Bongo Movie waikacha harusi ya Ringo

Muktasari:

  • Ringo alifunga ndoa Ijumaa iliyopita katika Kanisa la Free Church Mikocheni jijini Dar es Salaam kisha usiku akafanya sherehe katika Ukumbi wa Barakuda, Kinyerezi na kuhudhuriwa na wachekeshaji wenzake huku wale wa Bongo Movie wakikosekana ukumbini.

KATIKA hali isiyotarajiwa wasanii wanaounda kundi la Bongo Movie wameikacha sherehe ya harusi ya mchekeshaji maarufu nchini, Jacob William ‘Mkweche’ a.k.a Ringo iliyofanyika wikiendi iliyopita.

Ringo alifunga ndoa Ijumaa iliyopita katika Kanisa la Free Church Mikocheni jijini Dar es Salaam kisha usiku akafanya sherehe katika Ukumbi wa Barakuda, Kinyerezi na kuhudhuriwa na wachekeshaji wenzake huku wale wa Bongo Movie wakikosekana ukumbini.

Mwanaspoti lililokuwepo katika sherehe hiyo, liliwashuhudia wasanii waliofika ni wale anaofanya nao sanaa ya vichekesho hasa wa tamthilia ya Kitimtim ambao ni Mkojani, Tin White, Dulivan, Asha Boko, Mkali Wenu, Masantura, Gladness Kifaluka ‘Pili’, Mwene, Nagwa, Kupa, Love na wengineo.

Tukio hilo liliibua maneno mengi ukumbini, kwani harusi ya Ringo imefanyiwa promo nyingi katika mitandao ya kijamii na hata vituo vya redio na runinga na baadhi ya wasanii wa waigizaji wa Bongo Movie na waimbaji wa muziki wa kizazi kipya walionekana kutoa michango na kuahidi watahuduhria.

Mmoja wa wageni waalikwa Irene na Stella walisikika wakihoji kwa nini wasanii walioonekana mitandaoni wakichagiza hawakuonekana.

“Yaani hii harusi wamekuja wasanii wenzake wa vichekesho tu mbona wale wa Bongo Movie hawajafika na tuliwaona kwenye mitandao wakati wamefuatwa kwa ajili ya michango wakijinadi watakuwepo na hawajafika?” alihoji Stella.

Irene alisema: “Hawa wasanii wetu tatizo lao wanachagua sehemu za kutoka aidha kwenye sherehe kama hivi na hata misiba au inategemea na mtu mwenyewe anaishi nao vipi wenzake, japo tuliona mitandaoni baadhi yao walifuatwa kuombwa michango na wakatoa pesa nyinyi tu.”

Mwanaspoti lilizungumza na mmoja wa wana kamati wa harusi hiyo, Masantula juu ya sintomfahamu hiyo aliyesema huenda wenzao wana dharura.

“Mimi mwenyewe nashangaa kwa nini wasanii  wenzetu tuliowategemea wafike hawakufika, ila huenda wamepatwa na dharura ndio maana hawajajumuika nasi,” alisema Masantura, huku Tin White akiongeza kuwa wapo Bongo Movie waliotoa michango na wengine hawakutoa na pia inawezekana kwa waliotoa mambo yaliingiliana na kushindwa kufika.

“Aaaah buana weee! We acha tu ilimradi sisi tuliopo tumefika inatosha maana huwezi jua huenda mipango na ratiba zimeingiliana na kushindwa kufika, ila tunashukuru wapo,” alisema Tin White.