Mastaa Umitashumta kuitwa Stars

Muktasari:

  • Ndumbaro ambaye alikiri kupokea barua ya Samatta, alisema wizara imeshatoa maelekezo kwa vyama vyote vya michezo nchini wanapoita timu za taifa lazima wajumuishe angalau wachezaji wawili kutoka Umisseta na Umitashumta.

WAKATI Shirikisho la Soka nchini (TFF) likiwa limeshapokea barua ya kustaafu kuitumikia Taifa Stars ya nahodha, Mbwana Samatta, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Damas Ndumbaro ametaja mikakati ya kupata warithi wa wachezaji waliopo na mastaa wa baadae.

Ndumbaro ambaye alikiri kupokea barua ya Samatta, alisema wizara imeshatoa maelekezo kwa vyama vyote vya michezo nchini wanapoita timu za taifa lazima wajumuishe angalau wachezaji wawili kutoka Umisseta na Umitashumta.

Alisema wachezaji hao chipukizi watapata uzoefu, kujifunza, kufanya mazoezi na wachezaji wazoefu wa timu za taifa na wengine watabahatika kucheza mechi za kirafiki, huku akikisitiza kwamba wanafunzi waliochaguliwa wote waliochaguliwa na wataitwa timu za taifa.

Alisema tayari wameshaielekeza TFF kuhakikisha hawapangi mechi kwenye wiki ya mwisho wa mwezi kwenye ratiba ya Ligi Kuu ambayo itatumika kuita timu za taifa lakini sehemu kubwa itakuwa ni U-23 wakiwemo vijana kutoka Umitashumta na Umisseta watakaokaa kambini siku tano na kucheza mechi nne za kirafiki kila mwaka.

“Ukiangalia sifa za wachezaji wetu wa timu za taifa hasa kwenye soka wengi hawatoweza kuwepo mwaka 2027, Mbwana (Samatta) ameshatuandikia kuomba kustaafu sasa nafasi ile inazibwa na nani,”  alisema Dk Ndumbaro

“Inazibwa na watoto hawa jukumu letu ni kuwaandaa watakaa kambini kupata mafunzo wengine watapata bahati ya kucheza mechi za kirafiki, kwahiyo Umitashumta na Umisseta ndiyo chimbuko letu la kufanikisha hayo na hili tutafanya kwenye michezo yote.

“Kwenye soka tunatilia mkazo zaidi kwa sababu 2027 sisi na majirani zetu tutakuwa wenyeji wa Afcon, kwahiyo programu hii inakusudia kujenga timu itakayoshiriki Afcon 2027 na kutupeleka Kombe la Dunia 2030.

“Tumechukulia programu hii kwa umakini mkubwa na hii timu ya U-23 tumeipangia angalau itacheza mechi nne za kirafiki kwa mwaka mbili ndani ya nchi mbili nje ya nchi. Hatuwezi kuvuna pasipo kupanda, tupalilie tuweke mbolea tutavuna 2027 na 2030.”