Kwa Rayvanny mipango haijatiki tu

Muktasari:

Rayvanny aliliambia Mwanaspoti, suala la ndoa sio kitu cha kukurupukia badala yake linahitaji maandalizi na mipango mizuri kwani ni jambo la baraka kwa Mungu, hivyo wanaotaka alazimishe ni kutojua maana ya ndoa.

STAA wa Bongo Fleva, Rayvanny amewajibu wanaomchana kwamba ni mwoga wa ndoa ndio maana kila wakati mipango yake ya kuoa huyeyuka, akisema kinachomkwamisha ni mipango kwake haijatiki tu.

Rayvanny aliliambia Mwanaspoti, suala la ndoa sio kitu cha kukurupukia badala yake linahitaji maandalizi na mipango mizuri kwani ni jambo la baraka kwa Mungu, hivyo wanaotaka alazimishe ni kutojua maana ya ndoa.

“Ni kweli huwa nasema nitafunga ndoa na nakuwa kimya, hii haimaanishi kuwa ni mwoga wa ndoa, sababu ndoa ni baraka na majaaliwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kama ikifikia wakati wa kuoa, mtu unaoa tu hivyo kwa upande wangu, ukifika wakati nitaoa, hili ni jambo la heri, watu washikilie tu hizi kauli zangu,” alisema.

Rayvanny alitangaza kwa muda mrefu kutaka kufunga ndoa na mpenzi wa siku nyingi, Fahyma aliyezaa naye mtoto mmoja kwa jina Jaydan Vanny, lakini mawazo hayo huwa yanayeyuka na kuleta ukimya kila wakati.