Senzo ampa tano Mtine Yanga

Muktasari:

  • Senzo aliyekuwa CEO wa Yanga kwa kipindi cha msimu mmoja wa 2021-2022, amesema Mtine raia wa Zambia amekuwa kiongozi mwenye maono makubwa ya wakati ujao, jambo ambalo linaleta matunda mazuri klabuni hapo.

ALIYEKUWA Ofisa Mtendaji Mkuu wa Yanga, Senzo Mbatha raia wa Afrika Kusini amesema mrithi wake Andre Mtine anastahili pongezi nyingi kutokana na mafanikio ya timu hiyo.

Senzo aliyekuwa CEO wa Yanga kwa kipindi cha msimu mmoja wa 2021-2022, amesema Mtine raia wa Zambia amekuwa kiongozi mwenye maono makubwa ya wakati ujao, jambo ambalo linaleta matunda mazuri klabuni hapo.

Msauzi huyo ameyasema hayo leo Jumamosi Juni 15, 2024 katika hafla ya uzinduzi wa Kitabu cha Yanga uliofanyika jijini Dar es Salaam.

“Tuipongeze Young Africans (Yanga), tuupongeze uongozi chini ya Rais Hersi Said sambamba na mafanikio waliyokuwa nayo kuipeleka mbele klabu bila ya kumsahau huyu jamaa (Andre Mtine) CEO mwenzangu tumpongeze naye kwani wamebeba ubingwa mfululizo akiwa sehemu ya watu muhimu sana, ni kitu kizuri,” alisema Senzo.

Mtine alitangazwa kuwa CEO wa Yanga Septemba 27, 2022 akichukua nafasi ya Senzo aliyeitumikia nafasi hiyo klabuni hapo kuanzia Agosti 2021 hadi Julai 2022.

Mzambia huyo tangu awe CEO wa Yanga, timu hiyo imebeba mataji mawili ya Ligi Kuu Bara (2022-2023 na 2023-2024) na Kombe la Shirikisho (FA) mara mbili (2022-2023 na 2023-2024).

Pia Yanga imecheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 ikipoteza kwa kanuni ya bao.la ugeninibmbele ya USM Alger baada matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 2-2, huku 2023-2024 ilicheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka 25 ilipocheza mara ya mwisho 1998.

Senzo wakati akiitumikia Yanga alikuwepo katika mafanikio ya timu hiyo katika kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara 2021-2022 na Kombe la Shirikisho (FA) msimu huo.