Babu Seya afunguka usajili wa Chama Jangwani

BABU SEYA Pict
BABU SEYA Pict

Muktasari:

  • Babu Seya, mzaliwa wa DR Congo, ambaye ameishi Tanzania kwa miaka mingi, anasema yeye ni shabiki wa Yanga tangu mwaka 1972, enzi ambazo alikuwa akimkubali sana za marehemu Gibson Sembuli, gwiji wa Yanga aliyesifika kwa kupiga mashuti makali.

MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking 'Babu Seya' amefurahishwa na tetesi za usajili kwamba huenda kiungo wa Simba, Clatous Chama akajiunga na timu ya Yanga, akisema jambo hilo likitokea timu hiyo ya wananchi itakuwa haishikiki msimu ujao.

Babu Seya, mzaliwa wa DR Congo, ambaye ameishi Tanzania kwa miaka mingi, anasema yeye ni shabiki wa Yanga tangu mwaka 1972, enzi ambazo alikuwa akimkubali sana za marehemu Gibson Sembuli, gwiji wa Yanga aliyesifika kwa kupiga mashuti makali.

"Mimi naipenda sana timu ya Yanga, mimi ni wa Jangwani bana tangu mwaka 1972, na niseme tu nimefurahishwa sana na tetesi za usajili wa kiungo wa Simba, Clatous Chama kama atajiunga na Yanga timu yetu itakuwa haishikiki," amesema Babu Seya.

Aidha, Babu Seya amesema, anawapenda wachezaji wote wa timu ya Yanga: "Siwezi kubagua nani au nani, maana leo hii nikisema nampenda Aziz KI akiondoka je? Hivyo napenda timu nzima na ndio maana nimedumu kwa muda mrefu kuishabikia timu hii."

Babu Seya amesema ndapo Chama atajiunga yanga, ataunda kikosi cha kutisha akiungana na mastaa wengine Aziz KI, Pacome, Khalid Aucho,Max Nzengeli na Prince Dube anayesemekana amemwaga wino Yanga akitokea Timu ya Azam.

"Kila mchezaji ana kipaji chake, Chama naye ana vitu vyake, ila nasisitiza lazima atafanya vizuri na kuweza kuunda kikosi cha kutisha sana akiungana na mastaa wengine Aziz KI,Khalid Aucho,Pacome,Max Nzengeli na prince Dube ambaye inasemekana amesaini Yanga akitokea Timu ya Azam"amesema Babu Seya

Aidha Babu Seya amesema,kama Chama kipenzi cha mashabiki wa Simba anaweza kuvuka upande wa pili na kutua Jangwani akawa pia kipenzi chao.