HADITHI: Zindiko (sehemu ya 13)

Muktasari:

  • Huu ni mwendelezo wa hadithi tamu na ya kusisimua ya Zindiko iliyojaa visa na mikasa ya kimaisha kutoka kwa mtunzi mahiri wa riwaya, SULTAN TAMBA. Twende naye...

KATIKA familia yao, yeye peke yake ndiye mtu ambaye ana uwezo mkubwa kimaisha anayetegemewa na familia nzima. Kwa hiyo lolote linalomhusu mama yake, lilikuwa ni juu yake licha ya kuwa na kaka zake wawili, dada zake, shangazi na wajomba. Lakini yeye ndio alikuwa kila kitu kwenye tiba ya mama yake mzazi!

Nyakati fulani, hali ya mama yake ilikuwa mbaya sana, akalazimika kuishi naye nyumbani kwake na kikundi cha ndugu zake, dada zake, shangazi na ndugu wengine ambao wote walikuwa wakimhudumia mama kwa hili na lile. Yeye kwa sababu alikuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, hakuwahi kutetereka. Malipo ya ubunge, marupurupu na mambo mengine ya hapa na pale kwenye wadhifa wake, yalimfanya kuwa na maisha mazuri na kumudu kila alichotaka.

Siku moja mama yake aliamka vibaya zaidi, daktari akaja palepale nyumbani na kujaribu kumhudumia, maana kutokana na utu uzima wake, hospitali pakawa pamemchosha kwa hiyo madaktari wakati mwingine walikuwa wakija palepale na akizidiwa pia walikuwa wanafika kama hivyo.

Mama wa Mheshimiwa Mbunge huyo akapatiwa huduma na daktari akamchoma sindano ya usingizi ili apumzike. Hapo daktari akatoa maelekezo ya jinsi ya kumhudumia atakapoamka na Mheshimiwa Mbunge akampakia daktari kwenye gari lake na kuanza safari ya kumrudisha daktari kazini kwake!

Wakiwa njiani, wakazama katika mazungumzo. Wawili hawa walikuwa wanafahamiana. Pia kwa miaka mingi, daktari huyo amekuwa ni kama daktari wa familia, hasa kwa tatizo la mama yake – kwa hiyo waliongea mengi.

Kumbe wakati huo, simu nyingi kutoka nyumbani kwake zilikuwa zikipigwa! Yeye hakusikia! Simu alikuwa anaiweka mitetemo, kwa hiyo ikiita huwa haitoi sauti zaidi ya kutetemeka. Na sehemu aliyoiweka ilikuwa hairudishi mitetemo kiasi cha kusikika.

Alipomfikisha hospitalini, habla daktari hajashuka, akagundua kwamba simu yake inazimika mwanga – maana yake iliita na sasa imekata. Upesi akaichukua na kuiangalia. Akakuta dada zake wote walimpigia wakamkosa, kaka zake walimpigia wakamkosa, shangazi, mjomba na hadi marafiki zake!

Yaani alikuta ‘miss call’ kama 25 hivi! Alishtuka sana!

Alivyomwonyesha daktari wote waliipiga na kumkosa, daktari pia alionekana kuhuzunika! Wote wakawa na mawazo yaliyofanana kuhusu nyumbani walikotoka! Kuhusu mama yake!

Mbunge akaishiwa nguvu! Akatoa na kitambaa na kujifuta machozi.

Kisha simu ya mjomba wake, ambaye yuko palepale nyumbani ikaingia.

“Mjomba anapiga!”

“Pokea… Hakuna jinsi!”

Mbunge akaipokea simu hiyo!

Alichokisikia kikamshtua!

“Mjomba mbona hupokei simu! Huku nyumbani watu tuko nje hapa tunasheherekea!”

“Mnasheherekea! Kitu gani?”

“Umeteuliwa kuwa naibu Waziri! Wote tulikupigia hapa tukupongeze, ila ukawa hupokei simu! Rudi tusherehekee!”

Hiyo ndiyo stori ya Mbunge ambayo Zaka aliikumbuka! Akavuta tabasamu!

Kwamba na yeye simu ya mke wake inaita! Amemwacha mtoto akiwa na dalili za kurudiwa na ugonjwa wake!

Je, inaweza kuwa tofauti!

Akajipa moyo na kuipokea!

Alipoipokea tu, sauti ya mkewe anayelia ilisikika!

Akashtuka!

“Mke wangu... Vipi kwema?”

“Mume wangu... Njoo!”

Zaka akatumbua macho.

“Maua... Maua... vipi kuna nini?”

Maua akaendelea kulia simuni.

“Mtoto yuko mahututi... Tupo hospitalini.”

Zaka akahisi kuishiwa nguvu!

* * * * * * * * *

Ni hospitalini.

Ukumbini watu kadhaa walikuwa wamekaa wakiuangalia mlango wa daktari.

Ziada alikuwa amekaa sambamba, hawazungumzi na jirani yake, anauangalia mlango wa daktari ambako Maua na Zaka walikuwamo.

Alikuwa anasubiri kusikia kutoka kwao!

Ni mtoto wao tu aliyebaki na daktari ndani, Zaka aliyekuwa ameishiwa nguvu alilazimika kuingia ndani kujua hali ya mwanae kwa uhakika kutoka kwa daktari.

Mlango huo wa daktari ukafunguka.

Zaka akatoka ndani huku akijifuta machozi. Kwa pupa, Ziada akainuka kutoka kwenye benchi la peke yake alilokaa, akaenda kumpokea na kumshika mkono, akamkokota hadi alipokuwa amekaa, wakakaa pamoja.

“Enhe.. Zaka… Vipi huko ndani?”

“Daktari ameniambia nimwache apumzike. Nimemuacha na mama yake.”

“Dah! Lakini hali vipi, umemuonaje yaani. Mi nimeogopa sana.”

“Bado... Hali ni mbaya. Mwili bado umekakamaa na amepoteza fahamu.”

Zaka alijiinamia.

Ziada akatulia akionekana kuguswa sana.

“Ziada, na wewe alikupigia simu Maua hadi ukaja hapa?”

“Hapana shemeji... Mimi nilikuwa nafua. Nilimsikia tu mkeo anapiga makelele. Nikatoka nyumbani kwangu nikamkimbilia - ndo nikasaidiana naye mpaka tukamleta hapa – tulikupigia sana simu, ukawa hupatikani kwenye simu muda mrefu - tuliogopa sana.”

Zaka akajifuta machozi.

“Simu yangu haikuwa na chaji. Yaani mtoto wangu anavyoteseka vile - Mungu akimrudishia nguvu akarudi kwenye hali yake. Naapa. Ntapambana kwa nguvu zangu zote kuhakikisha anapatiwa vipimo na anatibiwa.”

Ziada akamtazama kwa huruma!

Ziada alikuwa na lake, lakini alisita kuongea!

Alisita kwa sababu alikuwa akiujua msimamo wa familia hii, hasa Zaka wa kutoamini mambo ya tiba za dawa za asili.

Lakini lilikuwa kama dukuduku, na sasa aliamua kulisema, “Lakini Zaka shemeji yangu, siku nyingi nimemwambia mkeo, yupo mzee mmoja anatibia kila ugonjwa. Yuko kijijini, anaitwa Mzee Zimataa. Ana uwezo mkubwa, alishamsaidia mama yangu. Wakati mnahangaikia pesa za vipimo na matibabu, bora tumpeleke kule.”

Zaka akatulia kidogo akipisha maneno yale yaingie vizuri akilini.

Ni kama aliyekuwa anayatafakari.

Ziada naye kwa kulijua hilo akanyamaza pia, akamwacha ashauriane na halmashauri ya kichwa chake, pengine jibu litapatikana.

Zaka akainua kichwa, “Nakumbuka... hata mimi uliniambia. Na kwa hali ilipofikia, ni kweli sasa hakuna jinsi. Kama unavyosema, wakati huu ambapo tunahangaikia pesa, itabidi uende na mwenzako mkajaribu.”

Ziada akapata nguvu.

“Sio kujaribu ni kutibiwa shemeji. Au huamini tiba za asili?”

“Iwe naamini au siamini. Hii hali inabidi kujaribu kila tiba. Siwezi kupuuza chochote kwa sasa. Inabidi niwe msikivu. Hizo dawa za asili zinatibu watu, hilo najua. Ila kwa sababu mimi sijawahi kutibiwa na dawa hizo, ndio maana nasema tukajaribu!”

Kutoka kwenye chumba cha daktari, Maua naye akatoka akitembea kwa kupepesuka. Kwamba hana nguvu za kutosha! Pengine kutokana na majonzi na wasiwasi ambao alikuwa ameulimbikiza kwenye akili yake.

Zaka na Ziada wakainuka na kumpokea. Wakasaidiana kumkokota na kumpeleka kwenye benchi, wakakaa naye kwa kumuweka kati. Wakamtazama kwa shauku. Kila mmoja akitaka kujua cha mwisho ambacho amekipata kutoka kwa daktari.

“Nataka kusikia – vipi, ameamka?”

Maua akajifuata machozi na kujitahidi kurudi kawaida.

“Ile sindano imesaidia, polepole mwili wake umeacha kukakamaa na ametingisha mguu!”

Moyo wa Zaka ukatulia. Angalau amepata habari ambazo alitamani kuzisikia.

“Hiyo ni habari njema sana... Hapo ni hatua nzuri - ataamka. Oh! Mungu...” Akainua mikono juu kushukuru, “nakushukuru Mungu wangu kwa kumuokoa mwanangu.”

Lakini bado Maua alionekana kuwa mnyonge. Habari za kutia matumaini kama hizo zilipaswa kumpa nguvu kama alizopata Zaka mumewe.

Kwa uzoefu wao kwenye ugonjwa huo hali ya kukakamaa inapoondoka, inamaanisha mgonjwa atarudi kwenye hali ya kawaida muda si mrefu.

Inaendelea...