Arsenal 5, Chelsea 0; Washika Bunduki wafumua Darajani

Muktasari:

  • Arsenal kwa sasa imeketi kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England, huku ikiwa na wastani mzuri kabisa wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa na +55

LONDON, ENGLAND. ARSENAL imelikataa gundu la Aprili baada ya usiku wa jana Jumanne kushusha kipigo kizito kwa Chelsea na kuweka hai matumaini yao ya kunyakua taji la Ligi Kuu England msimu huu.

Arsenal ikiwa kwenye uwanja wake wa Emirates iliichapa Chelsea mabao 5-0 na hivyo kuweka pengo la pointi tatu kwenye kilele cha msimamo wa ligi hiyo dhidi ya timu inayoshika nafasi ya pili, Liverpool na pointi nne dhidi ya timu iliyopo kwenye nafasi ya tatu, ambao ni mabingwa watetezi Manchester City.

Leandro Trossard aliifungia Arsenal bao la 100 msimu huu, kabla ya Ben White na Kai Havertz kila mmoja akifunga mara mbili wakikamilisha kipigo hicho kizito kabisa kwa vijana wa Stamford Bridge.

Baada ya kuchapwa na Aston Villa siku 10 zilizopita, kisha ikachapwa na Bayern Munich na kutupwa nje kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, wasiwasi uliibuka kama Arsenal imeendelea na gundu ambalo limekuwa likiwaandama katika mechi zao za Aprili.

Lakini, sasa ilichokifanya usiku wa jana, kimeonyesha mwaka huu wamedhamiria kufanya jambo kubwa na kumaliza ukame wao wa miaka 20 ya kusubiri taji la Ligi Kuu England.

Kwa upande wa kocha wa Chelsea, Mauricio Pochettino hali ilikuwa ngumu na kuonyesha kwamba kikosi chake kwa sasa ni cha Cole Palmer FC. Bila ya huduma ya kiungo huyo mshambuliaji mwenye mabao 20 kwenye Ligi Kuu England, Palmer, Chelsea ilikosa kabisa miujiza kwenye eneo lake la ushambuliaji na hivyo kukutana na kipigo kizito.

Arsenal kwa sasa imeketi kwenye kilele cha msimamo wa Ligi Kuu England, huku ikiwa na wastani mzuri kabisa wa mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa na +55, hiyo ni mabao 11 zaidi ya iliyonayo Man City na mabao 12 zaidi ya iliyofunga Liverpool.
Vikosi;

Arsenal (4-3-3): Raya; White, Saliba, Gabriel, Tomiyasu; Odegaard, Partey, Rice; Saka, Havertz, Trossard.
Chelsea (4-2-3-1): Petrovic; Cucurella, Badiashile, Disasi, Gilchrist; Fernandez, Caicedo; Mudryk, Gallagher, Madueke; Jackson.