Kanuni yaongeza utata sakata la Dube, Azam FC

Muktasari:

  • Kanuni ya 74 ya Ligi Kuu msimu huu ambayo ni mikataba, ibara yake ya nane inaonekana kumpa nguvu Dube ikiwa kweli mkataba huo wa nyongeza haukuwasilishwa TFF.

Wakati kukiibuka tetesi mkataba ulioongezwa wa Azam FC na Prince Dube hakuwasilishwa katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kanuni za Ligi Kuu 2023/2024 zinakinzana katika kuamua upande upi uko sahihi kati ya klabu hiyo na mchezaji huyo.

Kanuni ya 74 ya Ligi Kuu msimu huu ambayo ni mikataba, ibara yake ya nane inaonekana kumpa nguvu Dube ikiwa kweli mkataba huo wa nyongeza haukuwasilishwa TFF.

"Mikataba yote ya wachezaji wa Ligi Kuu lazima isajiliwe na kuthibitishwa na TFF. Mkataba wa mchezaji ambao haujasajiliwa na kuthibitishwa na TFF hautatambuliwa. Mkataba wa Nyongeza (extension of contract) Utasajiliwa TFF kwa sharti la Uthibitisho wa pande zote husika za mkataba," inafafanua ibara ya nane ya kanuni hiyo.

Hata hivyo, Ibara ya kwanza ya kanuni hiyo inaonekana kuipa nguvu klabu ya Azam kwa mkataba huo kwa vile inafafanua utawasilishwa TFF wakati wa maombi ya usajili, muda ambao huwa ni wakati wa dirisha la usajili.

"Klabu ya Ligi Kuu ni lazima iwe na mkataba na mchezaji wake kwa timu ya kwanza (senior) na timu za vijana (U20/U17) ili aweze kuidhinishwa kucheza katika michezo ya Ligi Kuu na mashindano yoyote mengine rasmi yanayotambuliwa na TFF, mkataba huo utawasilishwa TFF wakati wa maombi ya usajili wa mchezaji husika," inafafanua ibara hiyo.

Akizungumzia utata ulioibuka baina ya Azam na Dube, wakili Idd Monday alisema utata wa jambo hilo utamalizwa ikiwa kutakuwepo na kujiridhisha kama Dube na Azam walifikia makubaliano ya mkataba mpya au la na siyo hoja ya mkataba kusajiliwa au kutosajiliwa TFF.

"Mtazamo wangu ni kuwa uhalali wa mkataba utakuwepo iwapo masharti yote yanayotakiwa kuwepo ndani ya mkataba baina ya Azam na Mchezaji yalitimizwa na sio lazma mkataba huo uwepo kwenye TMS kama inavyodaiwa kwa kuwa hizo ni taratibu za kutafuta leseni ya mchezaji ili aweze kucheza ligi na sio taratibu ya uthibitishaji uhalali wa mkataba.

"Kwa suala la Dube, je anautambua mkataba wa nyongeza baina yake na Azam? Kama anautambua je pingamizi/hoja yake ni kuwa mkataba haukupelekwa TFF au hautambui kabisa mkataba husika? Kinachoanza ni mkataba baina ya Klabu na Mchezaji, baada ya hapo ndo taratibu za usajili zinafata ili mchezaji aweze kupata leseni ya kucheza ligi kuu ya Tanzania kupitia mifumo ya usajili iliyowekwa.

"Kwa mtazamo wangu Mkataba unakua halali baada ya kusainiwa na pande mbili kwenye mkataba, suala la mkataba kuthibitishwa na TFF linatokea pale na mnatafuta leseni ya mchezaji kucheza ligi ya Tanzania, kwa mantiki hiyo TFF ili watoe leseni wanahitaji mkataba baina ya klabu na mchezaji, je wanapolekewa mkataba husika wanakua wanapekewa mkataba pambo?" alisema Wakili Monday.

Mchambuzi wa soka, Michael Mwebe alisema mkataba kuwasilishwa TFF haipaswi kutafsiriwa kama kipimo cha mwisho cha uhalali wa mkataba huo.

"Kuna mifano mingi ya mikataba ambayo haikuwasikishwa kwenye mamlaka husika lakini ikajadiliwa uhalali wake. Mfano mzuri ni kesi ya Bernard Morrison. Kamati ilijadili kesi ya nyongeza ya mkataba wake. Haukuwepo TFF. Sidhani kama kamati ingesema hatuwezi kujadili kitu ambacho hakipo kwenye mfumo. Mfumo upo Kwa nia ya kuimarisha ushahidi na kupunguza utata.

Mfano mwingine ni kesi za wachezaji ambao wanaingia mkataba na timu lakini Kwa sababu moja au nyingine kama kukosa ITC, kufeli vipimo au timu kuwa imefungiwa wameshindwa kusajiliwa kwenye mfumo wa usajili.

Bado FIFA inatambua mikataba yao na klabu

Hoja ya kukazia. Ni kuwa wanaoweka mikataba kwenye mfumo ya usajili ni vilabu wala sio wachezaji au TFF. Huu ni ushahidi tu.

"Chukulia klabu imeweka mkataba feki kwenye system (mfumo), mchezaji akaja na nakala halisi au kuonyesha mkataba uliowekwa una saini ambazo sio zake. Tunafanyaje? Tunasema tunautambua huu mkataba kwa sababu uko kwenye system?," alimalizia Mwebe.

Straika huyo wa kimataifa wa Zimbabwe aliyejiondoa Azam FC, alikimbilia TFF kushtaki juu ya madai ya viongozi wa Azam kuwa na mkataba mpya utakaomalizika mwaka 2026, huku mwenyewe anadai utaisha 2024.

Katika kesi hiyo ilisikilizwa jana, Azam iliwakilishwa na wakili wa kimataifa kutoka Ureno kwa njia ya mtandao ambaye jina lake halikutambulika mara moja kutokana na usiri wa kamati hiyo ya TFF inayoongozwa na Mwenyekiti, Said Soud.

Mwanasheria wa mchezaji huyo, Respicius Didas alinukuliwa jana akisema anaamini kamati itatenda haki kwa mteja wake.

Didas ambaye ni mtu mwenye mwili mkubwa kimwonekano huku kivalia suti alisema tumesikilizwa vizuri pande zote mbili upande wao mwakilishi alijumuika nasi kwa njia ya mtandao.

"Siwezi kusema nini tumeongea ndani lakini suala ni kuhusu mkataba, tunachojua mteja wangu mkataba wake unaisha mwisho wa msimu huu, tumejieleza na wao wameeleza tunasubiri wapitie na kuona nini tena kinaweza kufuata," amesema.

Awali taarifa ya Azam waliyoitoa kuhusu Dube ni kuomba kuvunja mkataba, Azam walisema mkataba wao na mchezaji huyo utaisha 2026 na Mwanaspoti limeambiwa wanamuuza Sh700 milioni wakati alishawaomba awarudishie milioni 500 walizompa ili waachane kiroho safi.

Dube alijiunga na Azam, Agosti 2020 kwa kusaini mkataba wa miaka miwili hadi 2022. Mwaka mmoja baadaye, 2021, alisaini nyongeza ya mkataba hadi 2024, lakini klabu hiyo imeadaiwa aliongezewa hadi mwaka 2026, kitu mchezaji huyo aliyejiunga klabuni na kurudisha kila kitu amekikanusha kabla ya kukimbilia TFF kufungua kesi.