Mabao ya Freddy yamuibua Phiri

Muktasari:

"Bado wanaweza kubadilika kama viongozi na makocha watajua wapi kinapungua kipi na wachezaji wenye ubora gani wanahitajika, wakifanya hivyo Simba itarudi kama ilivyokuwa zamani," alisema Phiri ambaye msimu wa 2010-11 aliipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza mechi yoyote.

SIMBA mnamkumbuka kocha wenu wa zamani Patrick Phiri? Amewatumia salamu akiwaambia kuwa ilibaki kidogo tu presha ya mashabiki iwaondolee mshambuliji mzuri ambaye sasa ameanza kuonyesha mabao yake.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha huyo Mzambia ambaye amewahi kuinoa Simba kwa mafanikio alisema kitendo cha timu hiyo kukosa matokeo mazuri na mashabiki kuongeza presha kwa wachezaji ilikuwa mbaya kiasi cha kukaribia kumpoteza mshambuliaji Fredy Kouablan.

Phiri amesema amekuwa akizungumza na mshambuliaji huyo mara kwa mara na amekuwa akimtaka kupuuzia maneno ya watu na kufanya kazi yake iliyomleta Bongo, hatua ambayo sasa imerudisha ubora wa mshambuliaji huyo ambaye licha ya kucheza kwake Tanzania bado anaongoza kwa mabao katika Ligi Kuu ya Zambia msimu huu.

Mpaka sasa wakati Simba ikijiandaa kucheza na Tabora United, Freddy ameshafunga mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara akibakiza mabao mawili tu kuwafikia viungo washambuliaji Clatous Chama na Said Ntibazonkiza wenye mabao saba kila mmoja.

Katika mabao hayo matano Freddy hana hata bao moja la penalti huku viungo wao wawili wakiwa nayo ilhali yeye ameitumikia Simba kwa miezi michache tu baada ya kujiunga nayo katika usajili wa dirisha dogo.

"Freddy ni mshambuliaji mzuri sana, wakati Simba inamsajili niliwapongeza nikijua imefanya usajili mzuri bahati mbaya wakati anafika akakutana na presha kubwa ya mashabiki kuhusu timu yao kukosa matokeo mazuri," alisema Phiri.


"Unahitaji kuwa na timu iliyokamilika tu kuwa na viungo wazuri, huyu ni mshambuliaji ambaye kama anapata huduma nzuri ndani ya eneo la hatari anaweza kufunga kwa wingi, ni presha tu wakati anafika hapo Simba ndio ilikaribia kumuondoa."

Aidha, kocha Phiri aliongeza kuwa Simba inaweza kurudi kwenye ubora wake endapo tu itajua mahitaji ambayo yamepungua kwenye kikosi chao na kuyafanyia kazi kwa umakini.

Phiri alisema kikosi cha Simba kinahitaji wachezaji ambao watajitoa kwa kujiongeza nje ya ufundi ambao utatoka kwa makocha wao.

"Unapokiona kikosi cha Simba sasa kimepoteza wale wachezaji bora, nadhani hii ni nafasi kwao kujitathimini, kuna maeneo unaona viwango vya wachezaji hawana ubora kulinganisha na uzito wa presha ya jezi ya Simba.

"Bado wanaweza kubadilika kama viongozi na makocha watajua wapi kinapungua kipi na wachezaji wenye ubora gani wanahitajika, wakifanya hivyo Simba itarudi kama ilivyokuwa zamani," alisema Phiri ambaye msimu wa 2010-11 aliipa Simba ubingwa wa Ligi Kuu Bara bila ya kupoteza mechi yoyote.