jurgen Klopp anayeondoka kwenye timu yao mwisho wa msimu huu.

Ni hivyo pia kwa Bayern Munich. Ilimhitaji aje kwenye benchi lao la ufundi kumbadili Thomas Tuchel, ambaye pia mwisho wa msimu huu ataachana na maisha ya huko Allianz Arena.

Barcelona ilihusishwa naye pia, ambapo miamba hiyo ya Nou Camp itaingia sokoni kusaka kocha mpya mwishoni wa msimu huu, kwa sababu Xavi atakusanya virago vyake kuondoka.

Real Madrid nayo kuna wakati ilimpigia hesabu wakimtaka aje Bernabeu wakiamini atawafaa wakati Carlo Ancelotti atakapoondoka. Ndiyo hivyo. Kila kona wanamtaka Alonso.

Lakini, kocha huyo Mhispaniola amefanya uamuzi wa kubaki Bayer Leverkusen walau kwa msimu mmoja zaidi. Jambo hilo, litazifanya klabu zilizokuwa zinamhitaji, ikiwamo Liverpool kupoteza fursa ya kunasa chaguo lao la kwanza la kocha waliyemtaka aje kupiga kazi Anfield.

Klopp anaondoka Anfield baada ya karibu misimu tisa ya kuinoa timu hiyo. Liverpool chini ya Klopp imefanya mambo mengi, ikiwamo kumaliza ukame wao wa kubeba taji la Ligi Kuu England, ambalo walilibeba baada ya kusubiri kwa miaka 30. Chini ya Klopp, Liverpool imekuwa timu yenye ushindani wa kugombea mataji karibu ya mashindano yote yanayowaniwa kwa msimu.

Mashabiki wa Liverpool wanawaza, maisha yatakuwaje bila ya huduma ya Klopp hasa wakikumbuka alikowatoa Mjerumani huyo. Liverpool bila ya Klopp itakuwaje?

Alonso lilikuwa chaguo la kwanza na limekwama. Ruben Amorim, kocha wa Sporting Lisbon ya Ureno alitajwa kuwa chaguo la pili baada ya kukwama kwa Alonso. Naye, kuna dalili ya kumkosa pia.

Na sasa ubaoni kuna jina la Arne Slot. Unaweza kulisema ni chaguo la tatu kwenye orodha ya makocha waliofikiriwa huko Anfield. Slot ni kocha wa Kidachi na anafanya vizuri Feyenoord.

Je, kuna shida kuja kunolewa na kocha chaguo la tatu kwenye mipango yenu?

Ni hivi, hata Klopp mwenyewe hakuwa chaguo la kwanza wakati anapewa kazi Liverpool. Lilikuwa chaguo la pili.

Kwa alichokifanya kuna mtu anayekumbuka tena kwamba alikuwa chaguo la pili?

Wakati Liverpool inaachana na Brendan Rodgers chaguo lao la kwanza la kocha waliyekuwa wakimhitaji alikuwa Carlo Ancelotti. Fenway Sports Group, kampuni inayomiliki klabu ya Liverpool ilikuwa ikimfukuzia Mtaliano huyo akapige kazi Anfield. Kipindi hicho, Klopp hakuwa kabisa kwenye mipango.

Lakini, ilipokwama kwa Ancelotti ilihamia kwa Klopp, ambaye amekwenda kufanya mambo makubwa sana tangu alipojiunga na miamba hiyo. Kwa maana hiyo, hata chaguo la pili au tatu linaweza kufanya vizuri.

Si Klopp tu kuwa chaguo la pili Liverpool na kufanya vizuri, hata Jose Mourinho wakati anatua Chelsea mwaka 2004, hakuwa kocha chaguo la kwanza kwenye mipango ya miamba hiyo ya Stamford Bridge.

Wakati bilionea mmiliki wa klabu ya Chelsea kwa wakati huo, Roman Abramovich alipotaka kumbadili kocha Claudio Ranieri, chaguo la kwanza la kocha aliyemtaka aje Stamford Bridge alikuwa Sir Alex Ferguson wa Manchester United. Lakini, ilipoonekana kuwa hilo ni jambo gumu kumng'oa Ferguson huko Old Trafford, Abramovich alihamia kwa Mourinho, ambaye kwa wakati huo alikuwa ameipa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, FC Porto ya Ureno.

Na baada ya Mourinho kutua Stamford Bridge alichokwenda kukifanya, amemfunika Ferguson na kuvunja utawala wa kocha huyo Mskochi, ambaye kabla ujio wa Mourinho, mpinzani wake mkubwa alikuwa Arsene Wenger wa Arsenal.

Haikushia hapo, hata Rafa Benitez, aliyeipa ubingwa wa Ulaya Liverpool, naye wakati ananaswa na miamba hiyo ya Anfield hakuwa chaguo la kwanza, alikuwa chaguo la tatu.

Kwenye mipango wao wa awali, Benitez hakuwa chaguo lao la kwanza, walikuwa wakiwaza kuhusu makocha wengine kabisa, lakini walimpa kazi Mhispaniola huyo, aliyekuja kuwapa taji la tano la Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2005. Kipindi hicho, Liverpool ilikuwa inawafikiria makocha kama Gordon Strachan, Martin O’Neill na Alan Curbishley. Kilikuwa ni kipindi ambacho Liverpool iliachana na Gerard Houllier.

Mafanikio makubwa kabisa iliyopata Arsenal kwenye Ligi Kuu England ni kipindi ilipokuwa chini ya Mfaransa, Wenger. Kocha huyo aliipa Arsenal mataji matatu ya Ligi Kuu England na tangu aondoke, hawajafanikiwa kubeba tena taji hilo. Lakini, kwa taarifa tu, wakati Arsenal inamnasa Wenger, hakuwa chaguo lao la kwanza, alikuwa namba mbili kwenye orodha ya makocha ambao iliona wanafaa kupewa kazi Highbury, maskani ya The Gunners kwa wakati huo. Mabosi wa Arsenal, kwa wakati huo chaguo lao la kwanza lilikuwa Johan Cruyff.

Ilipokwama kumpata Cruyff, akili ya mpira kwenye vikosi vya Ajax na Barcelona, basi walihamia kwa Wenger na kuja kumpa kazi. Lakini, ni chaguo hilo la pili lililokuja kuleta mapinduzi makubwa ya kisoka kwenye kikosi cha Arsenal na soka la England kwa ujumla wake.

Ranieri, ambaye aliifanya Leicester City kuingia kwenye rekodi za kuwa moja ya timu zilizobeba ubingwa wa Ligi Kuu England, naye hakuwa chaguo la kwanza huko King Power, wakati anapewa mikoba. Alikuwa chaguo la pili, huku Marcelo Bielsa, aliyerejea Leeds United kwenye Ligi Kuu England baada ya miaka kibao, alikuwa chaguo la nne kwenye klabu hiyo yenye maskani yake Elland Road.

Hata Newcastle United ilimpa kazi Eddie Howe akiwa chaguo lao la pili kwenye orodha ya makocha iliyokuwa ikiwataka, huku Tottenham Hotspur, yenyewe kocha wao wa sasa Ange Postecoglou ni chaguo la tatu, kama ilivyokuwa walipompa kazi Mauricio Pochettino na kuwafikisha fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, naye alikuwa chaguo la tatu kwenye orodha ya makocha iliyokuwa inawataka wakapige kazi huko London.

Kwa maana hiyo, Liverpool bado itakuwa salama endapo itaamua kumpa kazi Slot kuja kumrithi Klopp baada ya kushindwa kwenye chaguo lao la kwanza la kumnasa Xabi Alonso.