Kibu, Tshabalala wamkuna Ferooz, starehe imeniachia makovu ya chuki

Muktasari:

  • Pita kila mtaa ulikuwa unasikia wimbo huo iwe kwenye sehemu za starehe au hata kwenye madirisha ya magheto ya vijana mwendo ulikuwa Starehe.

MWANZONI wa miaka ya 2000, chati zote za muziki kwenye redio za Tanzania ngoma namba moja ilikuwa Starehe.

Pita kila mtaa ulikuwa unasikia wimbo huo iwe kwenye sehemu za starehe au hata kwenye madirisha ya magheto ya vijana mwendo ulikuwa Starehe.

Achana na hiyo, kuna ngoma nyingine iliitwa Bosi. Kuna Kamanda na Barua pamoja na Jirushe Muziki - ulikuwa muziki na tungo zilikuwa tungo.

Lakini, unamfahamu mtu huyo aliyekuwa akitamba na ngoma hizo. Kwa vijana na miaka ya karibu watakuwa hawamjui vizuri, lakini jamaa anaitwa Feruz Mrisho na mtaani alifahamika kwa jina la Ferooz, lakini yuko wapi kwa sasa?

Ferooz buana maisha yake kwa sasa ni Sinza Kwa Remmy, Dar es Salaam na ni mzima wa afya tele ambapo Mwanaspoti lilipata fursa ya kupiga naye stori mbili tatu akazungumzia mambo mbalimbali ikiwemo maisha yake na ukimya wake juu ya muziki uliompa umaarufu. Kwenye muziki Ferooz anasema bado yupoyupo sana na hawezi kuacha japo  kuna skendo za madai ya kutumia madawa ya kulevya na kumsababishia ugumu wa kupata kazi na ukimya alionao kwenye muziki kwani kuna dili nyingi zinamhitaji anazikosa kutokana na tuhuma hizo anazodai kuwa siyo za kweli akisisitiza kwamba hakuwahi na hatatumia dawa hizo.

Ferooz anasema hata hali ya maisha aliyonayo sasa ni ya kujitafuta na wengine hudhani hayupo duniani na sitofahamu zote husababishwa na uzushi jambo ambalo linamuumiza katika maisha yake na halitakuja kumtoka kichwani mwake.

“Unajua wapo watu special kwa ajili ya kukuharibia CV yako bila hata ya mwenyewe kujua ama kufahamu imetokea wapi habari mbaya juu yako. Hakuna kitu kinachoniumiza hadi leo hii skendo ya  kutumia dawa za kulevya, acha leo niseme tu  kwani sikuwahi  kuzungumza sehemu yoyote jinsi gani hii skendo imenipotezea mwelekeo na kusababisha kukosa kazi za maana ama dili kwa baadhi ya watu kwa kunihofia ni  (mtumiaji) wa hayo madawa

“Nadhani watu wanavyodhani ama huenda hata kuwaona baadhi ya wanamuziki wa miaka yetu wapo wahanga wa matumizi wa dawa za kulevya sasa imekuwa ndio tunaingizwa na wengine  ambao hatuna hata hatia,” anasema Ferooz

Nyota huyo anasema kuna mpango anauweka sawa na anajiandaa kutoa wimbo mkali kama aina ya Starehe wenye ujumbe mujarabu ambao ulimsababishia kuchukiwa na baadhi ya wapenda starehe kutokana na kuambiwa amewagusa kwenye maeneo yao na kuonekana ni vicheche.

Ferooz anasema wimbo wa Starehe kuna baadhi ya watu wanajua ameshafariki dunia wakimhusisha pengine na ‘kutendea haki’ mashairi na video na kuna wakati aliwahi kukutana na mashabiki wake Mbagara jijini Dar es Salaam wakaanza kumshangaa kuwa bado kwamba yupo hai. “Nina mpango wa kutoa wimbo wa aina ya Starehe ambao ulisababisha nimechukiwa na baadhi ya wanaopenda starehe kusema nawadhalilisha, wanaonekana ni vicheche na waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi.

“Hivyo wimbo ujao nagusa sekta nyingine mbali na changamoto zote hizo nilizonazo, najitahidi kupambana na kufosi hadi kieleweke na nina imani wimbo utakuwa ni zaidi ya starehe kwani nyimbo zangu huwa nagusa matukio yanayozunguka jamii kama elimu, watoto, wazazi. mapenzi, unyanyasaji, usaliti ofisini na vitu vingine,” anasema.

“Kiukweli wimbo wa Starehe kwa jinsi nilivyoutendea haki hadi leo nikipita mitaani watu wanadhani nimefufuka eti nilikufa na ugonjwa wa Ukimwi kwani  kipindi naimba wimbo  ule  nilikuwa naumwa ugonjwa huo. Kuna siku nilikutana na mtu Mbagara akanishangaa ‘live’ kuwa bado nipo hai kumbe tena nina afya tele, alidhani nimefariki na ugonjwa wa ukimwi.”

ZAMANI NA SASA

Ferooz ambaye katika ngoma zake zote alizowahi kuimba anaikubari sana Jirushe anasema wasanii wa zamani wanao wakati mgumu sana mitaani kwa sasa na kila wanapojitahidi kurudi kwenye gemu ya muziki wanakutana na wasanii wa sasa wenye kupiga na kuimba nyimbo zenye mahadhi ya amapiano, ambayo wao enzi zao hayakuwapo na waliishi katika kuimba kile kinachoizunguka jamii.

“Nikizungumzia wasanii wa zamani tuna wakati mgumu sana huko mtaani na hata ukijaribu urudi katika muziki unakutana na wasanii wa sasa wenye kupiga sana amapiano na nyimbo za mapenzi za “nakupenda... nakupenda” hata hawaoni mambo yanatotokea kwa jamii wayakabili vipi kwa kufikisha ujumbe kupitia sanaa yao ya  muziki,” anasema mkongwe huyo.

KAMA SI MUZIKI

Kama isingekuwa muziki, Ferooz anasema angekuwa anatetea jamii kwa kuiongelea juu ya changamoto inazokutana nazo, lakini hilo aliliweka kando na kuamua kubaki akifikisha ujumbe kupitia tungo zake

“Napenda kudadisi mambo. Napenda kufanya uchunguzi wa mambo napenda. Napenda kutatua matatizo ya kijamii, sipendi kuona manyanyaso ndio maana kama unanifuatilia nyimbo zangu mimi zina ujumbe unaobeba jamii.”

SHABIKI WA SIMBA

Nyota huyo wa Bongofleva anasema kwenye soka anapenda kuishangilia na kuifuatia timu ya Simba kwa kuwa iko ndani ya damu yake.

“Mimi ni shabiki wa Simba nisiyekata tamaa na nimeshawahi kwenda uwanjani mara kadhaa na katika timu huwa nawakubali sana wachezaji wanaofanya vizuri na kuipa ushindi timu yetu. Ila kuna huyu Kibu Denis, Mohamend Hussen na Mzamiru huwa wananikosha sana,” anasema.

KWA WASANII SASA

Ferroz anawapenda wasanii wanaozungumzia ishu zinazoikabili jamii kwa sababu vipaji walivyo navyo wamepewa ili kuitumikia. “Nawakubali wasanii wanaoimba nyimbo zenye kufikisha ujumbe wa matatizo ya jamii. Nyimbo zinazoweza kuishi kwa miaka yote na sio tu msanii anaimba nyimbo haieleweki au wimbo unavuma kwa muda anapoteza. Mfano mzuri kuna wasanii wa zamani sisi ukiangalia baadhi ya nyimbo zetu zinaishi hadi leo

“Na produzya ninayemkubali pia awe mvumbuzi wa mambo. Awe muongozaji vyema wa mwanamuziki sio yule wa kuchukua hela na bora ngoma iende mtaani. Mimi buana hadi kufika hapa namshukuru sana P Funky Majani ndio aliyenitoa kimuziki na sitaacha kumpa heshima yake kila wakati.”

Watu wengi wanataka kujua Ferooz ni mtu wa namna gani, lakini hapa anaelezea alivyo: “Ferooz ni mtu mmoja mpole sana sina makuu, yaani kiufupi nimepoaaa, msikuvu sana na napenda kujishusha sio mgomvi, mcha Mungu na napenda amani na ndio maana kipindi navuma kwenye gemu sikuwahi kuwa na skendo za ugomvi na hata kama ugomvi ukitokea, basi unakuwa ni wa papo kwa hapo wa kupishana lugha na unaisha.