Penalti yamtoa machozi Ronaldo na mama yake

Muktasari:

  • Mama yake Ronaldo, Maria Dolores dos Santos Aveiro alikuwapo jukwaani uwanjani hapo na kuonekana mwenye huzuni kubwa baada ya kumshuhudia mwanaye akishindwa kufunga penalti iliyookolewa na kipa Jan Oblak.

LEIPZIG, UJERUMANI: SUPASTAA, Cristiano Ronaldo amemwaga machozi baada ya kukosa mkwaju wa penalti kwenye dakika za ziada katika kipute cha mtoano za hatua ya 16 bora kwenye michuano ya Euro 2024 dhidi ya Slovenia usiku wa juzi Jumatatu.

Mama yake Ronaldo, Maria Dolores dos Santos Aveiro alikuwapo jukwaani uwanjani hapo na kuonekana mwenye huzuni kubwa baada ya kumshuhudia mwanaye akishindwa kufunga penalti iliyookolewa na kipa Jan Oblak.

Jambo hilo lilimtikisa Ronaldo na kudhani kwamba amewafelisha wenzake baada ya mechi hiyo kufikia hatua ya kupigiana matuta na hatimaye, Ureno kushinda kwa penalti 3-0.

Ronaldo hakufunga kwenye penalti ya ndani ya muda wa mchezo na kuwaomba radhi madhabiki kabla ya Ureno kushinda kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya sare ya bila kufungana katika dakika 120.

Baada ya kukosa penalti yake kwenye dakika 105, Ronaldo aliweka mikono kichwani na kuendelea, kabla ya kuangua kilio baadaye alipomwaga machozi na kuwafanya wachezaji wenzake wa Ureno kuja kumtuliza.

Mchezaji mwenzake wanayecheza pamoja huko Al-Nassr, ambaye pia walibeba ubingwa wa Euro 2016 wakiwa na Ureno, Jose Fonte alisema: “Ni mtu mwenye hisia sana - anachotaka yeye ni kufunga. Hivyo imemuuma sana.”

Na kamera ilipohamishiwa jukwaani, mama yake naye alionekana kwenye machozi. Ronaldo aliingia kwenye mechi hiyo akiwa na rekodi ya kucheza mechi nyingi za kimataifa bila kufunga bao, mechi saba.

Na kwenye mechi hiyo ya Ureno, Ureno ilikuwa kwenye wakati mgumu wa kuvunja ngome nguvu ya Slovenia, huku Ronaldo akipata nafasi kadhaa na kushindwa kuzitumia. Hata hivyo, staa huyo alituliza akili yake kwenye hatua ya kupigiana matuta na kufunga penalti yake. Penalti nyingine za Ureno zilifungwa na Bruno Fernandes na Bernardo Silva, wakati Slovenia ilikosa penalti zake zote tatu za kwanza ambazo kipa Diogo Costa alizidaka kibabe kabisa na kuwa shujaa wa taifa.

Na sasa Ureno itakipiga na Ufaransa kwenye hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya kusaka ubingwa wa Ulaya.