Diarra dhidi ya Lakred

WAKATI homa ya pambano la Ligi Kuu Bara kati ya vinara wa ligi, Yanga dhidi ya Simba likizidi kupanda kutakuwa na vita nyingine mpya kwenye eneo la makipa wa timu hizo mbili.

Hapana shaka Yanga golini nafasi kubwa itakuwa kwa kipa namba moja, Djigui Diarra ambaye sio mgeni wa mechi hizo akicheza mechi yake ya tisa dhidi ya Wekundu wa Msimbazi tangu aanze kuitumikia timu hiyo.

Ikumbukwe kwamba Diarra mechi yake ya kwanza akiitumikia Yanga iliyokuwa dhidi ya Simba ilikuwa Septemba 25, 2021 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii na akapata ushindi wake wa kwanza kwa bao la mshambuliaji, Fiston Mayele.

Kwenye mechi tisa, Diarra ana rekodi nzuri na mbaya ambapo ameiongoza Yanga kucheza mechi tano za ligi na mchezo wa leo, Jumamosi utakuwa wa sita kwake.
Kwenye mechi tano za ligi Diarra ameshinda mechi moja katika ushindi wa msimu huu wa mabao 5-1 akipoteza moja na kutoka sare tatu.

Nje ya hapo amecheza mechi tatu za Ngao ya Jamii akishinda mbili na kupoteza moja ya msimu huu kwa penalti iliyopigwa  Tanga, lakini pia akikutana na Wekundu mara moja katika Kombe la FA akipata ushindi.

Kipa huyo raia wa Mali, kwa ujumla ameitumikia Yanga dakika 810 akiruhusu mabao matano pekee ndani ya mechi hizo.


Ayoub Lakred
Kwa upande wa Simba uhakika haitakuwa na kipa mkongwe, Aishi Manula anayetajwa kuwa majeruhi ambaye ndiye kipa aliyecheza mechi nyingi dhidi ya Yanga na nafasi kubwa inaweza kutua kwa Mmorocco Ayoub Lakred.

Tangu kutua kwa kocha Abdelhak Benchikha imeonekana kete yake kuelemea kwa Lakred kuwa kipa chaguo la kwanza kwake ambapo baada ya hivi karibuni kuwa kwao kwa ruhusa maalumu amerejea nchini na kuonekana anaweza kuwa golini.
Lakred huu utakuwa mchezo wake wa kwanza dhidi ya Yanga ambapo tangu atue nchini hajawahi kupata muda wa kucheza dhidi ya mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara na mara hii akienda kuonja joto la kwanza msimu huu.

Nje ya Lakred labda Simba inaweza kumpa nafasi Ally Salim ambaye naye ana rekodi yake ya kipekee akiwa hajawahi kuruhusu bao kwenye mechi mbili ambazo amewahi kuiongoza Simba, lakini pia akiwa ndiye shujaa wa Wekundu walipochukua taji pekee wanaloshikilia msimu huu la Ngao ya Jamii alipocheza penalti za Yanga jijini Tanga.

Katika dabi ya mwisho ya msimu uliopita kwa Simba langoni alisimama Salim na Wekundu kushinda kwa mabao 2-0, lakini dabi ya kwanza ya msimu huu alikuwa Manula na kukutana na kipigo cha mabao 5-1.

Kipa mwingine wa Simba ni Hussein Abel ambaye hajatumika sana katika ligi zaidi ya michezo ya Kombe la Shirikisho (FA) ambayo timu hiyo ilitolewa kwenye hatua ya 16 bora na Mashujaa ya mjini Kigoma kwa mikwaju ya penalti na dalili zote ni kwamba kwa Kariakoo Dabi inayopigwa leo  Mmorocco ndiye atakayesimama langoni kukabiliana na mashambulizo kutoka kwa watani zao wa jadi.

Diarra kamuacha hapa Lakred
Diarra msimu huu anamzidi jambo moja Lakred akiwa na ‘clean sheet’ tisa katika  Ligi Kuu Bara dhidi ya Mmorocco huyo mwenye tano.

Hata hivyo ni jambo la kusubiri na kuona nani ataendelea kuweka rekodi yake sawasawa kati ya Diarra na makipa wenzake wa Simba ambaye atapata nafasi ya kuongoza timu yake kwenye mchezo huo mgumu zaidi nchini.