Miaka minne Babu Tale akimuombeleza mkewe

Babu Tale akiwa na mkewe Shamsa enzi za uhai wake

Muktasari:

  • Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msanii Diamond Platnumz ameandika kuwa leo ni siku ngumu na moyo wake ni vigumu kupoa kwamba sababu kumbukumbu zinaishi na hajawahi kuhisi kama atapitisha hata wiki bila mkewe, Shamsa

MBUNGE wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamis Taletale maarufu Babu Tale anapitia wakati mgumu kila ifikapo kumbukumbu ya Shamsa Ahmad Kombo, aliyekuwa mkewe ambaye alifariki dunia Juni, 2020 na kumwachia watoto watatu.

Kupitia ukurasa wake kwenye mtandao wa Instagram, leo Juni 28, 2024, Babu Tale ambaye pia ni meneja wa msanii Diamond Platnumz ameandika kuwa ni siku ngumu na moyo ni vigumu kupoa kwamba sababu kumbukumbu zinaishi na hajawahi kuhisi kama ataweza kipitisha hata wiki bila ya mkewe huyo, lakini leo imetimia miaka minne bila uwepo wake.

"Leo ni tarehe na siku yenye kumbukumbu ngumu sana katika kila nukta ihesabiwayo (katika) majira ya dunia. Macho na masikio yanaweza kukubali jambo hili, lakini moyo ni vigumu kupoa maana kumbukumbu inaishi," ameandika mbunge huyo na kuongeza:

"Sijawahi kuhisi kama nitaweza kutimiza hata wiki bila ya wewe Mama TT, ila leo umetimiza miaka minne bila uwepo wako.

"Nashukuru kuwa zawadi njema ya watoto uliowaacha wanakua wakiwa kwenye misingi bora ya dini na hawajaacha kukuombea mama yao kwa kumbukumbu kila ikifika Alhamisi.

"Nashukuru nimeweza kumwambia @@babytatyana kuwa umetangulia mbele ya haki na ipo siku tutaonana, ila haikuwa rahisi kumfanya mtoto wa miaka sita ajue hilo, lakini sikuwa na jinsi kwa maana maswali yake juu ya kurejea kwako kutoka huko ulikokwenda yalikuwa mengi.

"Shida nyingine inakuja pale awapo shule na yakahitajika masuala yanayohusiana na mama mzazi, hii humpelekea kunitaka nikasimame kwenye nafasi yako, na hapo ndipo huwa siku au wiki yangu inakuwa ngumu na kufumua chemba za moyo wangu kwa maumivu makali.

"Bado nasimamia kile tulichokipigania wakati wa uhai wako, kuwa ni lazima watoto wasome na wasiishi maisha tuliyoishi na kubwa tuwape hofu ya Mungu na kuamini kuwa Mungu yupo na kuheshimu kila aliyezidi umri na maarifa.

"Shammy, jua tu haupo duniani ila moyoni mwangu utabaki milele. Nimemisi vingi sana toka kwako ila kikubwa ni kwamba busara zako ndizo zinaongoza mpaka sasa na kuondoka kwako kumeutia moyo wangu ganzi na hofu kubwa sana ya Mungu na kuona kifo kipo usoni mwangu.

"Katika kipindi chote nilichopitia msongo wa mawazo na kukosa mwelekeo ninasaidiwa na dua na ushauri wa watu wema walionizunguka na hawa watoto ulioniachia.

"Mungu aendelee kukupumzisha kwa amani. Mimi nipo na watoto wapo salama na maisha yanaendelea ingawa pengo limegoma kuzibika."

UNAISHI MOYONI MWANGU NA PUMZIKA KWA AMANI. #theblackgodfather"