Ramadhani Brothers wazifikisha tuzo na picha ya Rais kilele cha mlima Kilimanjaro

Muktasari:

  • Ndugu hao, Fadhili  Ramadhani na Ibrahim Job, ambao hivi karibuni walijinyakulia kitita cha dola 250,000 (Sh637 milioni) katika mashindano ya sanaa na burudani ya AGT ya Fantasy League nchini Marekani, wamewasili kileleni hapo leo saa 4 asubuhi baada ya kutumia siku tano hadi kufika katika kilele hicho kirefu zaidi cha Uhuru Peak kupitia njia na lango la Marangu.

MABINGWA na washindi wa America's Got Talent 2024 (AGT), Ramadhani Brothers, wamefanikiwa kufika leo Jumamosi, Mei 4,2024 katika kilele cha Mlima Kilimanjaro wakiwa na tuzo, bendera ya taifa, picha ya majaji wa AGT na ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Ndugu hao, Fadhili  Ramadhani na Ibrahim Job, ambao hivi karibuni walijinyakulia kitita cha dola 250,000 (Sh637 milioni) katika mashindano ya sanaa na burudani ya AGT ya Fantasy League nchini Marekani, wamewasili kileleni hapo leo saa 4 asubuhi baada ya kutumia siku tano hadi kufika katika kilele hicho kirefu zaidi cha Uhuru Peak kupitia njia na lango la Marangu.

Awali, Ramadhan Brothers walikabidhiwa bendera ya Tanzania na picha ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kuifikisha kileleni na pia katika safari hiyo walibeba tuzo zao za  AGT,, pamoja na picha za majaji wao ambazo wamefika nazo leo kileleni kwa lengo la kuongeza hamasa kwa watu wa ndani na nje ya  nchi kuupanda Mlima Kilimanjaro.

Ramadhani Brothers  waliianza safari yao ya kupanda mlima huo Aprili 29 kwa lengo la kutangaza utalii wa ndani pamoja na kuhamasisha Watanzania  kupigia kura Hifadhi za Taifa  za Serengeti na Mlima Kilimanjaro zinazowania tuzo ya kivutio bora cha utalii barani Afrika, shindano ambalo limeandaliwa na shirika la World Travel Awards (WTA).

Awali, wakizungumza na Mwanaspoti, Ramadhani Brothers wamesema: "Sanaa yetu ambayo tunaifanya, watu wengi wanaofuatilia michezo, huwa wanaona tunapenda kubebana kichwa kwa kichwa halafu pia tunapenda kutengeneza vitu virefu ambavyo mfano wake ni kama Mlima Kilimanjaro "

"Tuna furaha sisi Ramadhani Brothers kwa kumuunga mkono Rais wetu kwa kuendelea kutangaza nchi yetu vyema, tumefanikiwa kutangaza nchi yetu vizuri kule Marekani hata hapa Tanzania tunaendelea kupiga kazi."

Kwa upande wake Ofisa Mhifadhi Mkuu Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Gladys Ngu’umbi  ambaye ni Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Kilimanjaro amelipongeza kundi hilo na kueleza kuwa Watanzania watumie fursa hiyo kuupigia kura Mlima Kilimanjaro  unaowania tuzo ya kivutio bora cha utalii barani Afrika.

"Nitoe rai yangu kwa Ramadhani Brothers pamoja na wananchi kuonyesha uzalendo wao kwa kuhamasisha na kupigia kura Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ili uweze7 kushinda na kuwa mshindi katika vivutio bora vya utalii barani Afrika," amesema Gladys.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya utalii ya Zara Tours, Zainab Ansell amesema wameshirikiana na Tanapa kuandaa safari hiyo lengo likiwa  kuhamasisha Watanzania kupigia kura mlima huo kama kivutio bora duniani.