Wakongwe: Ni Dabi ya suluhu au sare

Muktasari:

  • Mzunguko wa kwanza Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo ilifungwa mabao 5-1, lakini pamoja na hilo mastaa hao hawaoni kama linaweza likajirudia.

 Mastaa waliowahi kuzichezea Simba na go Yanga wametoa utabiri wa mechi ya Kariakoo Dabi ya Ligi Kuu Bara inayopigwa kesho, Jumamosi, uwanjani Benjamin Mkapa, wengi wao wakiiona suluhu au sare.

Mzunguko wa kwanza Simba ikiwa mwenyeji wa mchezo ilifungwa mabao 5-1, lakini pamoja na hilo mastaa hao hawaoni kama linaweza likajirudia.

Mwanaspoti limefanya mahojiano na baadhi ya mastaa hao kwa nyakati tofauti wamezungumzia kwa uzoefu wao na huu ndio utabiri wao.

DANNY MRWANDA
Mshambuliaji wa zamani wa Simba na Yanga, Danny Mrwanda kwa mtazamo wake anaiona mechi hiyo inaweza ikamalizika kwa suluhu au sare ya bao 1-1.

Mrwanda ambaye  mara ya mwisho alionekana na timu Ken Gold ya Mbeya amesema: "Nimebahatika kucheza hizo klabu  mbili, wakati mwingine inakuwa vigumu kujua nini kitatokea zina maandalizi yao ya tofauti kabisa katika mechi ya dabi.

Ameongeza: "Hakuna ubishi Yanga ipo vizuri, ila hizo dabi wakati mwingine zinaweza zikawastaajabisha kwa kutumia mastaa wenye nyota na siyo kiwango cha mchezaji. Mengine sisemi sana maana mimi bado nacheza."


CHARLES ILANFYA
Mwaka 201, Charles Ilanfya alikuwa na kikosi cha Simba na sasa mshambuliaji huyo yupo na  Mtibwa Sugar, lakini utabiri wake ni kwamba Yanga itashinda ila siyo kwa mabao mengi kama ilivyokuwa mzunguko wa kwanza.

"Yanga ipo vizuri, naipa nafasi ya kushinda ingawa sijui idadi ya mabao. Pamoja na hilo yatakuwa chini ya mabao matano kama waliyofunga mzunguko wa kwanza. Simba haitakubali kupigwa kipigo kikubwa," amesema.

BALAMA MAPINDUZI
Winga  wa zamani wa Yanga, Balama Mapinduzi ambaye kwa sasa anaichezea Mashujaa anaamini mechi hiyo itamalizika  kwa sare ya mabao 2-2.

"Pamoja na kwamba Simba tuliwatoa kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC) haina maana ni timu mbaya siku hiyo hawakujitoa ni kama morali yao ilikuwa chini na ni jambo la kawaida kwa wachezaji. Halafu dabi ni dabi, kingine ninachokiona viungo wataamua mechi," amesema.


RASHID JUMA
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Rashid Juma, amesema dabi hiyo itamalizika kwa sare ila hajui itakuwa ya mabao mangapi.

Mchezaji huyo anayeichezea Mtibwa Sugar amesema, "ni kweli Yanga ipo vizuri ila hiyo mechi ni dabi, lolote linawezekana hata kama akili haitaki kukubaliana, pia inakuwa na presha kubwa ya vitu vingi."