Mfahamu Kingwendu nje na uchekeshaji

Muktasari:

  • Mwanaspoti limefanya mahojiano na Kingwendu nyumbani kwake Mbagala, anasimulia anavyojipambanua nje ya sanaa, kuhakikisha anafikia malengo ya ndoto zake.

MCHEKESHAJI mkongwe nchini, Rashid Mwinshehe 'Kingwendu' anaamini maisha bila 'plani B' ni vigumu kufanikiwa kwa haraka, vinginevyo mtu afanye kazi inayomuingizia pesa ndefu.
 
Mwanaspoti limefanya mahojiano na Kingwendu nyumbani kwake Mbagala, anasimulia anavyojipambanua nje ya sanaa, kuhakikisha anafikia malengo ya ndoto zake.

"Sijaangalia sanaa pekee, kwani kuna wakati dili za kuigiza haziendi, hivyo lazima niwe na kitu cha kuniingizia pesa ili watoto wangu waweze kusoma, kutunza mke wangu, nategemewa na ndugu na jamaa zangu," anasema.

UBUNGE ULIMKAMUA MAPENE
Licha ya mwaka 2015 kushindwa kupata ubunge katika Wilaya ya Kisarawe, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), hilo halijamkatisha tamaa, anajipanga kutupa karata yake uchaguzi wa mwaka 2025.

"Nilitumia takribani Sh28 milioni katika kampeni zangu, kwa ajili ya kulipa wasanii, magari ya kubeba wanachama, vyakula, mziki mnene, ambapo nilifanya ndani ya miezi mitatu, hivyo ilikuwa lazima pesa initoke ya maana," anasema na kuongeza;

"Pesa za kampeni nilipata kutokana na kuuza magari yangu matatu Toyota Crown, Toyota Land Cruiser na lingine silitaji na bado nilikuwa nadaiwa Sh8 milioni ambazo nilikuwa nimekopa, ili kuniwezesha kampeni zangu kufanyika.

"Nilikuwa najiamini kwa asilimia 99 kupita kwenye uchaguzi wa mwaka huo, wakati naangalia kwenye TV ninavyoongoza kama kata nane kati ya kata 17, basi nikaondoka na kufanya mambo mengi, nikaiachia familia yangu iendelee kufuatilia.

"Akili yangu ikawa inawaza namna ambavyo nitakuwa napiga suti za maana nikiwa naenda bungeni, lakini kuwatumikia wananchi, kuhakikisha wanabadilika, maana wapo nyuma kimaendeleo, mambo mengi Kisarawe yapo kizamani.

"Ilipofika wakati wa kutangaza matokeo, akatangazwa mshindani wangu kuchukua jimbo, nikajikuta nimepoa, sasa nikawa nawaza magari yangu yameenda, nimebakia na deni, ila bahati nzuri nilipata dili la kazi."


KWENDA UJERUMANI
"Desemba 5, 2015 nilikuwa na visa ya kwenda Ujerumani kwa ajili ya shoo, nilialikwa maeneo matatu, hivyo baada ya kufeli uchaguzi, nikakwea pipa kwenda huko.

"Wakati nipo kwenye ndege nilikuwa nafikiria nitafanya komedi za aina gani kwa wazungu, nitazungumza lugha gani, nikajikuta nina msongo wa mawazo wa kufeli uchaguzi na sehemu ninakokwenda," anasema na kuongeza;

"Nimeamini Mungu hawezi kumtupa mja wake, wakati nimeshuka uwanja wa ndege wa Ujerumani, nikaja kupokewa na wenyeji wangu, kumbe shoo iliandaliwa na watu weusi kutoka nchi mbalimbali za Afrika, nikasikia mmoja wao ananiita Kingwendu Mapepe, ikabidi nijitoe akili nikaanza utani naye hadi nilipopata akili kujua nitafanya kitu gani.

"Sehemu ya kwanza nilipopanda kufanya shoo, wakati naimba wimbo wa Binti Mapepe, akapanda bonge la mama jukwaani, nadhani alikuwa Mnigeria, basi nikaanza kucheza naye akawa mapepe wangu, tulikiwasha pale kila mtu aliondoka akifurahi.

"Ukiona wasanii wakubwa hapa nchini, wanakwenda kufanya shoo nje, wanakuwa wanaandaa watu weusi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika, baada ya kutoka Ujerumani, nikaenda Afrika Kusini na Congo, nikarejea Tanzania Januari nikiwa nimepata Sh8 milioni za kulipa deni, sidaiwi na mtu kwa sasa..."


KUHUSU MUZIKI
Anasema licha ya kutoa wimbo wa Mapepe haina maana anataka kujikita kwenye muziki, isipokuwa anafanya ubunifu wa kuwachekesha watu kwa njia ya kuimba.

"Nakumbuka baada ya kutoka kwa video ya wimbo wa Mapepe, kuna mashabiki walikuwa wananishambulia mitandaoni na kuniambia wee mzee achana na kuimba hujui, jamani mimi siyo  Ali Kiba, Diamond wala Konde Boy," anasema na kuongeza;

"Wapo baadhi niliowajibu, nadonyoa donyoa, hivyo watarajie kusikia nyimbo zangu za komedi, ambazo nachanganya na Kizaramu, Kisukuma japokuwa mimi siyo Msukuma, nitatumia lugha yoyote kulingana na wimbo husika."

Kuhusiana na kolabo yake aliyoitangaza kufanya na Diamond Platnumz, alijibu: "Hiyo lazima nitaifanya, kwa sababu aliniambia anatengeneza nyimbo kali, itakayoninufaisha kwenye kazi zangu, hivyo nasubiri vitu vikae sawa."

Anaongeza "Siyo huyo pekee, nitaomba kufanya na Ali Kiba, Konde Boy, nitajikita kwenye vichekesho zaidi, sina sauti kama zao ambazo wanaweza wakaimba nyimbo za mapenzi na wanaoimbiwa wakaingia laini, mimi nikiimba mapenzi nadhani nitakuwa kituko."


MKULIMA
Nje ya sanaa, Kingwendu anafanya kilimo cha mihogo kwa ajili ya biashara, anachofanyia katika Wilaya ya Kisarawe katika kijiji cha Malumbo na anakiri kunufaika nacho.
"Nikivuna nakodisha gari na kupeleka Buguruni sokoni, huko nawaachia madalali, wakifanya kazi nakwenda kuchukua pesa yangu, nimeanza kufanya hivyo kwa muda mrefu na nimeona manufaa yake," anasema na kuongeza;
"Kupitia kilimo nimeona vijana wengi katika wilaya hiyo, wamefungua maduka, wamenunua bodaboda, maisha yao yamebadilika, nimekuwa nikiwashauri watu wengi kuwekeza kwenye kilimo.
"Mwakani panapo majaaliwa ya Mwenyenzi Mungu, nawaza kulima matikiti, kwani shamba langu linakubali zao hilo, nione litaniingizia faida kiasi gani."
Kupitia sanaa yake na kilimo, amefanikiwa kujenga nyumba mbili, moja ipo Kisarawe anakotegemea kuishi siku za usoni na Mbagala anakoishi na familia yake ya watoto sita na mke mmoja.

"Nikiwa nyumbani napenda kukagua daftari za watoto wangu, kujua maendeleo yao ya shule, kwasababu najua bila elimu watateseka huku mbele, ukiachana na hilo pia nina kisehemu cha kulima mboga, mahindi kwa ajili ya chakula pia kuna wakati najichanganya na watu mtaani, ambako napata faida ya kujua vitu vinavyoendelea katika jamii, hata nikitunga vichekesho vitakuwa vya maisha halisi," anasema.


ALIKUWA DALALI
Kabla ya kuanza sanaa mwaka 2000, alikuwa dalali wa nyumba za kupanga na kuuza viwanja na akiwa kwenye harakati hizo alikutana na mkewe anayeishi naye hadi sasa.

"Madalali wa zamani tulikuwa smati, ukitoka kwenda kijiweni, unapiga suti, tai, kiatu kimepigwa dawa, pia hatukuwa matapeli, kwani tulitambua sheria, kama chumba kinapangishwa Sh100,000 kwa mwezi tulikuwa tunaitaja hiyo hiyo, ila madalali wa sasa sijajua wanafanyaje kazi zao," anasema na kuongeza;

"Nikiwa kwenye harakati za kumtafutia mteja chumba, nikakutana na mama watoto, ingawa kwenye ndoa hazikosekani changamoto, kuna wakati tuliachana baada ya kuzaa mtoto mmoja, ila nilipoanza kutoka na kuwa staa akarejea ndio nipo naye hadi sasa."


CHANGAMOTO ZA WAKONGWE
Anasema wasanii wakongwe kwa asilimia kubwa hawawezi kuandika stori kwa ajili ya filamu za vichekesho, hivyo wanajikuta wakipata changamoto ya kufanya kazi, tofauti na ilivyokuwa vichekesho vya majukwaani.
"Ujio wa wachekeshaji chipukizi unaiendeleza sanaa hii, ila tunawaomba wakumbuke kufanya kazi na wazee, yapo mambo wanaweza wakajifunza kutoka kwetu, wakati mwingine hata watunzi wa filamu, wajue tunaweza kuigiza sini (scene) ambazo siyo za kuchekesha," anasema na kuongeza;
"Kuna wakati mwingine hata wakitupa nafasi wanaona tunafaa kukaa kama walinzi magetini  kukatakata viuno, kuna wakati ninaweza nikaigiza kama mjomba, baba ama babu, ni vile bila kutujaribisha, hawawezi kutufahamu upande wetu wa pili."


VICHEKESHO VINAVYOMCHEKESHA
Anasema kuna wakati mwingine akifanya kazi, anajikuta akicheka mwenyewe kabla ya kwenda kwa jamii anayoifanyia kazi hiyo, "Kuna vichekesho nimefanya nikiangalia nacheka mwenyewe, kama Ben Masanduku, Kulipiwa Gengeni na HB.

Anaongeza: "Wakati mwingine muongozaji anajikuta anapata wakati mgumu, kwani kuna wakati naye anakuwa anacheka, ila mwisho wa yote lazima kazi iendelee."


BESTI YAKE
"Rafiki yangu wa shida na raha ni Bambo ndiye aliyenipeleka Kaole Sanaa Group, ndio maana nilipoona Jangwani wanabomolewa, nilimshauri aje huku kununua kiwanja na amefanya hivyo, na tayari kajenga na amehamia," anasema na kuongeza;

"Ukaribu wetu natarajia tutafanya kazi nyingi, tofauti na mwanzo ambapo tulikuwa mbali, hivyo mashabiki watarajie kuona kazi zetu nyingi."

Kwa waigizaji chipukizi anamtaja mchekeshaji Mkojani ambaye amefanya naye kazi baadhi na wana mpango wa kufanya nyingi zaidi, akimsifu ana utunzi mzuri wa maigizo yake.

"Mkojani anakuja vizuri, vichekesho vyake wanaweza wakaangalia watu wote, ndio maana nasema vijana wanapaswa wajichanganye na wazee, ili kupata maarifa ya kuwasaidia kwenye kazi zao," anasema Kingwendu ambaye ni shabiki wa Yanga