Kanoute awatikisa mabosi Simba

Muktasari:

  • Kanoute tangu ajiunge na Simba mwaka 2021 akitokea klabu ya Al-Ahli Benghazi ya Libya iliyokuwa imemnunua kutoka Stade Malien ya Mali, nchi anayotokea kiungo huyo mrefu.

KIUNGO wa Simba, Sadio Kanouté 'Putin' yupo mguu ndani, mguu nje kuwepo katika kikosi hicho kwa msimu ujao baada ya kuwatikisa mabosi wa klabu hiyo kiasi kwamba mazungumzo baina yao ili kusalia kikosini kushindwa kupata muafaka.

Kanoute tangu ajiunge na Simba mwaka 2021 akitokea klabu ya Al-Ahli Benghazi ya Libya iliyokuwa imemnunua kutoka Stade Malien ya Mali, nchi anayotokea kiungo huyo mrefu.

Pamoja na kuwa na mchango kubwa, kuifungia Simba mabao kadhaa, bado Kanoute hakuweza kufanikiwa kuvaa medali ya ubingwa wa Ligi Kuu Bara kutokana na misimu mitatu mfululizo Yanga kutawala ligi hiyo sambamba na Kombe la Shirikisho (FA).

Tangu ajiunge Simba, kiungo huyo amefanikiwa kuvaa medali ya Ngao ya Jamii msimu uliopita baada ya kuitungua Yanga kwa penalti 3-1 katika michuano iliyoshirikisha timu nne na kupigwa jijini Tanga.

Pamoja kusaliwa na mkataba wa mwaka mmoja katika mkataba alionao, Kanoute ameomba kuondoka ili kutafuta changamoto nyingine, jambo ambalo uongozi bado haujatoa maamuzi.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, uongozi unaona kubwa bado Kanoute ana mchango mkubwa katika timu yao pamoja naye kuafikia maamuzi ya kuondoka, hata kwa kuuzwa timu nyingine.

“Bado kuna shida kwa Kanoute kubakia Simba, ameomba kuondoka na amekuwa akisisitiza kufanya hivyo, uongozi umekaa naye, bado ameshikilia msimamo wake, kwa hatua hii, ni lazima aondoke na maamuzi ya kubaki ni madogo sana,” kimesema chanzo hicho, huku Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amekiri, Kanoute ameomba kuondoka na uongozi bado haujaamua kuhusu na hatma yake.

"Ni kweli tupo kwenye mazungumzo na mchezaji, anaomba akapate changamoto mpya, ingawa hilo bado halijafikia mwafaka kama ataendelea kuwepo. Kanoute ni mchezaji muhimu na ndio maana Simba ilimsajili, jibu litakapopatikana tutawataarifu kama tutaendelea naye au la."