Mabosi wapya soka la wanawake waahidi neema

Muktasari:

  • Mbeya licha ya kusifika kwa soka, lakini haijawahi kuwa na timu ya Ligi Kuu kwa Wanawake, huku daraja la Kwanza napo ikiwa ni kusuasua kwa timu zake kutofanya vizuri kwani Mpaju Queens waliowakilisha msimu huu wametoka patupu.

CHAMA cha soka la Wanawake Mkoa wa Mbeya (MWFA) kimeahidi kusimamia vyema soka hilo kuhakikisha kinaibua na kuendeleza vipaji vya wanawake mkoani humo na kufikia kiwango cha ushindani.

Mbeya licha ya kusifika kwa soka, lakini haijawahi kuwa na timu ya Ligi Kuu kwa Wanawake, huku daraja la Kwanza napo ikiwa ni kusuasua kwa timu zake kutofanya vizuri kwani Mpaju Queens waliowakilisha msimu huu wametoka patupu.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa nafasi ya Mwenyekiti katika uchaguzi uliofanyika juzi Jumamosi, Atupakisye Jabir alisema kwa sasa wanaenda kuanza kazi rasmi kuhakikisha soka la Wanawake linaamka upya.

Alisema kabla ya kumaliza muda wao wa miaka minne madarakani, wanahitaji kuacha alama ikiwa ni kupata timu za Ligi Kuu, daraja la Kwanza na ligi ya Mkoa kuchezwa.

“Tunalo deni kubwa katika soka hili, kama ambavyo tuliomba na kupewa kura za kutosha, tunapaswa kulipa tulichoahidi, tunataka kama ilivyo soka la wanaume, wanawake nao lazima tuache alama” alisema Atupakisye.

Mwenyekiti huyo alitumia nafasi yake kikatiba kuwateuwa Sarah Samson kuwa Katibu Mkuu na Sekela Donald kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa.

Waliochaguliwa wengine ni Elisia Mwaipopo (Mjumbe Mkutano Mkuu Taifa), Asumin Mbunda na Loveness Mwakanyamale nafasi ya Mjumbe kamati tendaji (MRWFA) Mkoa.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani humo (Mrefa), Sadick Jumbe aliwataka viongozi waliochaguliwa kusimamia vyema mpira wa Wanawake na kupata timu ya Ligi Kuu.

“Jukumu lenu siyo dogo, tunahitaji kuona mabadiliko, fanyeni kazi kwa ushirikiano, tengenezeni sekretarieti iliyo bora na imara kuhakikisha Soka la Wanawake linakua” alisema Jumbe.