Mwamnyeto apewa miwili Yanga

Muktasari:

  • Mwamnyeto aliyekitumikia kikosi hicho kwa misimu minne huku mitatu mfululizo ikiwa na mafanikio akiwa kama nahodha akitokea Coastal Union, alikuwa ni miongoni mwa nyota waliomaliza mikataba na kulikuwa na sintofahamu juu ya kusalia kikosini au kusepa

NAHODHA wa Yanga, Bakar Mwamnyeto ameongeza mkataba wa miaka miwili ili kukitumikia kikosi hicho, huku klabu hiyo ikitoa Sh300 milioni kama pesa ya usajili huo.

Mwamnyeto aliyekitumikia kikosi hicho kwa misimu minne huku mitatu mfululizo ikiwa na mafanikio akiwa kama nahodha akitokea Coastal Union, alikuwa ni miongoni mwa nyota waliomaliza mikataba na kulikuwa na sintofahamu juu ya kusalia kikosini au kusepa hasa baada ya Simba kudaiwa kwamba ilikuwa ikimpigia hesabu.

Na taarifa za ndani zinasema nyota huyo alikuwa na ofa kadha ikiwamo ya nje ya nchi, lakini menejimenti inayomsimamia iliamua kumuachia mwenyewe kufanya uamuzi wapi pa kwenda kwani ndiye mwamuzi wa mwisho.

"Ofa zote zilikuja mezani, lakini maamuzi ya mwisho tumemwachia mchezaji mwenyewe achague wapi atakwenda kuchezea msimu ujao,"alisema mtu wake wa karibu, huku taarifa za uhakika zinasema kuwa nahodha huyo kaamua kusalia Jangwani kwa kusaini mkataba wa miaka miwili na muda wowote taarifa zitatolewa.

"Ila popote atakapotangazwa basi hapo ndipo alipopataka mchezaji mwenyewe ila kazi yetu ni kumshauri kuchagua kilicho bora." 

Beki huyo amekuwa akitengeneza ukuta wa Yanga akishirikiana na mabeki wengine wa kati akiwamo Ibrahim Hamad 'Bacca', Dickson Job na Gift Fred, japokuwa mara nyingi alikuwa akianzia benchi kuwapisha wenzake kuanza kikosi cha kwanza.

Kabla ya kutua Yanga mwaka Agosti 2020, Mwamnayeto aliitumikia Coastal kwa misimu miwili akiwa pia kama nahodha akitengeneza ukuta imara kwa kushirikiana na Ibrahim Ame ambaye alisajiliwa na Simba wakati Nondo akitua Yanga.

REKODI ZAMBEBA
Kwa kipindi chote alichochezea Yanga, Mwamnyeto amekuwa miongoni mwa wazawa waliokuwa wakipata namba chini ya makocha waliomnoa wakiwamo Zlatko Krmpotic, Cedric Kaze, Juma Mwambusi kabla ya kupokewa na Nasreddine Nabi na Gamondi. Pia hata katika timu ya taifa, Taifa Stars pia nyota huyo amekuwa akiitumika mara kwa mara.

Licha ya hayo amekuwa na uwezo mzuri zaidi anapocheza pamoja na mabeki wenzake Ibrahim Bacca na Dickson Job ambao kwa pamoja wanajenga ukuta imara wa Yanga usiopitika kwa urahisi.

Hata hivyo, rekodi zinambeba kwani tangu atue Yanga kikosi hicho kimebeba ubingwa wa Ligi Kuu mara tatu mfululizo kama ilivyo kwa Kombe la Shirikisho, mbali na Ngao ya Jamii mara mbili na kufika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, huku msimu uliopita wakitinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa iliyocheza mara ya mwisho mwaka 1998.