Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ibraah yuko huru, sawa...ila mgogoro Konde Music, wasanii ulionekana kitambo 

IBRAH Pict

Muktasari:

  • Usiku wa kuamkia leo , Harmonize katika ukurasa wake wa Instagram alichapisha video akielezea kumalizana na Ibraah na kumsamehe kwa kila kitu na sasa yuko huru kufanya kazi zake mwenyewe.

HATIMAYE yuko huru. Ndiyo, msanii wa Bongo Fleva, Ibraah amemalizana na Konde Music Worldwide baada ya vuta nkuvute ya kutaka kuondoka katika lebo hiyo inayosimamiwa na Harmonize, mwanamuziki namba tatu kwa kutazamwa zaidi YouTube Afrika Mashariki na hadi kuitwa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata).

Usiku wa kuamkia leo , Harmonize katika ukurasa wake wa Instagram alichapisha video akielezea kumalizana na Ibraah na kumsamehe kwa kila kitu na sasa yuko huru kufanya kazi zake mwenyewe.

“Nikiri mdogo wangu alinitumia ujumbe na kuniomba anataka kutoka kwenye lebo na kwenda kujitegemea. Nami nilimjibu moja kwa moja nakutakia kila la kheri. Kaa chini na viongozi wa Konde Gang soma mkataba wako muone mnafanyaje. Mkataba unasema endapo atataka kuvunja mkataba na kumiliki nyimbo zote hata zile nilizofanya naye ziwe zake milele na zinaingiza kwake inatakiwa alipie hicho kiasi cha pesa kilichotajwa miaka minne iliyopita.”

“Hayo ndiyo yalikuwa mazungumzo, sijui nini kimetokea kwake baadae akaja kusema kwenye mitandao yake nimemdai kiasi cha Sh1 bilioni, nikiri sijamdai kiasi hicho na nisingependa pesa yangu tena ije kunichafua mwenyewe. Namtakia kila la kheri. Kuanzia sasa yeye ni msanii anayejitegemea. Mapromota mkiwa na shoo mwiteni apate riziki aisaidie familia yake.”

“Kuhusu kauli yake nilimuita chumbani, nimemwambia amtoe mama yake mzazi, inahuzunisha, sina namna mtoto akiunyea mkono huwezi kuukata, nimemuachia Mungu. Nimemsamehe na ninamwombea, sihitaji msamaha wowote kutoka kwake akiona kuna tija sawa, akiona kuna haja ya kuomba msamaha watu waliosikia maneno hayo ni sawa lakini anayestahili kuombwa msamaha zaidi ni Mwenyenzi Mungu.”

IBR 01

Ibraah aliyetikisa na kibao chake, Nitachelewa (2020), ndiye msanii pekee aliyekuwa amesalia ndani ya Konde Music baada ya wenzake watano kuondoka kwa nyakati tofauti, wapo waliojitoa kwa sababu zao na wapo waliositishiwa mikataba.

Kwa mujibu wa machapisho ya Ibraah katika mitandao ya Instagram na Facebook, alikuwa anahitajika kulipa Sh1 bilioni ili kuvunja mkataba na lebo hiyo, fedha ambayo hana ndipo akawaomba mashabiki wake kumchangia chochote kile. Hata hivyo, sasa hana deni tena yuko huru.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Harmonize Entertainment Limited mnamo Mei 11, 2025, haikukubali au kukanusha iwapo ni kweli msanii huyo alitakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha ila walikiri wana madai yake.

"Mei 3 tulipokea barua ya madai (demand notice) kutoka kwa wakili wa msanii wetu Ibraah, barua hiyo iliainisha madai kadhaa ambayo uongozi umeanza kuyafanyia kazi mara tu baada ya kuipokea, kwa mujibu wa taratibu za kimkataba na kisheria," taaarifa ilieleza.

Taarifa ilifafanua, licha ya juhudi za kujaribu kumwelekeza msanii taratibu za kufuata kwa mujibu wa mkataba wake, walibaini Ibraah amekuwa akitoa matamko kupitia mitandao na vyombo vya habari kwa lugha isiyofaa na kuharibu taswira ya lebo hiyo.

"Umma unapaswa kufahamu, Ibraah bado ni msanii halali wa lebo ya Konde Music na ina haki ya kuendelea au kusitisha mkataba wake kwa kufuata na kuzingatia taratibu rasmi zilizoweka katika mkataba aliosaini," Konde Music ilieleza.

IBR 02
IBR 02

Kutokana na hilo, lebo hiyo imechukua hatua mbili, mosi; ni kumsimamisha Ibraah kutoa au kushiriki katika shughuli zozote za kimuziki hadi pale suala hilo litakapopata ufumbuzi wa kudumu kwa mujibu wa mkataba wake na sheria.

Pili; ni kumpiga marufuku Ibraah kuchapisha, kutamka au kufanya mawasiliano yoyote kuhusu suala hilo katika mitandao na vyombo vya habari na endapo atakiuka hilo, basi lebo haitasita kuchukua hatua za kisheria katika mahakama za Tanzania.

Ikumbukwe mnamo Aprili 11, 2020 ndipo Konde Music walitangaza kumsaini Ibraah aliyetambulishwa na EP yake, Steps (2020) ikiwa na nyimbo tano, huku akiwashirikisha Harmonize pamoja na wasanii wawili wa Nigeria, Joeboy na Skibii.

Walifuata wasanii wengine watano, Country Wizzy, pamoja na Cheed na Killy waliotoka kuachana na Kings Music ya Alikiba, pia Anjella na Young Skales kutokea Nigeria ingawa huyo haijajulikana aliondoka vipi katika lebo hiyo.

IBR 03

Harmonize alitangaza rasmi kuanzisha lebo ya Konde Music hapo Oktoba 10, 2019 ikiwa ni kipindi kifupi baada ya kujitoa katika lebo ya WCB Wasafi yake Diamond Platnumz ambapo anadai alilipa Sh600 milioni ili kuvunja mkataba wao.

Hata hivyo, mapema tu ilionekana ndani ya Konde Music kuna vitu havipo sawa, hiyo ni baada ya hapo Januari 2022, lebo hiyo kutangaza kumalizika kwa mkataba kati yao na msanii wake, Country Wizzy ikiwa ni takribani mwaka mmoja wa kufanya kazi pamoja.

Lakini kwa mujibu wa Country Wizzy, rapa aliyemtambulisha S2kizzy kupitia ngoma, Aah Wapi (2016), mkataba wake na Konde Music ulikuwa wa miaka mitano ila aliamua kuachana na lebo hiyo baada ya kuona waliyokubaliana hayatekelezwi.

Alisema miongoni mwa makuliano yao yalikuwa ni pamoja na kupeleka muziki wake kimataifa kwa kumtafutia kolabo na wasanii wakubwa wa nje lakini siku zilizidi kwenda bila hilo kutimia kikamilifu.

Vilevile alidai alipoteza nafasi ya kutumbuiza kwenye shoo nyingi kama za vyuo ambazo alikuwa anahitajika kutokana na Konde Music kuhitaji fedha nyingi ambazo yeye anaona haikuwa sawa kwa kiwango cha muziki wake.

Licha ya kuachana vizuri, Country Wizzy anadai alipoteza zaidi ya Sh12 milioni katika mchakato wa kuhama kampuni iliyokuwa inasambaza muziki wake chini ya Konde Music na kwenda kampuni mpya ambayo anaitaka yeye.

Haikuishi kwa CountryWizzy, kwani Oktoba 2022, Konde Music walitangaza kusitisha mikataba ya wasanii wawilli, Cheed na Killy kwa sababu mbalimbali walizodai zipo nje ya uwezo wao.

IBR 04

"Kwa hiyo, wasanii hawa watakuwa huru na kufanya kazi na kuingia mkataba na kundi au mtu yeyote na kuendeleza kazi zao, kwani tunaamini ni vijana na wasanii wenye uwezo mkubwa wa kufanikiwa katika safari yao ya muziki," taarifa ya lebo ilieleza.

Miezi michache mbele, yaani Januari 2023, msanii pekee wa kike wa Konde Music, Anjella naye akaonyeshwa mlango wa kutokea kabla hata ya kuutumia nusu ya mkataba wake wa miaka mitano.

Kwa mujibu wa Anjella aliyetambulishwa rasmi Konde Music hapo Machi 2021, mkataba wake ulivunjwa kutokana na kushindwa kukamilisha albamu ndani ya muda aliopangiwa sababu alikuwa ni mgojwa ila lebo hiyo ikamua kuachana naye.

Sasa Ibraah, msanii pekee alisalia katika lebo hiyo, naye anaondoka akiwa tayari ametoa EP tatu, Steps (2020), Karata 3 (2021) na Air Piano (2024) pamoja na albamu moja, The King of New School (2022) chini ya Konde Music.

Migongano ya kimaslai na mikataba kati ya wanamuziki na rekodi lebo imekuwa ikiripotiwa mara kwa mara ndani ya Bongo Fleva miaka ya hivi karibuni, sasa wasanii na wadau wamekuwa na maoni mbalimbali wakati wakiongea na gazeti hili kwa nyakati tofauti.

Rapa Soggy Doggy ambaye pia Katibu Mkuu wa Chama cha Muziki wa Kizazi Kipya Tanzania (TUMA), amesema wasanii wengi wanapoingia mikataba wanakuwa na njaa tu ya kutaka kufahamika kupitia lebo ila hawaangalii mkataba unawambana vipi.

"Huku mtaani kuna wasanii wazuri kuliko ambao wapo kwenye lebo ila hawana jinsi ya kutoka kwa sababu hawana kipato, kwa hiyo nikitumia fedha juu yako halafu ukapata jina ukafikia wakati wa kula matunda unataka kujitoa, tayari hiyo kwangu ni hasara ndiyo maana wanagombana," amesema.

Soggy Doggy amesema wao kama TUMA wameweka mwanasheria na mwanachama wao akitaka kusaini makubaliano yoyote yale, anaweza kuwaona na wao watamkutanisha na mwanasheria ili kuona kama masilahi ya pande zote mbili yanazingatiwa.

Kwa upande wake mtangazaji wa DJ Show ya Radio One, DJ Nicotrack amesema mara wasanii wanapobaini kile wanachoingiza ndipo mara nyingi wanataka kuachana na lebo zao maana mwanzo wakiwa bado hawajatoka kimuziki wanakuwa hawafahamu chochote.

"Kwa mfano Marioo pale alipo kwa sasa akiamua kwenda WCB Wasafi ataweza kudumu kuliko wasanii waliotangulia kwa sababu alishafahamu anaingiza vipi fedha yake," amesema DJ Nicotrack.

 Mkurugenzi Mkuu wa Utawala kutoka Taasisi ya Haki za Wasanii (TARO), Wakili Joshua Msambila amesema wasanii wanapoingia mikataba na rekodi lebo wanatakiwa kujua mambo mawili, upande wa kibiashara na kisheria.

Amesema wasanii baadhi hawana elimu ya biashara na wana mtazamo kwamba kazi za sanaa zinavyofanyika ni kama wanasaidiwa tu, wanasahau kuwa ile ni biashara, yeye anatakiwa apate na anayewekeza apate. 

"Mara nyingi hii biashara inapokuwa imeanza huyu msanii anakuwa hana kitu ila ana kipaji lakini kipaji chake bila fedha hawezi kufanikiwa. Kwa hiyo watu wanaowekeza wanategemea mwishowe na wao wapate faida, sio warudishe mtaji wao," amesema.

"Wasanii wengi wanavyoongea na kama yule aliyewekeza alifanya hivyo ili arejeshe mtaji wake, hapana!. Aliwekeza ili msanii akiwa mkubwa apate na yeye mwekezaji apate na aendelee kuingiza faida zaidi ya hata ya mtaji aliowekeza," amesema Msambila.

Wakili Msambila amesema kwa upande wa kisheria, msanii anapoingia kwenye kazi ya sanaa anatakiwa kuelewa mfumo mzima wa ukusanyaji na ugawanyaji wa mapato kwa faidi na hasara. 

Amesema wasanii wengine wanaingia kwenye mikataba ambayo haipo wazi au kuwalalia kwa upande mmoja, mkataba unakuwa yule anayewekeza fedha ndio apate kila kitu. Sasa msanii anausaini vile vile na baadaye unakuja kulalamika wakati yeye ndiye ametupa haki zake mwenyewe.