Biashara ya lebo Tanzania imekufa rasmi, 2025

Muktasari:
- Rafiki wa kwanza wa biashara hiyo alikuwa ni Diamond Platnumz, ambaye alianzisha lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) na kumsajili Harmonize. Kisha wasanii wengine wakaona Mondi anafaidi sana urafiki wake na Bbiashara ya Lebo Tanzania, nao wakajifanya kuanzisha lebo zao ili wawe karibu na biashara hiyo.
MAREHEMU anayefahamika kwa jina la biashara za Lebo Tanzania alizaliwa mwaka 2015 kwa kasi kubwa. Alikuja na nyota ya kupendwa kweli kinoma kwani alipozaliwa tu alikuwa anatrendi ya mjini na wasanii wenye majina walimpapatikia huku wakishindana kuonyeshana umwamba wa nani atadumu naye kwa muda mrefu.
Rafiki wa kwanza wa biashara hiyo alikuwa ni Diamond Platnumz, ambaye alianzisha lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) na kumsajili Harmonize. Kisha wasanii wengine wakaona Mondi anafaidi sana urafiki wake na Bbiashara ya Lebo Tanzania, nao wakajifanya kuanzisha lebo zao ili wawe karibu na biashara hiyo.
Ommy Dimpoz, Shilole, Nandy, Marioo, Harmonize, Joh Makini ni baadhi tu ya listi ndefu ya wasanii waliowahi kumiliki lebo, lakini hadi hivi tunavyozungumza nyingi kati ya hizo ni kama zimeangukia pua kama siyo kufa. Na vifo au kusuasua kwingi kwa lebo hizo kumetokea mwaka huu, 2025.
Nandy na lebo yake The African Princess walisajili msanii wa kuitwa Yammy ambaye mwaka huu aling’atuka kwa amani katika lebo hiyo. Harmonize wa Konde Gang alikuwa na wasanii wanne Country Boy, Cheedy, Killy, Anjela na Ibrah na wote walishasepa huku Ibra akifunga dimba kwa kuachana na lebo hiyo mwaka huu - tena kwa kutupiana kauli kali na bosi wake kwenye mitandao ya kijamii.
Diamond na WCB yake alikuwa na wasanii kibao kina Harmonize, Queen Dareen, Rayvanny, Rich Mavoko, Lava Lava, Zuchu, Mbosso na D Voice. Hata hivyo, kwa sasa lebo imebaki na wasanii wawili … Zuchu na D Voice. Mbosso ameng’oka mwaka huu na kuna tetesi Lava Lava pia ameshang’oka bado kutangazwa tu.
Rayvany na lebo yake ya Next Level Music walikuwa na msanii mmoja wa kuitwa Mac Voice ambaye mwaka huu tetesi ziliibuka dogo alishajichenga kutoka kwenye lebo hiyo. Majuzi kati akaonekana akipiga shoo za chaka to chaka huku uongozi ukionekana ni kama vile hauna taarifa.
Kwa matukio hayo, inatosha sisi kusema biashara ya lebo ni kama imekufa rasmi Tanzania.
Na kifo hiki pia kinatupa nguvu ya kusema wasanii wengi waliopapatikia lebo hawakuwa wamejipanga kuzimiliki bali walikuwa wanataka kujimwambafai kwa wenzao na ile mikato ya ‘si unaona na mimi nina lebo yangu.’
Lakini lebo nyingi zikichunguzwa utakuta zimejaa mikataba mibovu na ya kinyonyaji, uendeshaji wa kienyeji na kuwa taasisi zilizokosa sifa ya kusimamia msanii.
Hata hivyo, hatujapoteza sana wasanii waliojaribu kuanzisha lebo bila shaka wamejifunza mengi na huenda wakayatumia kwenye kutengeneza kitu ambacho pengine kinaweza kuwa na faida kama lebo za muziki, lakini kikadumu muda mrefu zaidi.