Kwenye soka pele, ngumi kuna ali, kriketi yupo

Muktasari:

  • Ameitangaza vyema nchi yake na kuipa heshima kubwa kimataifa akiwa mchezaji wa kriketi maarufu miaka ya 1980.

Garfield (Gary) Sobers. Moja ya majina makubwa sana katika Kisiwa cha Barbados ikiwa ni zaidi ya miaka 40 anaimbwa na kila mtu.

Ameitangaza vyema nchi yake na kuipa heshima kubwa kimataifa akiwa mchezaji wa kriketi maarufu miaka ya 1980.

Sober ni jina lililoingia kwenye ukurasa maalumu wa miamba ya mchezo huo duniani waliofanya mambo ambayo hayakutarajiwa na yanayohesabika kama historia katika mchezo huo.

Katika lugha ya Kiingereza mtu ambaye ni makini na mwenye busara anaitwa ‘sobers’ Wataalamu na mashabiki wengi wa kriketi duniani wanasema hadi leo hakuna kama Sobers  katika mchezo huo, kama ilivyo kwa Pele wa Brazil katika soka na Muhammad Ali wa Marekani katika ndondi.

Sasa akiwa na miaka 86 bado anakumbukwa kwa kuumudu mchezo huu kwa kila hali kati ya mwaka 1952 hadi 1974.

Ni mchezaji aliyesifika kwa kuwa makini katika mchezo kama lilivyo jina lake.

Utafiti uliofanywa nchi mbalimbali katikati ya miaka ya 1960 ulionyesha zaidi ya asilimia 15 ya vijana waliijua nchi inayoitwa Barbados kutokana na Sobers alivyotamba katika kriketi.

Kila yanapofanyika mashindano ya kimatifa, kama ya Kombe la Dunia la kriketi, jina la Sobers huchomoza kuelezea mafaniko yake.

Mwaka 1968 alifanya maajabu kwa kupata alama 36 katika mzunguko mmoja kwa kila mkwaju kupata alama Barbados ilipotembelea England na kucheza na Swansea.

Wengine wenye sifa kama yake ni Brian Lara wa Trinidan na Tobago na alipata alama 501 bila ya kutotolewa nje  katika uwanja wa Edgabston, Birmingham katika mwaka 1994 na Jim Laker wa England kwa kuchukua alama 90 kwa mikwaju 19 tu, Uwanja wa Old Traford, England, mwaka 1956.

Mwaka 2023 katika zoezi la sensa ya watu na makazi na utafiti uliofanyika huko Barbados, watu waliulizwa kama wangekuwa na zawadi za thamani za kuukaribisha mwaka mpya wangempa nani, zaidi ya robo tatu walisema Gary Sobers.

Utafiti mwengine ulionyesha watu wa kisiwa hicho chenye wakazi  300,000, wanajua zaidi habari Sober kuliko viongozi wa nchi akiwamo Waziri Mkuu wao, Mama Mia Amor Mottley,  ambaye yupo madarakani kwa mwaka wa sita sasa.

Aliiongoza timu ya visiwa hivi vya Carribean vilivyokuwa vikijulikana kama West Indies na hata timu ya dunia akiwa nahodha na kuelezwa kama mfano mzuri wa kuigwa na wachezaji wengine.

Licha ya sifa alizopata na kutunikiwa zawadi na wafalme na wakuu wa nchi nyingi, Sobers aliyetunukiwa heshima ya ‘Bwana mkubwa’ (Sir) na Malkia Elizabeth wa Uingereza.

Sobers aliwaheshimu wachezaji wenzake, mashabiki na hata watoto wadogo waliolilia saini yake kama kumbukumbu.

Majirani zake wanasema milango ya nyumba yake siku zote ipo wazi kwa watoto na wengine huwafunza kriketi katika uwanja mdogo wa nyumbani kwake hata nyakati za usiku.

 Siku hizi anatambulika kama balozi wa nchi yake na wa mchezo wa kriketi duniani na ni kawaida kualikwa katika mashindano ya kimataifa ya kriketi.

Pia anatumia muda mwingi kuitangaza taasisi iliyopewa jina lake iliyopo New York, Marekani, inayokusanya pesa kuwasaidia vijana chipukizi wa mchezo huo.

Wakati alipokuwa uwanjani Sobers mara nyingi  alifanya maajabu yaliyobadili sura ya mchezo na kuipatia West Indies ushindi hata palipokuwa hapana matumaini.

Alipokuwa akipiga mpira alikuwa hashikiki na hatabiriki mipira yake aliyoirusha wakati alipokuwa akidima, hasa ile inayozunguka (spinning balls),  ilikuwa moto.

Namna livyoongoza timu kama nahodha, hasa wakati ilipobanwa, ni mfano mzuri wa kuigwa na nahodha yoyote yule katika kriketi.

Alikuwa stadi wa kudaka mipira pembezoni mwa wiketi (vijiti vitatu viliosimama vinavyosakwa kugongwa) ili mchezaji atolewe nje.

Alikuwa mwepesi kurukia na kudaka mipira iliyopigwa ‘kimo cha mbuzi’ na hii kusababisha gazeti moja la Uingereza kumuita ‘Nyani wa Carribbean’.

 Kuna wakati ilikuwa kawaida kufikiria amedaka hewa, lakini kila alipovua kofia kwa mkono mmoja kila shabiki alielewa  mkono wa  pili ulikuwa na mpira.

Sobers aliyezaliwa na vidole sita kila mkono na kulazimika kupunguzwa mikono yote ni mcheshi na mara nyingi watu huvutiwa na hadithi zake za mikasa.

Maumbile yake ya kuzaliwa na vidole sita kila mkono yalizusha mzaha wa kueleza ndiyo maana alipenda kukumbuka utoto wake kwa kupiga mipira ya alama sita.

Vile vile aling’ara katika riadha, gofu, soka na mpira wa kikapu, mchezo alioumudu vizuri na kuchaguliwa katika timu ya West Indies akiwa na miaka 16.

Miongoni mwa rekodi zake za kupiga mipira katika kriketi ni kucharaza mikwaju ya alama 365 Barbados ilipocheza na Pakistan  1972.

Siku aliochukua pointi zote 36 kwa mipira sita inajulikana hadi leo Barabaos kama Siku ya Sobers na husherehekewa nchi nzima.

Kama wachezaji wengi wa West Indies wa wakati ule na sasa, Sobers alicheza kwa muda mrefu  nje ya nchi yake kama mchezaji wa kulipwa.

Kwanza alikuwa na Nottinghamshire ya Uingereza na baadaye klabu moja ya Australia.

 Malkia Elizabeth wa Uingereza alimtunukia heshima ya Sir(Bwana mkubwa) mwaka 1975 kwa mchango wake uliotukuka katika kriketi.

Katika ujumbe wake wa kumtunuku Sobers Malkia aliuliza: Nani kama Sobers? Jawabu ilikuwa fupi, “Hakuna”.

Mwaka 1998, Barbados ilimtangaza shujaa wa taifa na vyama vingi vya kriketi vilimpa tuzo za vitu vya thamani.

 Wapo wanaoamini hatakuwepo mtu kama Gary Sobers katika kriketi, kama alivyouliza na kujibiwa Malkia Elizabeth.

Karne ya 20 ilipomalizika Sobers alichaguliwa mmoja wa wachezaji watano bora wa karne wa mchezo wa kriketi.

Sobers alizaliwa Barabados tarehe 28 Julai, 1936 na kukulia katika vichochoro vya Bay Land alipoanzia kucheza kriketi katika viwanja vya mchanga na changarawe. Alipanda na kuwa nahodha wa kudumu wa West Indies.

 Mchezo wake wa kwanza wa kimataifa ulikuwa kutoka Machi 30 hadi Aprili 3, 1954 West Indies ilipopambana na Uingereza kule Jamaica na wa mwisho uliowatia simanzi mashabiki duniani ni wa West Indies na England  uliofanyika Port of Spain kutoka Machi 30 hadi Aprili 3, 1974.

Mwisho wa mchezo baadhi ya mashabiki walibubujikwa na michezo na kusikika wakipiga kelele; “Sobers usitukimbie”. Naye alijibu atakuwa pamoja nao, lakini sio uwanjani.

Alipostaafu, Sobers alikuwa bado anaumudu vizuri mchezo, lakini alisisitiza umri ulimwambia jua limekuchwa na hakutaka atolewe uwanjani kwa machela ndio aseme anapumzika.

Siku zote Sobers amesistiza kutoamini ushirikina na kuchukizwa na wanaofikiri hiyo inaweza kuwapatia ushindi na kutoboa siri siku moja aliwafukuza wachezaji wake wawili baada ya kugundua wanafanya ushirikina.

Amekuwa akiwataka vijana kupenda kriketi kwa vile unamfinyanga mtu kuwavumilia wachezaji wenzake na wapinzani.

Alisema uvumilivu unaokosekana miongoni mwa watu na nchi nyingi ndio sababu ya dunia kuwa na matatizo.

Jambo linaloshangaza ni Sobers tangu akiwa mdogo amekuwa hapendi kuangalia mchezo wa kriketi na alipotakiwa aeleze kwa nini alifanya hivyo alisema siku zote amefurahia kucheza na sio kuwa mtazamaji.

 Alisema Wamarekani hawawezi kupendaa kriketi kwa sababu tabia yao ni watu wanaopenda mambo ya haraka na hili linaonekana hata kwa aina ya vyakula vyao, kama chipsi.

 Alipoulizwa anaonaje mchezo wa kriketi ulivyo sasa na zama zake,  alisema hilo anawaachia watazamaji walizungumzie, lakini alikuwa na uhakika kwamba ushabiki wa wakati ule ulikuwa umetokana na mapenzi ya moyoni ya timu na sio kugombania fedha na zawadi kama ilivyo sasa.

 Garfield  Sobers ni mchezaji mbaye hatasashaulika katika kriketi. Nani kama Gary Sobers? Hakuna!

 Linalobakia kuulizwa ni jee mchezo huu utampata Sobers namba mbili.

Wakati ndio utatoa jawabu.