HADITHI: Zindiko (sehemu ya 10)

Muktasari:

  • Huu ni mwendelezo wa hadithi tamu ya Zindiko iliyojaa visa na mikasa ya kimaisha kutoka mtunzi mahiri wa riwaya SULTAN TAMBA. Twende naye...

MPANGAJI akatabasamu na kukubali kwa kichwa. Mwenye nyumba pia akatabasamu na kukubali kwa ishara.

“Asante. Wakati wowote mpangaji akitoka nipigie kama ulivyofanya, ntakuletea wapangaji sahihi. Nafikiri sijawahi kukuangusha.

Wakapeana mikono, Zaka na Kazumba wakaondoka na kuwaacha mwenye nyumba akimwongoza mpangaji kuingia ndani.

Zaka na Kazumba wakawa kwenye furaha – kazi yao imekwisha na bakshishi yao imepatikana.

“Biashara imekwisha. Huyu mama huwa nampenda sana. Hana longolongo.”

Wawili hawa wakasimama kando ya njia, wakapasuliana chao. Zaka akatoa hela ambazo alishapewa kabla ya kusaini makaratasi ya mkataba, akampachulia Kazumba noti kadhaa – akampa! Naye akapokea.

Ni hapohapo ambapo simu ya Kazumba ikaita!

Akaitoa na kuangalia namba!

Ni Ras Kim!

Akaipokea.

“Hallow bosi Kim”

“Hallow, Kazumba, vipi hali yako?”

“... Ni nzuri....”

“Sawasawa, mimi nakuombea dua kila siku mambo yako yaende vizuri.”

“Nashukuru sana, asante bosi kwa kuniombea, na mimi nakuombea pia,” akacheka kidogo.

“Sasa nataka tukutane kwenye ile sehemu niliyokuwa nimekuelekeza.”

“Sawa...Palepale si ndio....”

“Angalia usichelewe, nina mambo mengine ya kufanya.”

“Sawa haina shida...”

Kazumba akakata simu.

Safari ya kutembea ikaendelea, lakini umbea ukamjaa Zaka.

“Mteja gani huyo unayekwenda kukutana naye, mpya au?”

“Anaitwa Ras Kim!”

“Kim ndo nani, mbona hujawahi kunambia kuhusu yeye?”

Zaka na Kazumba katika mwendo mfupi tu wakawa wamefika dukani. Hapo ndipo mahali ambapo Zaka alikuwa amepeleka simu yake kuchajisha. Ni sehemu aliyoizoea kati ya sehemu nyingi za aina hiyo kwenye mji wao. Ni utaratibu aliouzoea baada ya kutokuwa na chaja ya kuchajisha simu yake.

Zaka akamfikia mwenye duka, “Aisee niangalizie hiyo simu hapo kama imepata chaji kidogo. Dili zinanipita.”

Mwenye duka akamuitikia na kuhudumia wateja alionao – ikawa amemuweka kiporo!

Zaka akarudi kwa Kazumba aliyekuwa amesimama pembeni, stori zao zikaendelea.

“Huyu Ras Kim, nilimpangisha kwenye ile nyumba ya kule juu. Alikuwa anaishi Zimbabwe karibu miaka 15, ameamua kurudi nyumbani. Pia nahisi ana jengo lake amenambia anataka nimsaidie. Nahisi ndo anachoniitia.”

“Jengo? Anataka kuliuza au?”

“Mimi ni dalali wa kimataifa. Hata akitaka kuliuza, kulijenga au kulikarabati kwangu inawezekana. Au ushasahau kama mjombaangu ana kampuni ya ujenzi nilikokuwa nafanya kazi zamani, kwa hiyo kama ni ujenzi nitapelekea tenda. Kila siku mjomba ananishawishi nirudi kufanya kazi zake, lakini nakataa.”

Kazumba alijitapa!

Ni kweli, mjombake anamiliki kampuni kubwa ya ujenzi wa majumba ambayo huwa inapata hadi tenda mbalimbali. Lakini yeye hakutaka kufanya kazi hapo baada ya kukwaruzana na machawa wa mjomba wake.

“Sasa kwa nini na wewe usirudi ukale mshahara. Au unaona raha kuzurura.?

“Ana machawa wamemzunguka wanazingua zingua, wananikera sana. Nikipeleka dili, wanataka kudandia juu kwa juu. Lakini kama Ras Kim ataniletea dili la masuala ya ujenzi ntampelekea. Najua lazima atanipa pasenti yangu.”

Zaka akarudi kwa mwenye duka, akalipa pesa na kuchukua simu yake. Baada ya kupewa, akaiwasha na kubonyeza namba kadhaa, akapiga!

Alikuwa anampigia Katibu wa Chama cha Madalali, mtu ambaye alikuwa ameahidiana naye kwenda kufuatilia mkopo wa matibabu ya mwanae.

Bahati nzuri ikapokewa!

“Hallow Katibu...”

“Hallow Zaka…” Sauti ya Katibu ilisikika kutoka upande wa pili.

“Leo ndo uliniahidi nije kwa ajili ya lile suala la mkopo.”

“Ni sawa, lakini nilikwambia uwe na subira zaidi si unajua…”

“Ndio sawa, lakini mtoto wangu leo alivyoamka, amenipa wasiwasi sana. Naomba nije leo kama tulivyoahidiana.”

“Hebu njoo, wacha muda huu niulizie vizuri, ukija nitakupa jibu.”

Zaka akakata simu.

“Nani huyo, Katibu wa chama chetu kuhusu ule mkopo wako? Au?” Kazumba aliuliza kwa shauku.

“Ndo yeye. Ila kama simwelewi - hivi hawa watu wakoje. Mambo siriasi kama haya wanaanza kuongea lugha za kubahatisha, wengine wanaenda kukopa na wanapewa hela wanalewea tu tunawaona na wanasumbua kurudisha marejesho. Mimi hata sijawahi kukopa, ndiyo kwanza nataka kukopa tena kwa jambo la dharura, lakini nahisi kama wanataka kunizingua!”

“kKwa nini unasema wanataka kukuzingua!’

“Ananiambia kwamba niende, lakini ananiulizia! Akaulize wapi wakati yeye ndiyo kila kitu!”

“Hapana, sio kila kitu, yeye ni mtendaji tu, kuna bodi si unajua. Halafu una wasiwasi gani, labda jibu linaweza kuwa zuri!”

“Ananiambia eti niwe na subira! Subira gani wakati leo ndio tarehe ya mimi kwenda pale na kupewa pesa. Mwanangu anateseka, sote tuna wasiwasi pale nyumbani. Ingekuwa ugonjwa mdogomdogo tu, saa hizi nishamaliza mwenyewe.”

“Lakini Zaka. Tatizo la mwanao si ndo kama lilelile lililokuwa linamsumbua yule pacha mwenzake?”

“Na hilo ndilo linalotuogopesha. Na leo asubuhi hakuamka vizuri. Kuna kama dalili za ugonjwa kutaka kumjia tena. Unajua huwa haumjii mara kwa mara, unaakaa sana, wakati mwingine hadi miezi sita au minane. Ila dalili zake ndizo kama hizi tulizoamka nazo leo. Imetupa wasiwasi sana.”

“Kwani... Ni ugonjwa gani ule. Hujawahi kusema. Ni ugonjwa wa kurithi au?

“Daktari alipokuwa anajaribu kuokoa maisha ya yule mtoto wetu, alituambia kwamba huu ni ugonjwa wa kurithi. Yaani mmoja wetu kati ya sisi ana asili ya ugonjwa huo. Nahisi inawezekana nikawa mimi kwa sababu siijui historia yangu ya utotoni.”

“Mlijaribu dawa za asili?”

“Wala hatukuthubutu. Ushamwona huo ugonjwa ukimtokea anavyokuwa? Kwanza analegea, anakuwa kama kalewa hivi, kisha mwili unakuwa na joto kali, halafu baada ya muda mwili unakakamaa sana. Mwisho anazimia. Kuzimia kwenyewe kama hatukuwahi hospitalini, anaweza kuzima hata siku nzima.”

“Mh! Ugonjwa gani huo wa ajabu.”

“Ni wa ajabu kweli. Hata matibabu yake yanahitaji pesa nyingi. Vipimo peke yake tunahitaji kuwa na milioni mbili! Tena kwenye hospitali kuu ya Taifa. Halafu majibu ndo yatatuambia tiba yake ni kiasi gani. Ila tumeshauriwa tuwe angalau na milioni 4 kwa vyote viwili, tiba na vipimo. Magonjwa ya watoto wa kitajiri yanawapata watoto wa kimasikini.”

Mazungumzo yao yakaishia hapo kwa sababu kila mtu alikuwa na safari yake. Zaka alikuwa anakwenda huko alikokuwa ameongea na simu na wakati huohuo, Kazumba alikuwa na safari yake katika shughuli zake za udalali.

Zaka alitembea kwa haraka huku kichwa kikimuwanga kwa mawazo. Maongezi ya simu na katibu yalikuwa yamemtia wasiwasi. Kauli kwamba ‘ngoja nikuulizie, njoo nitakupa jibu,’ ni majibu ya kimjini sana! Ni aina ya jibu linalotolewa na mtu ambaye jibu tayari analo, ila anahamishia sehemu nyingine, ionekane kwamba yeye hahusiki kama jibu litakuwa baya!

Alifikiria sana kuhusu uhai wa mwanae na furaha yao!

Yeye na Maua kwa sasa, furaha yao ni afya ya mtoto wao!

Yeye na Maua, ndoto yao ni kuona kwamba mtoto wao anakuwa na afya njema yenye uhakika. Anapona! Anapona kile kinachomsumbua! Akipona maana yake mashaka ya kupoteza maisha kwa ugonjwa huo yanakuwa yametoweka! Na hilo ndilo analolitaka!

Inaendelea...