Hii ndiyo Yanga ya Chama

Muktasari:

  • Chama atakuwa mmoja wa wapambanaji wa timu hiyo msimu wa 2024/2025 ambapo timu hiyo itakuwa ikishiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrka, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA) na mashindano mengine ambayo timu hiyo itashiriki.

KLABU ya Yanga imemtangaza aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama kuwa mchezaji wake baada ya kumaliza mkataba na waliokuwa waajiri wake wa zamani jana, Juni 30, 2024

Chama atakuwa mmoja wa wapambanaji wa timu hiyo msimu wa 2024/2025 ambapo timu hiyo itakuwa ikishiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrka, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho (FA) na mashindano mengine ambayo timu hiyo itashiriki.

Huu ni utambulisho wa kwanza kwa klabu hiyo kuelekea msimu mpya wa 2024/25 ambapo inatajwa pia hata aliyekuwa mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube naye tayari amemalizana na wana Jangwani.


Chama, Dube na mifumo minne Yanga

Vuta picha hapa kuna Clatous Chama kule Prince Dube katika kikosi cha Yanga chenye nyota wengine kama vile Stephane Aziz KI, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli na Mudathir Yahya ambao waliwafanya Wananchi kutembea vifua mbele msimu uliopita na kusherehekea ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo na Kombe la Shirikisho (FA).

Chama ambaye mkataba wake umemalizika Msimbazi inadaiwa amemalizana na Yanga huku Dube akitajwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya mabingwa hao wa kihistoria baada ya sakata lake na waajiri wake wa zamani, Azam kufikia tamati.

Ishu iliyopo kwa sasa ni wachezaji hao namna watakavyotumiwa na kocha Miguel Gamondi ili kupata kilicho bora kutoka kwao kwenye kikosi ambacho msimu uliopita kilifanya vizuri kuanzia kwenye ligi hadi Ligi ya Mabingwa.

Yanga ya msimu uliopita ikiongozwa na Stephane Aziz KI kwenye safu ya ushambuliaji ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi ligi kuu (71), ilikuwa na wastani wa kufunga zaidi ya mabao mawili (2.3) katika kila mchezo na hapo waliuanza msimu huo bila ya kuwa na mshambuliaji hatari wa kati kiasili.

Nyuma yake Yanga waliondokewa na aliyekuwa mshambuliaji kinara Fiston Mayele, hivyo Kennedy Musonda na Clement Mzize walishindwa kuvaa viatu vya Mkongomani huyo aliyetimkia Misri, ndipo wakati wa dirisha dogo alipotua Joseph Guede.

Kutua kwa Joseph Guede kulikuwa na maana kwamba Gamondi alihitaji nguvu zaidi eneo hilo na je kuongezeka kwa Dube kuna maana gani? Na vipi kuhusu Chama? Hii ni mifumo tofauti ambavyo Yanga inaweza kucheza ikiwa na wachezaji hao.

4-3-3

Huu ni miongoni mwa mifumo maarufu na wa kisasa, ambao unatoa uwiano mzuri wakati wa kushambulia na kuzuia. Unaundwa na mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu.

Katika mfumo huo Dube ambaye msimu uliopita alifunga mabao saba katika ligi akiwa na Azam FC, anaweza kuwa mshambuliaji kiongozi kati ya nyota watatu wa mwisho kwa kushirikiana na Pacome, Nzengeli/ Mzize au Mudathir ambaye hivi karibuni amekuwa akitumika katika eneo hilo ndio maana msimu uliopita alimaliza akiwa na mabao tisa katika ligi.

Nani wa kuanza kati ya hao wa kusaidiana na Dube, itategemea na Gamondi atakavyoamka siku hiyo na aina ya mpinzani ambaye wanakabiliana naye lakini kati ya watatu wa nyuma ya Mzimbabwe huyo, anaweza kuanza Khalid Aucho kama kiungo pekee mwenye jukumu la kukaba huku kushoto akicheza Chama na kulia Aziz KI.

Nyota hao watakuwa huru katika eneo hilo kuchezesha timu, hivyo Yanga inaweza kuwa moja ya timu yenye safu bora zaidi ya viungo wachezeshaji kutokana na rekodi za wachezaji hao, wote ni wazuri katika upishi wa mabao kutokana na ufundi walionao.


4-4-2

Miongoni mwa mechi ambazo Yanga ya Gamondi iliutumia mfumo huo ni pamoja na ile ya hatua ya robo fainali ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns, Gamondi aliwavuruga matajiri hao wa Afrika Kusini kwa kuanza na washambuliaji wawili kiasili, Mzize na Guede japo walikuwa na majukumu tofauti.

Katika mfumo huo, Dube anaweza kuanza sambamba na Mzize au Musonda kama atahitaji kuanza na washambuliaji wawili wa kati kiasili au anaweza kuanza na mshambuliaji mmoja wa kati kiasili ambaye ni Dube huku akicheza sambamba na kiungo mwenye uwezo wa kusimama eneo hilo ambaye ni Aziz KI ameonyesha msimu uliopita.

Kati ya viungo wanne, kama Gamondi atataka kuanza na wawili wenye uwezo wa kukaba zaidi basi nafasi inaweza kuwa kwa Aucho na Mudathir huku jukumu la kuchezesha timu likiwa mikononi mwa Chama na Aziz KI watakaokuwa na jukumu la kushambulia kutokea pembeni, watakuwa mabeki wa kushoto na kulia ambao ni Kouassi Attohoula Yao na Nickson Kibabage au Chadrack Issaka Boka.

Ikiwa Gamondi atataka kuanza na kiungo mmoja tu mwenye sifa nzuri za kuzuia zaidi basi Aucho au Mudathir mmoja atasubiri benchi hivyo itakuwa ni nafasi ya Pacome au Nzengeli kuungana na Chama pamoja na Aziz KI kunogesha eneo hilo.


4-2-3-1

Muundo huu unatoa nafasi ya kucheza na mabeki wanne, viungo wawili wa ukabaji, na watatu wanaoshambulia huku mshambuliaji wa kati akiwa mmoja.

Dube anasimama kama mshambuliaji kiongozi huku nyuma yake kukiwa na viungo watatu washambuliaji ambao wanaweza kuwa Chama, Aziz KI na Pacome au Nzengeli.

Uwepo wa Dube unaweza kumfanya Gamondi amrudishe Mudathir katika eneo la ukabaji hivyo katika mfumo huo anaweza kushirikiana na Aucho huku Jonas Mkude akiwa na kibarua cha kupambana kupenya eneo hilo sambamba na Salum Abubakar 'Sureboy'.


3-5-2
Uwepo wa Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Hamad 'Bacca' na hata Gift Fred ambaye hazungumzwi sana unatoa nafasi kwa Gamondi kutumia mfumo huu ambao huwa na mabeki watatu wa kati, idadi ya viungo huwa watano wapo ambao huwa na jukumu la kusaidia kulinda.

Yanga ilicheza hivyo wakati ambao ilimkosa Yao kutokana na majeraha huku Nzengeli akifanya vizuri upande wa kulia kati ya viungo watano huku akiwa na jukumu la kushuka chini ya kusaidia kuzuia, katika mfumo huo tunaweza kuona Chama, Aziz KI, Pacome, Aucho na Mkongomani huyo wakicheza kwa pamoja.

Huku Dube akiendelea kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo sambamba na Mzize au Musonda.