Liverpool yajiweka pabaya ubingwa EPL

Muktasari:

  • Liverpool imeendelea kuangusha pointi katika mechi za dakika za mwishoni ambapo jana ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Everton na katika mechi tatu imeshinda moja na kufungwa mbili.

LIVERPOOL, ENGLAND: Matokeo ya Liverpool yamezidi kumvurugia kocha wao Jurgen Klopp ambaye alikuwa na matumaini ya kuondoka mwisho wa msimu huu akiwa na ubingwa wa Ligi Kuu, lakini sasa mpango huo unaonekana kuingia katika mtihani mgumu kwelikweli.

Liverpool imeendelea kuangusha pointi katika mechi za dakika za mwishoni ambapo jana ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Everton na katika mechi tatu imeshinda moja na kufungwa mbili.

Kwa sasa majogoo hao wa Jiji la Liverpool wana pointi 74 wakiwa nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 34 ikiwa ni tofauti ya alama tatu dhidi ya Arsenal inayoongoza ligi ikiwa na pointi 77.

Lakini kama Manchester City iliyopo nafasi ya tatu kwa pointi 73 ilizopata katika mechi 32, itashinda viporo vyake vya mechi mbili itakuwa imeishusha hadi nafasi ya tatu kwa tofauti ya alama tano.

Mbaya ni kwamba mechi zilizosalia hadi sasa kwao ni nne pekee hivyo ni ngumu hata kuzitegemea timu pinzani kuwa zitaangusha pointi.

Ili Liverpool ichukue ubingwa inahitaji kuziombea mabaya Man City na Arsenal zifungwe walau mechi mbili kila moja katika mechi zilizobakia.

Ukiondoa matokeo haya jana Man United ilipata ushindi wao wa kwanza tangu Machi 30, ikiifunga Sheffield United kwa mabao 4-2.

Ushindi huo umeisogeza Man United hadi nafasi ya sita ikiishusha Newcastle na sasa timu hizo zina tofauti ya pointi tatu, Man United 53 na Newcastle 50.

Jana pia AFC Bournemouth ilipata ushindi wa bao 1-0 mbele ya Wolves na ikafikisha pointi 45 ikiishusha Brighton kwenye nafasi ya 10.

Vilevile Newcastle ilipokea kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Crystal Palace ambayo imeonekana kuwa na moto kwa siku za hivi karibuni ikiwa imeshinda mechi tatu mfululizo kuanzia dhidi ya Liverpool, West Ham na jana Newcastle, hiyo imewafanya kusogea hadi nafasi ya 14 ikifikisha pointi 39.