Ibenge: Huyu Chama ni mtu sahihi

Muktasari:

  • Mzambia huyo alijiunga na Yanga juzi Jumatatu akitokea Simba aliyomaliza nayo mkataba baada ya kuitumikia kwa mafanikio ikiwemo kuipeleka kwenye robo fainali za mashindano ya klabu Afrika mara kadhaa.

KOCHA maarufu kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kaskazini anayeikochi Al Hilal ya Sudan, Florent Ibenge amefafanua jambo kuhusiana na staa mpya wa Yanga, Clatous Chama.

Mzambia huyo alijiunga na Yanga juzi Jumatatu akitokea Simba aliyomaliza nayo mkataba baada ya kuitumikia kwa mafanikio ikiwemo kuipeleka kwenye robo fainali za mashindano ya klabu Afrika mara kadhaa.

Ibenge ambaye yuko Dar es Salaam na timu yake ya Al Hilal wanajinoa kwenye viwanja vya Ghymkana wakijiandaa na mashindano mbalimbali ya msimu ujao nje ya ardhi ya Sudan.

Akizungumza na Mwanaspoti kwenye mahojiano Jijini Dar es Salaam, Ibenge alimzungumzia ubora wa nyota mpya aliyesajiliwa na Yanga sambamba na kilichomkwamisha kufanya vizuri kwenye Ligi ya Morocco.

Mbali na huyo pia akitia neno kwa kiungo wa wana Jangwani hao, Stephane Aziz Ki akisema ni miongoni mwa mastaa anaowakubali sana.

Chama baada ya kufanya vizuri msimu wa 2020/21 akiichezea Simba, RS Berkane chini ya Ibenge ukavutiwa na kiwango chake na ukamsajili msimu wa 2021/2022 ambao alidumu kwa miezi sita kisha akarejea tena kwa wana Msimbazi jambo lililoibua mijadala mitandaoni kwamba alifeli.

“Chama ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa, ana ujuzi, kipaji kikubwa, hakuna kocha ambaye anaweza asitamani kuwa naye kwenye kikosi chake. Kitu kilichomrudisha Tanzania ni suala la familia yake, ikumbukwe alipoteza mkewe, aliacha watoto wake Zambia, hivyo alihitaji ukaribu na watoto wake.

“Naheshimu sana familia, nilimuelewa alivyosema anahitaji kukaa karibu na watoto wake, kama watoto hawana mama watahitaji kumuona baba yao.”

Kuhusu Tripple C kwenda Yanga, Ibenge anasema: “Kama nilivyosema Chama ni mchezaji mzuri na kwenda kwake Yanga itakuwa faida kubwa kwa timu hiyo.”

Anamtaka Azizi Ki? “Niliwahi kumhitaji wakati anachezea ASEC Memosas, lakini alichagua kwenda Yanga, kiukweli ni mchezaji mzuri na sidhani kama kuna kocha asiyemtamani, ukiwa naye ni jambo zuri katika timu.” Usikose mfululizo wa mahojiano maalum na Ibenge kwenye Mwanaspoti kesho pamoja na mitandao yetu ya kijamii.