Azam waipa Simba bei ya Fei Toto

Muktasari:

  • Fei Toto ambaye alitua Azam FC akitokea Yanga, alisaini mkataba wa miaka mitatu na tayari ameutumikia kwa msimu mmoja akiisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi ya pili na kupata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

SIMBA na Mamelodi Sundowns zimeulizia uwezekano wa kumsainisha mkataba staa wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’ lakini zikaambiwa hauzwi.

Fei Toto ambaye alitua Azam FC akitokea Yanga, alisaini mkataba wa miaka mitatu na tayari ameutumikia kwa msimu mmoja akiisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi ya pili na kupata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Chanzo cha kuaminika kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli vilabu hivyo viwili vimepeleka ofa mezani kuuliza uwezekano wa kumpata kiungo huyo ambaye ameifungia Azam FC mabao 19 msimu ulioisha lakini wakagonga mwamba.

Wakati suala la Mamelodi halijapoa Simba nao wamepeleka ofa wakimfikiria kama mbadala wa Clatous Chama ambaye ameibukia Yanga. Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba kimelithibitishia Mwanaspoti kuwa mabosi wamekutana na viongozi wa Azam FC kwa ajili ya mazungumzo ya kufanya biashara ya kumnunua kiungo huyo lakini hawajafanikiwa.

Mwanaspoti lilimtafuta Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ akadai thamani yaFei Toto ni Dola 5 milioni  (takriban Sh13 bilioni) ambazo kiuhalisia hakuna klabu ya Afrika inayoweza kufanya biashara hiyo kwa sasa kutokana na uwepo wa machaguo mengi kama yeye ya bei nafuu sokoni.