Makocha sita watajwa kumrithi Ten Hag

Muktasari:

  • Mwenendo usioridhisha wa Man United katika Ligi Kuu England msimu huu umeonekana kuupa wasiwasi uongozi wa timu hiyo chini ya Sir Jim Ratcliffe ambao umeamua kuchukua uamuzi mgumu wa kuachana naye mwishoni mwa msimu.

Manchester, England. Kibarua cha kocha Erik ten Hag kuinoa Manchester United kinaelekea kuota nyasi na imeripotiwa kuwa timu hiyo ina orodha ya makocha sita ambao mmojawapo atarithi mikoba ya Mholanzi huyo.


Mwenendo usioridhisha wa Man United katika Ligi Kuu England msimu huu umeonekana kuupa wasiwasi uongozi wa timu hiyo chini ya Sir Jim Ratcliffe ambao umeamua kuchukua uamuzi mgumu wa kuachana naye mwishoni mwa msimu.


Licha ya kuingia fainali ya Kombe la FA, uongozi wa Manchester United inaonekana haufurahishwi na namna timu hiyo inavyocheza na hivyo umeanza kupembua majina ya makocha sita ili ubaki na mmoja.


Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate anatajwa kuushawishi uongozi wa Man United kumuweka katika vipaumbele kama ilivyo kwa kocha wa Sporting Lisbon anayewaniwa pia na Liverpool na West Ham Utd, Ruben Amorin.


Ukiondoa wawili hao, kocha ambaye ameifanya Brighton kuwa timu sumbufu kwenye Ligi Kuu England, Roberto de Zerbi naye anatajwa kuwa kwenye mpango wa Manchester United kama ilivyo kwa kocha wa zamani wa Chelsea, Graham Potter.


Makocha wengine wawili ambao wanatimiza orodha ya sita waliopo katika hesabu za Manchester United ni Thiago Motta wa Bologna na Thomas Tuchel ambaye ataachana na Bayern Munich mwishoni mwa msimu huu.


Kwa mujibu wa ripoti, mchakato wa kusaka kocha mpya kati ya hao sita tayari umeshaanza na upo chini ya mkurugenzi mpya wa michezo wa Manchester United, Jason Wilcox.


Manchester United ipo katika hatari ya kukosa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwani ipo katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa EPL ikiwa na pointi 50 ambazo ni 16 pungufu ya zile za Aston Villa iliyopo katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.


Kitendo cha Aston Villa kupata pointi tatu katika mechi mechi nne ilizobakiza kitamaanisha kuwa Man United itakosa tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao kwani haitafikisha pointi 71 ambazo Villa itazifikisha. Pia timu hiyo inakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Newcastle United, West Ham na Chelsea katika kuwania tiketi ya kushiriki mashindano ya Europa League.