Simu ya Popat ilivyomrudisha Adam Adam Azam FC

Muktasari:

  • Kama kuna mambo ambayo alitamani yatokee na sasa anachekelea, ni kurudi Azam baada ya kuishia timu ya vijana ya Azam B.

STRAIKA Adam Adam tayari ametua Azam FC kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano mbalimbali ya Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika, Kombe la Shirikisho la FA na mengine itakayoshiriki klabu hiyo tajiri zaidi Tanzania.

Kama kuna mambo ambayo alitamani yatokee na sasa anachekelea, ni kurudi Azam baada ya kuishia timu ya vijana ya Azam B.

Haikuwa kazi rahisi kurudi lakini anasema simu moja tu ya Abdulkarim Amin ‘Popat’ ilitimiza ndoto yake hiyo na sasa anasubiria kuanza kazi.

Nyota huyu ambaye anaishi kwake Bunju A, anasema amepitia mengi ikiwamo magumu kwenye soka la kulipwa alikokuwa akikipiga Libya na alivyoamua kurudi licha ya mshahara mzuri aliokuwa akipokea Al-Wahda ya Tripoli.

Pia anazungumzia maisha yake kwa jumla ni mtu wa aina gani na mengi aliyopitia nje ya soka.


SIMU YA POPAT

Anasema aliyefanikisha dili lake la kurudi Azam ni Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Abdulkarim Amin ‘Popat’.

“Alinipigia simu na kunieleza kocha anahitaji niwe miongoni mwa wachezaji wake kwa msimu ujao, sikusita kwani ni timu ninayoipenda kutoka moyoni.”


AZAM IKO MOYONI

Anasimulia licha ya kwamba alikuwa timu nyingine, lakini akicheza na Azam na kuifunga alikuwa anaumia sana kwa sababu ni timu ambayo anaipenda sana, hata hivyo anasema hakukuwa na namna kwa sababu alikuwa anatafuta maisha na soka ni ajira.

“Nimerejea Azam kwa mara nyingine, hivyo ni timu ambayo naipenda, hata wakati nacheza timu nyingine ilikuwa ikifungwa nilikuwa naumia, ingawa nimewafunga sana.”


MKATABA NI MWAKA TU

Anaelezea tabia yake ya kusaini mwaka mmoja na kila timu amekuwa akifanya hivyo na kukiri si jambo analolipenda.

Anasema anatamani awe anasaini mkataba wa miaka miwili au mitatu lakini mara nyingi amekuwa akisaini mwaka.

“Nawaambia marafiki zangu kina Metacha Mnata, Juma Makapu, natamani itokee nipate timu ambayo tutaelewana vizuri, nicheze misimu mitatu ama miwili, ila sijabahatika na hilo,” anasema straika huyo ambaye hata Azam amesaini mkataba wa mwaka mmoja.


ATIMIZA NDOTO ZAKE KWA FEI

Msimu wa 2020/21 akiwa na JKT Tanzania, anasema walicheza dhidi ya Yanga, baada ya kumaliza mechi alimfuata aliyekuwa kiongo wa Wanajangwani, Feisal Salum ‘Fei Toto’ akamwambia siku akicheza naye pamoja atafunga mabao mengi sana.

“Nashukuru ndoto yangu inakwenda kutimia kucheza na Fei Toto, ana kipaji cha hali ya juu, kuichezesha timu, kutoa asisti na kufunga. Mkiwa na mchezaji kama huyo kwenye timu haiwezi kukosa kufunga mabao. Baada ya kusikia nimesaini Azam alinipigia na akasema sasa tufanye kazi,” anasema.


KILICHOMKUTA LIBYA, KURUDI TANZANIA

Anasema wakati anaichezea Al-Wahda ya Tripoli ya Libya, maisha ya nchi hiyo yalimfanya akose amani na aliwaza watoto wake wataishije endapo atafia huko.

“Picha lilianza niliposhuka uwanja wa ndege wa Libya nikawekwa selo kama saa moja hivi, ndipo akaja anayenipokea kwenda kujiunga na klabu hiyo, niliwaza mengi sana.

Anaongeza “Kuna siku lilitoka tangazo asionekane mtu saa 10:00 jioni nje ya nyumba yake wala barabarani, nyumba ambayo nilikuwa naishi tulikuwa na wachezaji kutoka mataifa mengine, hivyo tukapigiana simu tukashuka hadi pembeni kulikuwa na msikiti, tukashangaa wanajeshi wapo na silaha, wakatukamata, uzuri wakagundua sisi ni wageni wakatuacha.”

Anasema ilibidi atumie uongo ili arejee Tanzania na aliwaambia viongozi wa klabu mama yake ni mgonjwa kazidiwa na anatakiwa afanyiwe upasuaji.

“Nikampanga mama ili waandike ujumbe wa kuumwa na kutaka kufanyiwa upasuaji, wakaniambia tutakupa pesa watumie, halafu tutakupa siku saba, ujitafakari kama bado una msimamo wa kurejea kwenu.

“Baada ya siku mbili, nikarudi tena kuwaambia na nikampigia wakala wangu alikuwa anaishi Uturuki, akaja hadi Libya kuzungumza nao, sasa nilipoona wanasuasua nikatoroka kwenda uwanja wa ndege, nilirudishwa mara tatu zote nilizofanya jaribio hilo, baadaye wakaniruhusu, mwaka huu kabla ya kusaini Azam walinitumia ofa tena.

“Mshahara wangu kwa mwezi nikiwa Libya nilikuwa napokea zaidi ya Sh13 milioni, hivyo pesa za matumizi nyumbani nilikuwa natuma Sh5 milioni, pamoja na hayo yote niliiona amani ni kitu muhimu zaidi,” anasema.


KUFIKA HAPA HAIKUWA RAHISI

Anasema mama yake alikuwa anafanya biashara ya ‘mama lishe’ na walizaliwa wawili ambapo mdogo wake alitangulia mbele ya haki, mateso aliyokuwa anayaona kwa mzazi wake yalimfanya ajitume kupata maisha mazuri.

“Kwanza niliwahi kufanya kazi ya seremala, hivyo naweza nikatengeneza vibanda, niliendesha bodaboda, kuna siku rafiki yangu alinipa ishu ya kupata pesa ya kubeba mizigo ya wazungu kwenye Mlima Kilimanjaro.

“Ilikuwa ni dili la siku (Porter), nilibeba gesi, kuku na soseji, mlima unauzunguka awamu ya kwanza nikapanda chapu ya pili nikachoka hadi nikafika hatua nikaitupa gesi chini, ikaanza kushuka kwenda chini zaidi, nikawaza hapa napaswa kushuka nitajilipa hizo soseji na kuku.

“Nikawa naongea kwa nguvu kama vile nipo na mtu, huku nikiwa na uchungu mkubwa, baadaye nikajipa moyo, ikabidi niifuate gesi ambayo iliserereka chini, mara akaja rafiki yangu ambaye alinipa dili kunisaidia, yeye akabeba gesi, mimi nikabeba kuku, nilipomaliza hiyo kazi nikapewa Sh50,000, nilipofika geto nikaiweka kwenye droo kama siku tatu nikawa naiangalia tu, nikaapa sihitaji umaskini katika maisha yangu.

“Nilipoona kipaji changu cha soka ni kikubwa, nikaamua kuweka nguvu huko, ndio maana najituma kwa bidii, ili kuwaandaliwa maisha mazuri watoto wangu na mama.”


MSIKATE TAMAA

Anasema binadamu hatakiwi kukata tamaa, pindi anapokuwa anajitafuta akiamini bidii ndiyo kila kitu.

Anasema kuna wakati mwingine mtu anaweza akapitia hali ngumu akaamini inaweza ikaishi milele, lakini anawapa somo la uvumilivu.

“Angalau nimejipata, sina maana ni tajiri, lakini kwa historia ya maisha yangu, nimetoka maisha ya chini sana. Kuna wakati nilikuwa najua sitakaa nione mwanga wa kiuchumi katika maisha yangu, ila kuna siku niliwaza kwa sauti, sitaki umaskini na nitapambana usiku na mchana ili watoto wangu waje kuishi maisha mazuri,” anasema.


BOCCO NAMBA NYINGINE

Katika washambuliaji anaowakubali wazawa, alimtaja John Bocco anayetajwa anakwenda kujiunga na JKT Tanzania kama kocha mchezaji baada ya kuachwa Simba.

“Nimecheza naye Azam, nikiwa kikosi B, alikuwa ananishangaza alivyokuwa anapigania masilahi yetu, hata baada ya kucheza timu nyingi alikuwa ananishauri kukitunza kiwango changu, kiukweli tuna kazi kubwa ya kufikia rekodi yake na haya mabao tunayofunga 10, saba, mara tisa,” anasema.


TIMU ALIZOPITIA

Timu alizocheza Adam ni JKT Ruvu, Al-Wahda Tripol, Polisi Tanzania, Mtibwa Sugar, Ihefu na Mashujaa.