JICHO LA MWEWE: Maisha yameenda kasi sana kwa Djuma Shabani

Muktasari:

  • Ubora wake kule pembeni katika beki ya kulia pale AS Vita ikaonekana Djuma hawezi kucheza mpira Tanzania. Kumbuka wakati huo pia alikuwa anacheza timu ya taifa ya Congo. Kwa kile kiwango chake ilikuwa inaonekana Djuma angeenda Al Ahly au Wydad Casablanca au kwingineko kule Afrika Kaskazini.

NYUMA ya pazia katika stori ambayo inasisimua sana ni namna ambavyo Yanga walimpata mchezaji anayeitwa Djuma Shabani kutoka AS Vita ya DR Congo. Yanga walilazimika kupitia njia nyingi za panya kumpata Djuma. Alikuwa keki ya moto kwelikweli.

Ubora wake kule pembeni katika beki ya kulia pale AS Vita ikaonekana Djuma hawezi kucheza mpira Tanzania. Kumbuka wakati huo pia alikuwa anacheza timu ya taifa ya Congo. Kwa kile kiwango chake ilikuwa inaonekana Djuma angeenda Al Ahly au Wydad Casablanca au kwingineko kule Afrika Kaskazini.

Injinia Hersi Said akasafiri kwenda hadi Congo kumfuata Djuma wakati huo akijaribu kuitengeneza Yanga mpya ambayo wakati huo pia ilikuwa inamuona Kibwana Shomari kama vile anatosha katika nafasi yake katika jezi za njano na kijani. Ilionekana kama vile ni ndoto ya kijinga tu kutoka kwa Msomali wa Yanga.

Na kweli. Simulizi nzuri ya namna ambavyo Yanga walimpata Djuma inaelezea namna ambavyo Injinia Hersi Said alipata moja kati ya nyakati ngumu kusajili mchezaji katika zama hizi ambazo Yanga wanamuona shujaa wao. Alipambana haswa. Inadaiwa kwamba kila kitu kilikwenda ovyo mpaka simu muhimu zaidi kutoka Tanzania.

Congo mchezaji anaweza kumilikiwa na timu. Anaweza kumilikiwa na mtu binafsi. Anaweza kumilikiwa na wakala. Anaweza kujimiliki yeye mwenyewe. Djuma alikuwa anamilikiwa na mmoja wa wakuu wa majeshi pale Congo. Diplomasia ililazimika kuingilia kati. Mkuu mmoja wa zamani hapa nchini akapiga simu Congo kutoa maelekezo Injinia Hersi Said asaidiwe.

Ni hapo ndipo Yanga wakafanikiwa kumpata Djuma. Nakumbuka rafiki yangu mmoja kiongozi wa watani wa Yanga, Simba aliwahi kunipigia simu akiniambia; “Huyo Hersi anajisumbua tu Djuma hawezi kucheza Tanzania. Yanga sio level zake arudi tu nchini kupata wachezaji wake wa bei rahisi.”

Miezi 24 tu baada ya kauli yake, leo Djuma Shaban anakaribia kucheza Coastal Union ya Tanga. Mchezaji ambaye ilionekana hata Yanga sio hadhi yao kutokana na ubora wake leo anakaribia kucheza Coastal ya Tanga. Hivi ndivyo ambavyo maisha yamekwenda kasi kwa Djuma Shabani. Nini kimemtokea? Hatuelewi. Labda alikuja nchini wakati akianza kushuka kisoka.

Alipotua alionekana kuwa mzito. Ikasemwa akiwa fiti atakuwa bora zaidi. Tukamsubiri awe fiti lakini haikuwezekana. Hakuwahi kurudi kuwa yule Djuma Shabani tuliyemfahamu. Tofauti pekee na mabeki wengine wa kulia ni uamuzi wake wakati akiwa katika kibendera cha kona. Hata hivyo, katika maeneo mengine alikuwa anaonekana anachezea zaidi uzoefu.

Wakati mwingine nilikuwa namuona Djuma kama mchezaji anayeudharau zaidi mpira wetu. Alikuwa anataka kucheza bila ya kutumia nguvu nyingi. Sawa, akili ya mpira anayo lakini alikuwa hapendi purukushani za mara kwa mara uwanjani. Kama tabia hii alikuwa nayo mazoezini pale Kigamboni basi ndio maana alionekana kuongezeka uzito mara kwa mara hasa katika nchi hii ambayo ina starehe nyingi.

Mwishoni mwa msimu uliopita Yanga waliamua kuachana naye. Inatajwa kwamba yeye na Mcongo mwenzake, Yannick Bangala walionekana kuwa kama virusi katika kambi ya Yanga. Kwamba walikuwa wanaongoza migomo ya chini kwa chini ya wachezaji dhidi ya uongozi, hasa ilipokuja katika masuala ya fedha. Yanga wakaamua kuachana nao huwa mashabiki wakiwa hawana uhakika kama ulikuwa ni uamuzi sahihi.

Uamuzi huo uliwashangaza wengi lakini ulikuja kuonekana kuwa halali pale Yanga ilipomsajili Yao Kouassi. Yao amepiga kazi kubwa katika nafasi hiyo kuliko Djuma. Wakati mwingine uamuzi wa viongozi au makocha huwa unanusurika kwa namna hii. Ni pale tu mbadala atakapopiga kazi zaidi.

Kuanzia hapo Djuma alijikuta katika kambi ya Azam FC. Wengi tuliamini kwamba huenda Azam walikuwa wanasubiri dirisha dogo au hili kubwa ili wamchukue. Nadhani lilikuwa lengo lao hadi pale walipomtazama Djuma kwa karibu zaidi mazoezini. Nadhani wameona wazi kwamba Lusajo Mwaikenda na Nathaniel Chilambo wapo hatua nyingi mbele ya  Djuma. Wameamua kumtosa Djuma.

Ni wazi kwamba Azam wanatuthibitishia kwamba uamuzi wa Injinia Hersi Said kuachana na Djuma ulikuwa sahihi. Ni nadra sana Simba na Yanga kumuachia huru mchezaji ambaye ni mzuri. Ni kama Simba walipomuacha Haruna Niyonzima na Yanga wakadhani Simba wamefanya makosa. Aliporudi katika kipindi chake cha pili alikuwa mchezaji wa kawaida sana na Yanga wakaamua kumtema moja kwa moja.

Na sasa Djuma anaangukia Coastal. Nilimuuliza kiongozi mmoja wa timu hiyo ya Tanga kama habari hii ina ukweli akanijibu kwa Kiingereza cha Fabrizio Romano ‘its almost a deal done’. Hatimaye huko ndiko ambako Djuma ameangukia. Sio Zamalek, Al Ahly, Wydad wala Mamelodi Sundowns ambako yule kiongozi wa Simba aliamini kwamba angeweza kucheza katika hadhi yake na sio Yanga.

Azam wamemkwepa na hata Simba ambao waliona gere wakati Yanga wanamchukua Djuma nao wamemkwepa katika dirisha hili. Nadhani Djuma sasa ataingia katika mkumbo wa wachezaji kadhaa wa kigeni wanaoongozwa na Obrey Chirwa na Meddie Kagere ambao walitua nchini wakiwa na hadhi kubwa lakini sasa hivi wanahaha kucheza katika timu za kawaida za mikoani.

Sijui kama ataweza kurudisha kiwango chake kile cha AS Vita na kuzitamanisha timu kubwa za Dar es Salaam zimchukue tena. Kuna wachezaji wachache wa Tanzania waliofanikiwa kuibukia timu ndogo baada ya kutemwa na timu kubwa, kisha wakacheza mpira mwingi na kurudi tena timu kubwa. Hassan Dilunga, Amri Kiemba na Saido Ntibazonkiza ni kati ya waliowahi kufanya hivyo.

Lakini labda michuano ya Shirikisho inaweza kumrudisha Djuma katika ubora wake na akajikuta akiangukia katika klabu nyingine za nje. Hauwezi kujua. Inategemea tu na akili yake ilivyo kwa sasa. Sisi mashabiki tunabaki kushangaa tu kitu kilichomtokea ndani ya miezi 24 iliyopita.

Kutoka katika vita kubwa ya kuipata saini yake kutokea Congo hadi kupiga penalti muhimu katika fainali ya Shirikisho dhidi ya USM Alger, leo anaangukia Coastal katika kipindi kifupi tu nadhani maisha ya Djuma Shaban yanabakia kuwa kielelezo dhairi cha namna maisha yanavyokwenda kasi. Miezi 24 tu Djuma ameanguka kutoka kuwa mfalme hadi kuwa raia wa kawaida tu.