Mboneke gumzo Sokoine,  Mgunda ampa tano Mwamnyeto

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Mwamnyeto amewashukuru wachezaji wenzake, wadau na mashabiki kwa kumsapoti katika mechi hiyo maalumu, akieleza kuwa kilichopatikana kitaelekezwa kwa jamii.

ACHANA na matokeo ya ushindi wa mabao 2-1 iliyopata timu Mwamnyeto dhidi ya Mbeya All Stars,  burudani ilikuwa kwa mchekeshaji, Oscar Mwanyanje  'Mc Mboneke' aliyeteka mashabiki kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini hapa, jioni ya leo Jumamosi, licha ya kwamba aligusa mpira mara tu uwanjani.

MC Mboneke aliingia uwanjani hapo dakika ya 90 akichukua nafasi ya Yacouba Songne akiichezea timu Mwamnyeto, ambapo kabla ya kuingia alianza kurukaruka huku akishikwa na kocha Juma Mgunda.

Hata hivyo, kuingia kwake mchekeshaji huyo aligusa mpira mara moja ambapo shuti lake lilitoka nje na kuamsha shangwe kwa mashabiki ambao walivutiwa na madoidoi aliyokuwa nayo.

Katika mchezo huo, Mbeya All Stars ndio ilitangulia kupata bao kupitia kwa George Mpole dakika ya 24 kabla ya Yacouba kusawazisha dakika ya 39 na kufanya hadi mapumziko timu hizo kuwa nguvu sawa.

Dakika ya 90, Nkane aliiandikia bao la pili timu ya Mwamnyeto na kumaliza mechi hiyo kwa ushindi huo.

Mchezo huo maalumu wa hisani, ulilenga kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia wasiojiweza wakiwamo wagonjwa, yatima, walemavu na masikini kupitia programu ya Mwamnyeto Foundation.

Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda aliyeinoa timu ya Mwamnyeto, amesema programu kama hizo zinaamsha hamasa kwa wachezaji ambao wanarejesha nguvu kwa jamii kwani baada ya mpira hurudi kwa wananchi.

"Hii ni nzuri sana, kwa sababu hiki kinachofanywa na wachezaji kinapaswa kupewa sapoti kwani baada ya mpira wachezaji hurudi kwao na hakuna cha usimba wala uyanga" amesema Mgunda, nyota wa zamani wa kimataifa aliyewahi kutamba na CDA Dodoma na Coastal Union.

Kwa upande wa Mwamnyeto, mratibu wa programu hiyo, amewashukuru wadau na mashabiki pamoja na wachezaji wenzake walioweza kumsapoti na kwamba kilichopatikana anakirudisha kwa jamii.

"Naenda kujipanga tena mwakani kuboresha pale patakapoonekana mapungufu,  lakini kwa ujumla niwashukuru wote waliokuja kunisapoti na kilochopatikana kitaenda kwa walengwa" amesema Mwamnyeto, beki na nahodha wa Yanga anayekipiga pia timu ya taifa na aliyewahi kuwika na Coastal Union.