Xavi Simons agombewa Manchester, London

Xavi Pict
Xavi Pict

Muktasari:

  • Baadhi ya timu hizi zinadaiwa kutuma wawakilishi wake kwenda Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo ya kina zaidi na mabosi wa PSG juu ya usajili wa Simons aliyelelewa na Barcelona.

MANCHESTER United, Arsenal, Manchester City na Bayern Munich zote zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili kiungo mshambuliaji wa Paris St-Germain na Uholanzi, Xavi Simons, 21, katika dirisha hili.

Baadhi ya timu hizi zinadaiwa kutuma wawakilishi wake kwenda Ufaransa kwa ajili ya mazungumzo ya kina zaidi na mabosi wa PSG juu ya usajili wa Simons aliyelelewa na Barcelona.


LIVERPOOL inafikiria kuwasilisha ofa nyingine kwenda Lille kwa ajili ya kumsajili beki wa timu hiyo Leny Yoro katika dirisha lijalo baada ya ofa yao ya kwanza ya Euro 50 milioni kukataliwa.

Liverpool inahitaji huduma ya fundi huyu wa kimataifa wa Ufaransa ili kuboresha eneo lao la ulinzi ikiwa ni moja ya maeneo ambayo kocha wao mpya Arne Slot ameyabainisha kwamba yana udhaifu.


MANCHESTER City imeiambia Barcelona kwamba haitokuwa tayari kumuuza beki Joao Cancelo kwa ada ya uhamisho ya chini ya Pauni 25 milioni.

Cancelo mwenye umri wa miaka 30, ameonyesha kiwango bora kilichovutia benchi la ufundi la Barca ambalo limependekeza asajiliwe. Beki huyu Mreno mwenyewe anataka kuondoka City na kutua Barca.


BAYERN Munich inafikiria kuachana na mpango wa kutaka kumsajili beki wa Chelsea, Levi Colwill, 21, katika dirisha hili kutokana na kiasi kikubwa cha pesa wanachotajiwa na Chelsea.

Awali, Bayern ilikuwa inaamini kwamba ada ya uhamisho ya fundi huyu haiwezi kufika Pauni 20 milioni, lakini Chelsea imeripotiwa kuhitaji zaidi ya hicho na haitaki kushusha bei.


EVERTON imeanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili beki wa Hull City, Jacob Greaves, 23, kama mbadala wa beki wao wa kati raia wa England, Jarrad Branthwaite, 21, katika dirisha hili.

Kwa sasa kuna mazungumzo yanaendelea baina ya mabosi wa Everton na Man United inayohitaji kumsajili Jarrad.


ASTON Villa ipo kwenye mazungumzo na wawakilishi wa straika wa Leicester City na Nigeria, Kelechi Iheanacho, 27, kwa ajili ya kuipata saini yake katika dirisha hili.

Iheanancho ambaye msimu huu alifunga mabao sita na kuisaidia Leicester kupanda daraja, mkataba wake unatarajiwa kumalizika katika dirisha hili la usajili la majira ya kiangazi.


TAARIFA zinadai Liverpool imeanza mazungumzo na Sporting Lisbon kwa ajili ya kumsajili beki wa timu hiyo na Ureno,  Goncalo Inacio, 22, katika dirisha hili.

Goncalo ni mmoja kati ya mabeki wa kati waliofanya vizuri kwa mwaka huu ndani ya Ureno kiasi cha kuvutia vigogo wengi barani Ulaya. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2027.