JIWE LA SIKU: Ukishangaa ya Simba utayaona ya Tshabalala

Muktasari:

  • Pamoja na mambo yote yanayoendelea, kikubwa zaidi wanachotaka kujua mashabiki wa Simba ni mustakabali wa timu hiyo kwa msimu ujao.

SIMBA kwa sasa ipo kwenye presha. Moja haikai, mbili haikai lakini kazi inaendelea. Ni kipindi ambacho kila kitu ndani ya klabu hakina jibu la kueleweka kuanzia kwenye uongozi wa juu kabisa wa bodi, benchi la ufundi, wachezaji hadi wanachama na mashabiki. Ni kipindi cha mpito.

Pamoja na mambo yote yanayoendelea, kikubwa zaidi wanachotaka kujua mashabiki wa Simba ni mustakabali wa timu hiyo kwa msimu ujao.

Wanataka matokeo chanya uwanjani. Uongozi imara na wachezaji watakaoipambania timu hiyo kurejesha ufalme ambao kwa misimu mitatu mfululizo umeenda kwa watani wao wa jadi Yanga.

Hapo ndipo linaibuka jina la beki wa timu hiyo Mohamed Hussein. Marafiki zake wanapenda kumuita Tshabalala tangu kitambo lakini yeye kwa sasa anapenda zaidi kuitwa 'Zimbwe Jr', aliyejiunga na kikosi cha hicho mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.

Ni usajili bora uliofanywa na Simba katika muongo mmoja sasa kwani Juni 23, mwaka huu nyota huyo atakuwa anatimiza rasmi miaka 10 ndani ya kikosi hicho.

Klabu hiyo imekuwa ikisajili wachezaji wengi lakini hakuna hata mmoja aliyefikia rekodi za kiungo huyo pale Msimbazi kuanzia mataji hadi mechi za kucheza kwa waliopo sasa.

Wakati viongozi wa Simba wakiwa chimbo kutafuta mastaa wapya, wanatakiwa kumkumbuka Tshabalala kama mfano wa usajili unaohitajika pale Msimbazi. Wanatakiwa kusajili wachezaji kama Tshabalala.

Hivi karibuni atatangazwa kuwa Nahodha Mkuu wa Simba baada ya John Raphael Bocco kustaafu. Lakini Tshabalala ni picha kamili ya wachezaji wanaohitajika Simba.

Marehemu, Zakaria Hans Poppe huko aliko anastahili kupewa maua yake kwani ndiye aliyekamilisha dili la nyota huyo kutua Simba kwa mara ya kwanza.

Licha ya kwamba, Hans Poppe hayupo kwa sasa lakini Wanasimba wakimuona Tshabalala hususani kipindi hiki cha usajili wanamkumbuka zaidi Mafia yule.

Cresentius Magori, swahiba wake na Hans Poppe kwa muda mrefu, leo hii ndiye amepewa kazi ya kusimamia usajili pale Simba, atakuwa anaukumbuka sana uwepo wa Hans Poppe katika nyakati hizi.

Anayeongelewa hapa ni yule Tshabalala aliyedumu kwenye kikosi cha kwanza cha Simba kwa miaka 10 mfululizo. Ni chini ya makocha wasiopungua 15 lakini yeye aliendelea kubonda mali bila wasiwasi katika upande wa beki ya upande wa kushoto.

Kuanzia kwa Zdravko Logarusic, Goran Kupunovic, Dylan Kerr, Jackson Mayanja, Joseph Omog, Pierre Lechantre, Patrick Aussems, Sven Vandenbroeck, Didier Gomes, Pablo Franco, Zoran Maki, Roberto Oliveira 'Robertinho', Abdelhak Benchikha hadi sasa kwa Juma Mgunda, Tshabalala bado ana uhakika wa namba katika kikosi cha kwanza ndani ya Simba.

Haikuwa rahisi lakini alithubutu na kuweza, ukiachana na wachezaji viraka, katika eneo lake aliletewa washindani wa namba zaidi ya 20 lakini wote waligonga mwamba na hata wale waliothubutu kumng'oa baadaye aliwapindua na kukaa katika nafasi yake hiyo pendwa.  

Jamal Mwambeleko baada ya msimu bora akiwa na Mbao FC, alisajiliwa na Simba ili kuongeza nguvu kwa Tshabalala na ikiwezekana kumpumzisha lakini alijikuta akisugua benchi na baadaye kuondoka Msimbazi na kutimkia Stand United.

Mwingine ni Mghana, Asante Kwasi aliyejiunga na Simba mwaka 2017 akitokea Lipuli. Huyu kwa kiasi alifurukuta na kumuweka benchi Tshabalala kwenye baadhi ya mechi lakini baadaye alipoteza namba na mwisho wa yote kuondoka Simba na kujiunga na Hafia ya Guinea mwaka 2019.

Baada ya hapo Simba ilimsajili Gadiel Michael Kamagi akiwa wa moto kutoka Yanga. Kipindi hicho hata timu ya taifa Tshabalala alikuwa akisubiri kwa Gadiel lakini pale Msimbazi mambo yakabadilika kwani alisota benchi na baadaye kuamua kuondoka kujiunga na Singida Big Stars kabla ya kwenda Afrika Kusini.

Kwa sasa yupo Tshabalala amebaki mwenyewe kwenye eneo lake. Hakuna beki wa kushoto asilia ndani ya kikosi cha Simba na mara nyingi Israel Mwenda ambaye asili yake ni kulia ndiye hupewa nafasi ya kucheza eneo hilo kama Tshabalala hayupo.

Akiwa na jezi ya Simba, Tshabalala ametwaa mataji mengi ikiwemo ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nne, Ngao ya Jamii mara tano, Kombe la Mapinduzi mara mbili na Kombe la Muungano mara moja.

Pia ameisaidia Simba kufanya vizuri kwenye michuano ya CAF akiifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara nne, na robo fainali ya Kombe la Shirikisho mara moja.

Aidha, ni mchezaji muhimu katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ambapo amecheza fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) mara mbili kati ya tatu ambazo Stars imeshiriki.

Makocha Juma Mgunda na Roberto Oliveira waliowahi kumnoa Tshabalala kwa nyakati tofauti wanamzungumzia kama mchezaji mwenye nidhamu, juhudi na uelewa zaidi wa kazi yake.

"Ni mchezaji ambaye ukimwambia kitu anakifanya vyema lakini pia ni kiongozi kwa wenzake. Nidhamu yake binafsi ndiyo siri ya ubora wake," alisema Robertinho ambaye kwa sasa yuko nchini kwao Brazil.

"Ukimzungumzia Tshabalala ni mchezaji aliyekamilika. Ni beki anayejituma na kutimiza vyema majukumu yake. Ana nidhamu kubwa na amekuwa na muendelezo bora kila siku," alisema Mgunda ambaye ukiachana na Simba pia anamfundisha Tshabalala katika kikosi cha Taifa Stars.

Nyota wa zamani wa Simba Mghana, Asante Kwasi aliyewahi kucheza kwa wakati mmoja na Tshabalala alisema, moja ya siri kubwa kwa mchezaji huyo ni namna bora anavyolinda kipaji chake, kwani ni mtu wa kufanya mazoezi mara kwa mara bila ya kufuatiliwa.

"Msimu wangu wa kwanza wakati nasajiliwa Simba nikitokea Lipuli mwaka 2017, niliambiwa kabisa natakiwa kupambana kwani mtu ninayeenda kukutana naye ni bora, kwangu nikachukulia kawaida ila baada ya kujiunga nikaona nina kazi ya kufanya."

Kwasi aliyeitumikia Simba kwa kipindi cha misimu miwili kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 aliongeza, awali mashabiki wa timu hiyo walipenda uchezaji wake ingawa jambo lililomuharibia na Tshabalala kuzidi kumpiga bao ni kitendo cha kuzembea zaidi mazoezi.

Kwa upande wa aliyekuwa beki wa Simba, Boniface Pawasa alisema, mafanikio makubwa kwa mchezaji huyo ni kutokana na kujitunza na kuhimili usupastaa wake.

"Nidhamu ndiyo ambayo inamfanya Tshabalala afike hapa alipo leo kwa sababu ni mchezaji ambaye hana skendo na huwezi hata siku moja kusikia kashfa kama wengine, binafsi nampongeza Henry Mzozo kwani amekuwa kama baba kwake katika malezi yake."

Huyu ndiye Tshabalala ambaye haimbwi sana lakini ana rekodi na ubabe wake ambao ni ushawishi tosha kwa vizazi vya sasa na vijavyo.