2000 kuliamsha Msoga Marathon

Rais mstaafu, Jakaya Kikwete akiwa na jezi aliyokabidhiwa kwa ajili ya kushiriki mbio za Msoga Marathon

Muktasari:

  • Wanariadha hao watachuana katika nusu marathoni (kilomita 21) kilomita 10 na kilomita tano.

ZAIDI ya wanariadha 2000 wanatarajiwa kushiriki msimu wa kwanza wa Mbio ya Msoga Marathon zitakazofanyika kesho Jumamosi.

Mbio hiyo inalenga kukusanya kitita cha Sh700 milioni kwa ajili ya kusaidia afya ya mama na mtoto kwenye hospitali ya wilaya ya Chalinze.

Wanariadha hao watachuana katika nusu marathoni (kilomita 21) kilomita 10 na kilomita tano.

Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete amesema Msoga Marathon ina lenga kukusanya fedha kusaidia afya ya mama na mtoto.

Amesema mbio hiyo ni kielelezo cha kuonyesha historia ya Halmashauri ya Chalinze ambayo inazidi kujipambanua sanjari na kutengeneza ajira kwa vijana kupitia michezo.

Ridhiwani ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma wa Utawala Bora), amesema Msoga ndipo kitovu cha Halmashauri ya Chalinze kilipo ambapo hospitali ya wilaya inajengwa.

"Uwepo wa hospitali hii ndio umechangia kuwepo kwa mbio ya Msoga Marathon ambayo itawakusanya wadau watakaochangia huduma ya mama na mtoto hospitalini hapo. Serikali imetoa fedha nyingi ikiwamo zaidi ya Sh12 bilioni za ujenzi wa hospitali hii unaoendelea," amesema.

Ameongeza kwamba baada ya kupata wazo la kufanya mbio hiyo, waliwaita wadau ili kusapoti ujenzi ambao unaendelea na ndani yake kuna huduma ya mama na mtoto ambayo inahitaji kupewa sapoti ili izidi kuwa bora zaidi.

"Tulikutana na mratibu wa mbio hii (Nelson Mrashani) kufanikisha wazo hili na sasa ni gumzo kote nchini," amesema.

Mrashani akizungumzia maandalizi, amesema uandikishaji umefikia tamati na mbio itaanza saa 11:30 asubuhi kesho Jumamosi ikiongozwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete na viongozi mbalimbali.

"Wakimbiaji wengi kutoka mikoa yenye ushindani katika riadha nchini ya Arusha, Mbeya, Kilimanjaro, Pwani, Dar es Salaam, Dodoma, Tanga na mikoa jirani wamehamasika kushiriki. Maandalizi yamekamilika, kinachosubiriwa ni mbio tu na kupata mabingwa wa kwanza wa Msoga Marathon wakati huohuo tukisapoti afya ya mama na mtoto," amesema Mrashani aliyewashukuru wadhamini wote kwa kuifanikisha mbio hiyo kwa kiwango bora akieleza medali za mbio hiyo zitakuwa na nembo ya picha ya nanasi ambayo ni ya halmashauri hiyo.