Bayern yaamua liwalo na liwe kwa Alphonso

Muktasari:

  • Mabosi wa Bayern hawana mpango wa kumuuza na wana matumaini kwamba watafanikisha mchakato wa kumsainisha mkataba mpya.

HADI sasa Bayern Munich haijafikia muafaka katika mazungumzo yao na wawakilishi wa beki wake raia wa Canada, Alphonso Davies ambaye anawindwa na Real Madrid iliyopanga kusubiri hadi mwisho wa msimu ujao ambapo mkataba wake utakuwa umefikia ukomo.

Mabosi wa Bayern hawana mpango wa kumuuza na wana matumaini kwamba watafanikisha mchakato wa kumsainisha mkataba mpya.

Hata hivyo, vyanzo vya karibu na staa huyu vinaeleza kwamba hana mpango wa kuendelea kusalia Bayern na amevutiwa sana na ofa ya Madrid, hivyo hata kama timu hiyo ikikataa kumuuza kwa sasa yupo tayari kusubiri na kuondoka bure mwakani.

Pia taarifa nyingine zinaeleza kuwa Madrid ndio inamshawishi asikubali kusaini dili jipya ili wao wampate kiurahisi mwakami bila ya kutoa ada ya uhamisho.

Davies ambaye msimu uliopita alicheza mechi 42 za michuano yote na kufunga mabao matatu ni mmoja kati ya wachezaji tegemeo wa Bayern.

Real Madrid imemnasa bure nyota mkubwa, Kylian Mbappe katika dirisha hili.