Nyota Simba aangua kilio uwanjani

Simba U17 (1)
Simba U17 (1)

Muktasari:

  • Camavinga ambaye alionyesha kiwango bora katika mchezo huo, ilibidi abembelezwe na wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi la Simba kutokana na kipigo hicho ambacho kimewashusha kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo ya vijana.

NAHODHA wa timu ya vijana ya Simba U17, Abdul Salum 'Camavinga' ameangua kilio  baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa kwanza wa Ligi ya Vijana dhidi ya Yanga kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Camavinga aliyeonyesha kiwango bora katika mchezo huo,  ilibidi abembelezwe na wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi la Simba kutokana na kipigo hicho  kilichoishusha Simva kutoka kilele cha msimamo wa ligi hiyo.

Kocha wa Simba, John Bocco aliyesimama kwa dakika 70 za mchezo huo, aliwatia moyo wachezaji ambao nyuso zao zilionekana kuwa na simanzi  huku upande wa pili wa Yanga ukiwa ni kicheko.

Akiwa na maumivu ya kupoteza mchezo huo wa kwanza kwa Simba katika ligi ya vijana, Camavinga alikimbilia katika vyumba vya kubadilishia nguo akiwa analia akifuatiwa na wachezaji wenzake pamoja na benchi la ufundi, huku wakiwaacha Yanga wakitamba.

Matokeo hayo yameifanya Simba yenye pointi 17  kushushwa na Azam (20) ambao mapema ilipata ushindi wa bao 1-0 mbele ya JKT Tanzania kwenye uwanja huo. Awali Simba na Azam kila moja ilikuwa na pointi 17,  na kutofautiana  mabao ya kufunga na kufungwa 

Katika mchezo huo, Simba ndio iliyokuwa ya kwanza kupata bao  kupitia kwa Athuman Idd katika kipindi cha kwanza, lakini Yanga ilipindua meza kipindi cha pili kwa kutoka nyuma na kufunga mara mbili.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Chitunzi Masaka na Hamis Idd ambaye aliingia kipindi hicho cha pili, kwa zaidi ya dakika 10 vijana wa Bocco waliweka kambi katika nusu ya wapinzani wao.

Hata hivyo, Yanga ilikuwa imara na kwa kuwa ilikuwa mbele huku wachezaji wa timu hiyo wakionekana kupoteza muda jambo ambalo lilionekana kumkwaza Bocco aliyekuwa akitazama saa kila wakati.

Licha ya matokeo hayo, Simba bado ina nafasi ya kupigania ubingwa 8katika ligi hiyo kutokana na kusaliwa kwa michezo mitano.
Kabla ya mchezo wa leo, Yanga ilikuwa nafasi ya saba ikiwa na pointi 10,  hivyo kwa sasa imefikisha pointi 13.