HADITHI: Zindiko (sehemu ya 11)

Muktasari:

  • Huu ni mwendelezo wa hadithi tamu ya Zindiko iliyojaa visa na mikasa ya kimaisha kutoka kwa mtunzi mahiri wa riwaya SULTAN TAMBA. Twende naye...

ALIFIKA kwenye jengo la ofisi ya chama chao, akagonga mlango na kuingia.

Katibu alikuwa amekalia kiti chake akiendelea na kazi zake.

Alipoingia, akainua sura na kumtazama.

“Karibu Zaka, kabla hujanipigia simu muda ule, nilikuwa nilitaka kukupigia simu. Ila ukaniwahi.”

Zaka akamtumbulia macho!

Neno hili nalo likamweka kwenye maswali!’

Alitaka kumpigia simu amwambie nini?

Amwite kwamba njoo uchukue pesa?

Au amwite kumwambia kwamba pesa zimekosekana, mkopo wako umeshindikana, au subiri mkopo wako tunaushughulikia?”

Kichwa chake kilitengeneza maswali, kikatengeneza majibu!

Akawa anajiuliza na kujijibu!

Lakini bado Katibu alikuwa bado yuko mbele yake na ana majibu ambayo alitakiwa kusikiliza! Majibu ambayo yataondoa kile kinachomsumbua kichwani kwa maana ya maswali na majibu ya kujijibu mwenyewe kabla ya kusikia kauli ya Katibu.

“Kwa nilivyopagawa, kwa kweli niliona nije tu bila kusubiri simu yako. Hata hivyo, leo ndio ahadi yetu au umeshasahau.”

Katibu akakataa kwa kichwa, “Hapana.. hapana.. Sijasahau. Na ndiyo maana nilisema nilitaka kukupigia simu tuzungumze.”

Zaka akatumbua macho.

“Tuzungumze? Kusema tuzungumze una maana gani Katibu. Hapa kinachotakiwa si unakijua? Sio mazungumzo. Unantisha ujue unavyosema hivyo?”

“Zaka, mbona una wasiwasi – nakuona umekuja hapa hauko sawa. Hata kama pesa zipo, hakuna au za kusubiri, lakini ukweli unabaki palepale, lazima mazungumzon yatakuwepo! Kwani hata kukwambia marejesho yako hivi na vile nayo sio mazungumzo?”

Zaka akatangulia kukubali kwa kichwa, “Sawa. Nipo hapa nimekuja Katibu. Unajua hili suala linanipasua kichwa sana. Sina amani, sina raha.”

“Lakini, labda nikuulize kidogo, unajua hili jambo lako ni nyeti sana, je katika hili, umeshashirikisha pia ndugu zako katika kukusanya michango. Itakuwaje sasa.”

Zaka akamtazama katika hali ya wasiwasi.

“Mbona kama unantisha. Itakuaje kivipi. Mliniahidi kunisaidia, sasa mbona tena unasema itakuwaje. Una maana gani.”

Katibu akakaa kimya kidogo.

“Suala lako limekuwa gumu kwa kweli. Bodi imekaa, tumeangalia mahesabu na majukumu ambayo chama tunayo, kwa mfano tuna kesi tano za madalali na zinahitaji fedha ili kuwasaidia.”

“Unanichanganya. Sijaelewa unakoelekea, hebu niweke wazi.” Zaka aliongea kwa hasira kidogo.

Katibu akakaa kimya kidogo.

“Tuseme Imeshindikana kwa sasa. Yaani ni suala la kusubiri kidogo – kama mwezi au miezi miwili hivi au labda uandike barua upya uombe angalau robo ya ile hela na ukusanye michango ya wadau. Mimi ntakusaidia kuchangisha.”

Zaka akakaa kimya akijiinamia katika hali ya majonzi.

“Sijui ndio wanasema aliwazalo mjinga ndilo linalomtokea?” Zaka alijisemea. Katibu akasikia sauti hiyo, akaweka umakini katika kumsikiliza.

“Unamanisha nini kusema aliwazalo mjinga ndilo linalomtokea?”

“Tangu niongee na simu na wewe pale mwanzo, nimekosa amani kabisa. Nimekuwa nikihisi kupata jibu kama hili – ona sasa ndicho nilichokipata!”

“Sikiliza Zaka, ni suala la subira tu, usikate tamaa!

Zaka akagonga meza kwa hasira, “Hakuna muda wa kusubiri. milioni nne tu nisubiri hadi lini. Hiyo si ni sawa na dili langu moja tu... Ila kazi za dili kubwa zimekuwa ngumu ndo maana nimeona nije mnisaidie. Mtoto wangu bila vipimo sahihi na tiba tutampoteza kama yule mwingine. Hulioni hilo?”

Katibu akatulia akimtazama.

Zaka akajiinamia chini kwa uchungu.

“Nakupeni muda mchache sana, nitarudi tena hapa. Na nawahakikishia, mtoto wangu akipoteza maisha kwa ugonjwa huu na nyinyi kunizungusha kunipa hela za kunisaidia, nawaahidi nitatoka kwenye chama chenu, na sio peke yangu, nitakuwa shahidi na mzungumzaji wa madalali wengine wote. Yaani mnathamini kesi za madalali matapeli mliowaweka kwenye chama na mnakataa kunipa hela mimi zinisaidie kwa mtoto wangu? Naapa!”

Katibu akamtazama akionekana kukosa cha kusema.

Zaka akafungua mlango na kutoka nje.

Zaka akatembea polepole mtaani akionekana kuwa na mawazo mengi kichwani, akapishana na watu katika hali ya kwamba aliopishana nao ndio waliofanya juhudi za kumwachia njia apite! Vinginevyo wangegongana. Yeye alikuwa anatembea tu kama mzigo uliowekwa magurudumu na kisha kushushwa kwenye mteremko.

Kwa namna moja au nyingi alikuwa ameanza kukata tamaa!

Kupata milioni nne au nusu yake, lilikuwa ni jambo gumu sana kwa kipindi kile! Lakini lazima zipatikane!

Lazima!

Kwa sababu mtoto pia ameshaanza kuonesha dalili za ugonjwa! Ugonjwa hatari ulioondoa maisha ya pacha wake ulikuwa umeanza kujitokeza asubuhi ya siku hiyo! Kwa hiyo suala la hela, sio tena ni la kusikilizia, ni lazima kuzitafuta kwa udi na uvumba!

Lazima zipatikane!

Swali lililoko kichwani mwake ni lilelile ambalo alikuwa nalo kabla hajaenda kuomba mkopo!

Zitapatikanaje?

Jirani na alipopita, kulikuwa na kibaraza. Akakikalia!

Pengine kichwa kilikuwa kizito, kilimwelemea! Angeendelea kutembea, labda kingesababisha aanguke! Kwa sasa kichwa hicho kilikuwa kama vile kimebeba mzigo! Mzigo wa mawazo!

Machozi yalikuwa yakimlengalenga.

Akaunyoosha mkono wake na kuiangalia alama yake! Alama ya mhuri wenye chata ya nyoka ambayo aliwekewa kwa kuchomwa alipokuwa mtoto mdogo wa miaka mitano.

Aliitazama alama hiyo kama mwenye swali juu yake! Kama ambayo labda ingeweza kufanya miujiza yoyote!

Kumbukumbu ya picha na sauti ya mama aliyekuwa akimlea kabla ya kupelekwa kwenye kituo cha watoto yatima ilimjia!

Ni kumbukumbu ya miaka mingi iliyopita! Akiwa mdogo, lakini alikumbuka vile mama huyo alivyokuwa ameushika mkono wake na kuiangalia alama hiyo. Aliikumbuka na sauti yake pia aliposema, “Umeelewa? Wala usihangaike mwanangu, hii alama haifutiki. Nilikuwa nasubiri ukue kidogo nikwambie. Nilioteshwa nikwambie haya ninayokwambia.

“Huu ni mhuri mzuri. Utakulinda dhidi ya uchawi wa aina yoyote. Hakuna mtu atakayekudhuru kwa uchawi. Ni mhuri uliotokana na nguvu ya jiwe jekundu.”

Kumbukumbu hiyo iliondoka!

Ilipotea kama zinavyopotea picha zinazokuja mawazoni!

Sura ya Zaka ilikuwa imejaa machozi!

Bado aliitazama alama ile, na sasa alipata la kusema, alipata kitu cha kuiambia alama hiyo. “Wewe mhuri, kama ulikuja kwa nguvu za ajabu usingizini, naomba nipe ufumbuzi ili nimwokoe mwanangu. Fanya miujiza nipate pesa za kumtibu mwanangu.”

Licha ya kumaliza kusema hayo, lakini bado alikuwa akiitazama alama hiyo. Aliitazama kana kwamba alikuwa anasubiri kupewa jibu! Yaani asikie jibu la sauti! Yaana mhuri uzungumze!

Hayo ndiyo mambo yanayoweza kumtokea yoyote pale anapokuwa amezidiwa. Pale anapokuwa hana majibu ya kile kinachomtatiza!

Zaka alikuwa bado hana majibu!

Akajiinua na kusimama! Akageuka nyuma kuangalia! Kutoka alipo, jengo na maandishi ya OFISI YA CHAMA CHA MADALALI vilionekana. Akasonya.

* * * * * * * * *

Kazumba alikuwa amefika kwenye ahadi yake. Na sasa alikuwa mbele ya Ras Kim, wamekaa kwenye mgahawa mdogo wa kawaida ulioko kwenye mji wao mdogo.

Inaendelea…