IMEKAAJE! Wasanii kuwa na mabodigadi, ni ulinzi au kiki?

Muktasari:

  • Hata amani ilitawala katika shoo zao licha ya nyingine kuharibiwa na vurugu mbalimbali. Hata hivyo, unajua waliokuwa wakiwalinda?

MUZIKI wa Kizazi kipya ulianza mwishoni mwa miaka ya 90. Wasanii wengi ambao kwa sasa ni wakongwe kama MR II ‘Sugu’, Afande Sele, Profesor Jay, Juma Nature, Jay Mo, Inspector Haroun, Solo Thang na wengine kibao, walilishika soko la muziki nchini na kila kona walikokwenda walisababisha shangwe.

Hata amani ilitawala katika shoo zao licha ya nyingine kuharibiwa na vurugu mbalimbali. Hata hivyo, unajua waliokuwa wakiwalinda?

Ni hivi, zamani wasanii walipata shoo na walikuwa wakizurura mitaani na kokote pale, watu waliwapa maua yao na wakuwakosoa waliwakosoa, lakini hakuna aliyetaka kulindwa na inawezekana hakukuwa na wazo kama hilo.

Kama sio askari polisi waliokuwa kwenye shughuli maalumu hasa shoo za wasanii hao, basi walilindana wenyewe, yaani msanii anajilinda maisha yake na hafikirii suala la kuletewa vurugu au kutekwa au kuwa na watu wabaya wanaomuwinda. Wakati mwingine alikuwa akizurura tu na washkaji wake.

Miaka inakimbia na wasanii wanazidi kuongezeka. Wasanii wanakamata pesa na zinawapa kiburi wengine. Hapo ndipo linapokuja suala la matumizi ya pesa na wengine licha ya kuishi kifahari, huajiri hadi mabodigadi wa kuwalinda na wengine wanadai wamezungukwa na watu wabaya na wengine wanasema ni kampani.

Achana na wale wanaoitwa ‘Machawa’ ambao wao kazi yao ni kumpamba msanii kwa kila aina ya maneno ili kuendelea kuwa juu. Hapa tunazungumzia mabodigadi ‘walinzi maalumu kwa watu maalumu’.

Je walinzi hao ni ‘show off’ tu na mbwembwe za wasanii wetu? Unakuta msanii ana mabodigadi saba hadi 12, wa nini? Au ni kutafuta kiki.

Hapa Mwanaspoti linakuletea baadhi ya wasanii wanaopenda kutembea na mabodigadi zaidi ya watano na wenyewe wamefunguka sababu ya kufanya hivyo.


Diamond Platnumz

Ndiye msanii wa kwanza kuonekana akiwa na bodigadi wake binafsi. Mara nyingi akiwa kwenye matukio yake na mizunguko mbalimbali, huzungukwa na walinzi 10. 


Harmonize

Kama ilivyoi kwa Mondi, huyu pia anatembea na walinzi wengi (watano) kila anakokwenda. Alishawahi kuliambia Mwanaspoti sababu ya kuwa na mabodigadi wengi ni ana maadui wanaoweza kumvamia na kumfanyia kitu kibaya, ndiyo maana kunakuwa na ukuta huo wa walinzi.


Wema

Sepetu

Ni msanii wa filamu. Naye anaingia kwa orodha ya wasanii wanaotembea na mabodigadi wengi kwenye matukio mengi yanayohusu mikusanyiko ya watu.

Mwanaspoti limemuuliza Wema kuhusu kuzungukwa na bodigadi na alisema; “Sifanyi kiki wala mbwembwe kutembea na mabodigadi wengi, ila ni kwa ajili ya usalama wangu, kwani huwezi jua tunaishi na watu ambao wana siri kubwa ndani ya mioyo yao, hivyo unaweza cheka na mtu kumbe ni adui yako akakutumia watu wengini kutaka kukudhuru.”


Irene Uwoya

Msanii huyu wa filamu hupenda kuongozana na mabodigadi wengi zaidi ya watano na amekuwa akionekana nao kwenye matukio mbalimbali. Hata hivyo, yeye anafunguka wengine ni kampani tu ingawa ulinzi ni muhimu kutokana na mambo yaliyopo kwenye jamii.

“Napenda kuongozana na Mabodigadi wengi kwa ajili ya ulinzi pale panapotokea kitu kibaya juu yangu wananisaidia, ila kuna mabodigadi wengine ni kampani yangu tu hivyo watu waondoe hofu ya kuona nakuwa nao wengi kwenye matukio.”


Rayvanny

Msanii mwingine aliyeanzia kwenye lebo ya Wasafi Classic Baby kabla ya kufungua yake ya Next Level, anapenda pia kutembea na mabodigadi wengi kwenye mikusanyiko ya watu wengi. Anafunguka yeye kwake ni amani tosha akiona amezungukwa kwani anaweza kufanya mambo yake yakaenda na si vinginevyo.

“Nakuwa na amani sana nikiwa na mabodidadi zaidi ya watano na ndiyo maana naenda nao kwenye matukio mbalimbali kwa ajili ya usalama wangu na sio vinginevyo.”

Hata hivyo, wapo wasanii wengi kama Dulla Makabila, Nandy na Zuchu wanaotembea na mabodigadi ingawa wenyewe wanasema ni kampani kwani msanii lazima uwe na watu wa karibu wa kukufanya ujisikie amani.