Tajiri aingilia dili la Mpanzu anayetajwa kutua Simba

Muktasari:

  • Mbali na Simba ambayo imeonyesha nia ya dhati ya kumpata Mpanzu, lakini inaelezwa mabosi wa Wydad Casabalanca ya Morocco ni miongoni pia wa waliojitosa katika dili hilo, huku uamuzi wa mwisho ukibaki kwa mchezaji mwenyewe.

RAIS wa Klabu ya AS Vita, Amadou Diaby amekutana na winga wa kikosi hicho, Elie Mpanzu Kibisawala ili kumshawishi aendelee kubaki ndani ya timu hiyo baada ya hivi karibuni kuhusishwa kuhitajika na miamba wa soka nchini, Simba.

Winga huyo ni miongoni mwa wachezaji wanaohitajika na Simba katika dirisha hili la usajili ili kuboresha kikosi hicho ambacho kinajengwa upya ili kuleta ushindani msimu ujao baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo.

Taarifa kutoka DR Congo zinaeleza kwamba, Mpanzu  ameshawaaga wachezaji wa timu hiyo huku akiwaambia anataka kupata changamoto sehemu nyingine jambo ambalo limemfanya Amadou kufanya kikao cha siri na mchezaji huyo.

Katika kikao hicho inaelezwa hawajafikia muafaka wa kile anachotaka mchezaji huyo, huku ofa aliyowekewa na timu yake ikiwa ni kubwa kuliko ya Simba japo mchezaji mwenyewe ameonyesha utayari wa kuondoka ili kutafuta changamoto sehemu nyingine nje ya mji wa Kinshasa.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata zinaeleza kwamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba ambaye kwa sasa ni mjumbe baada ya kujiuzulu nafasi hiyo, Salim Abdallah 'Try Again' yupo DR Congo kwa mazungumzo.

"Ni kweli Try Again yupo Congo, lakini siwezi kusema kwamba ameenda kwa ajili ya dili hilo kwa sababu huwa ni mtu ambaye anaenda nchi mbalimbali kwa mambo yake binafsi. Kama ni hivyo sawa ila siwezi kukuhakikishia," kimesema chanzo kutoka ndani ya Simba.

Hivi karibuni Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally wakati wa maswali na majibu katika mtandao wake wa kijamii wa Instagram alipoulizwa kuhusu usajili wa Mpanzu, alisema wamemuona winga huyo kuwa ni mchezaji mzuri ila hawezi kuweka wazi kama wamemsajili.

"Hili ni dirisha la usajili na mengi yanazungumzwa. Nikisema nizungumzie kila mchezaji anayetajwa kutua Simba nitachoka. Naomba hili tuliache kwanza kwani muda wa kutambulisha wachezaji tuliowasajili ukifika tutafanya hivyo," alisema Ahmed.

Hata hivyo, wakati AS Vita ikihaha kubaki na nyota huyo, lakini Mwanaspoti linatambua kwamba, uongozi wa timu hiyo tayari umeanza kutafuta mbadala wake huku ikielezwa inahitaji kumrejesha aliyekuwa winga wa kikosi hicho, Marouf Tchakei.

AS Vita inapiga hesabu za kumrudisha Tchakei ambaye kabla ya kutua nchini alitokea timu hiyo na kujiunga na Singida Big Stars na baadaye Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars kuanzia Julai Mosi, mwaka jana.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alipotafutwa na Mwanaspoti kuhusu Tchakei kutakiwa na AS Vita amesema zipo ofa kutoka klabu mbalimbali zinazomtaka nyota huyo ingawa sio muda muafaka  kuzungumzia hilo.

Tchakei ambaye msimu uliopita alifunga mabao tisa ya Ligi Kuu Bara huku pia akihusishwa na Simba ambayo msimu uliopita ilizidiwa kete na Singida, inaelezwa ilimuwekea kiasi kikubwa cha fedha kilichomshawishi kuendelea kubaki.

Mbali na Simba ambayo imeonyesha nia ya dhati ya kumpata Mpanzu, lakini inaelezwa mabosi wa Wydad Casabalanca ya Morocco ni miongoni pia wa waliojitosa katika dili hilo, huku uamuzi wa mwisho ukibaki kwa mchezaji mwenyewe.

Tayari Simba imeshatangaza kuchana na wachezaji sita akiwamo aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, John Bocco, Shaaban Chilunda, Saido Ntibazonkiza 'Saido', Kennedy Juma, Henock Inonga na Luis Miquissone ili kulewa mastaa wengine wapya.

Wakati ikiwatema nyota hao, timu hiyo imemtambulisha aliyekuwa beki wa Coastal Union, Lameck Lawi huku Israel Mwenda, Mzamiru Yassin na Kibu Denis wakitangazwa kuongezewa mikataba mipya ili kuendelea kusalia ndani ya kikosi hicho kwa msimu ujao.