Sakata la Kibu kugomea mkataba Simba, udalali watajwa

Muktasari:

  • Simba inataka kumwongezea mkataba. Yanga inataka kumhamishia kwa Wananchi. Ihefu nao wamemwambia aachane na timu za Kariakoo aendee akatulie mkoani na pesa ipo. Hili picha la wakubwa hao watatu lina mambo mengi na Mwanaspoti linafuatilia hatua kwa hatua;

Habari ya mjini kwa sasa ni kuhusu Kibu Denis ‘Mkandaji’. Ni kiungo mshambuliaji wa Simba anayemaliza mkataba wake kwa Wekundu wa Msimbazi hao na ameziingiza timu hizo kwenye vita kubwa na picha lake linatisha.

Simba inataka kumwongezea mkataba. Yanga inataka kumhamishia kwa Wananchi. Ihefu nao wamemwambia aachane na timu za Kariakoo aendee akatulie mkoani na pesa ipo. Hili picha la wakubwa hao watatu lina mambo mengi na Mwanaspoti linafuatilia hatua kwa hatua;

YANGA WAMETIBUA MAMBO

Hadi tunakwenda mitamboni jana usiku, Yanga ndio ilikuwa kipaumbele cha Kibu licha ya kwamba mwili uko ndani ya jezi ya Simba. Wameshampa hadi mkataba wa awali na imebaki kusaini tu.

Mshambuliaji huyo ametaka dau la Sh400 milioni ambazo anataka zote zilipwe kwa mkupuo mmoja. Kati ya timu zilizoweka ofa mezani, hakuna ambayo imefikia fungu hilo. Yanga iko tayari kumlipa Sh300 milioni na mshahara mnono.

Ihefu ‘Singida Black Stars’ yenyewe katika ofa yake iko tayari kutoa kiasi cha Sh 500 milioni kwa mkataba wa miaka mitatu lakini kwa awamu, jambo ambalo halionekani kumshawishi Kibu na hivyo kuona Yanga ndio wako siriazi zaidi katika ofa ambayo wameleta mezani.

Nyota huyo wa zamani wa Kumuyange, Geita Gold na Mbeya City, amehitaji mshahara wa Sh15 kwa mwezi ambao Yanga na Ihefu kila moja imeridhia kumpa lakini Yanga imeenda mbali zaidi kwa kuwa tayari kumnunulia gari ya kutembelea, pia kumlipia nyumba kwa kipindi chote ambacho ataitumikia klabu hiyo.

Lakini sababu nyingine ambayo inamfanya Kibu avurugwe na ofa ya Yanga ni uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao na kufanya vizuri jambo ambalo litamhakikishia bonasi nzuri ya fedha tofauti na Ihefu ambayo haiwezi kushiriki lakini haina uhakika wa kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Ingawa imeingia hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania ambalo bingwa wake anakata tiketi ya moja kwa moja ya kwenda Kombe la Shirikisho Afrika.

NAMBA ZINAITISHA SIMBA

Tumpe Mil 500 kwa goli mmoja msimu mzima? Hapana. Za ndani kabisa ni Simba wanamwimbisha Kibu asalie msimu ujao lakini si kwa dau analotaka yeye. Simba wanaamini katika kujipanga upya hawawezi kupata staa mzawa mwenye kiwango cha Kibu hivyo wanapambana na menejimenti wakae chini kwa mara nyingine mambo yazungumzike.

Katika msimu huu, Kibu amefumania nyavu mara moja tu kwenye ligi na ilikuwa ni katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu dhidi ya Yanga ambao Simba ilipoteza kwa mabao 5-1.

Mshambuliaji huyo pia amefunga bao moja tu katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ikumbukwe msimu uliopita, Kibu alifunga mabao mawili tu Ligi Kuu huku Ligi ya Mabingwa Afrika hakufunga bao lolote na msimu wake wa kwanza ndani ya Simba 2021/2022 alifunga mabao manane kwenye ligi na kutoa pasi za mwisho nne akiibuka mfungaji bora wa kikosi hicho kwani hakuna mchezaji mwingine alimfikia Kibu.

Mmoja wa watu wa karibu wa Kibu aliliambia Mwanaspoti jana kuwa; “Kibu hana presha. Ametulia anasikilizia ofa nzuri zaidi na tayari kila timu inayomtaka ikiwemo Simba inayotaka kumwongeza mkataba zimepewa masharti anayoyataka. Hadi sasa Yanga inaongoza mbio za kumsainisha.”

UDALALI MWINGI

Habari za ndani zinasema uongozi wa Simba unaona kama ofa zinazotajwa kufikishwa mezani kwa Kibu zimejaa udalali na zinalenga kuwaingiza mkenge ili watumie kiasi kikubwa cha fedha kumbakisha mshambuliaji huyo tofauti na kile ambacho imepanga kukitumia jambo ambalo linaweza kuathiri bajeti yao ya usajili katika dirisha kubwa.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema; “Tunaenda kufanya usajili mkubwa na bora zaidi katika timu yetu. Pia tunaendelea na mazungumzo ya kuwaongezea mikataba wachezaji wetu ambao tunahitaji kuendelea nao na kila tunayemtaka atabaki hususani wale bora na wenye moyo wa kuitumikia Simba.”