Mwanaume amfungulia Diddy kesi akidai kulazimishwa kingono

P. Diddy
Muktasari:
- Kesi hiyo inakuja siku chache baada ya jaji mmoja kuruhusu kuendelea kwa kesi nyingine ya madai ya unyanyasaji wa kingono yenye maombi ya fidia ya Dola 30 milioni dhidi ya mwanamuziki huyo ingawa baadhi ya madai aliyafuta.
Manhattan, Marekani
MWANAMUZIKI Sean “Diddy” Combs anakabiliwa na kesi nyingine mpya ya madai - safari hii kutoka kwa mpigapicha mwanaume anayedai kwamba rapa huyo alimlazimisha kufanya naye ngono ya mdomo pamoja na vitendo vingine vya ajabu akimshawishi kumpa kazi ya upiga picha.
Kwa mujibu wa New York Post katika kesi hiyo ambayo imefunguliwa mjini Manhattan, mlalamikaji huyo ambaye jina lake limehifadhiwa akitajwa kama John Doe, anasema alikutana na Diddy kwa mara ya kwanza alipokuwa akifanya kazi kwa ajili ya tangazo la biashara lililorekodiwa kati ya 2022 na 2023.
Hiyo itakuwa kesi ya sita dhidi ya mwanamuziki huyo ambaye ni miongoni mwa mastaa wa muziki wenye utajiri mkubwa duniani.
Doe anasema wakati wa tukio mojawapo la shughuli hiyo, Diddy alimuita kwenye gari lake kwa kile kilichoonekana kama fursa ya kumtaka kumfanya asonge mbele katika taaluma yake ya upigapicha ambapo mwanzilishi huyo wa Bad Boy Records alimlaghai akitaka wafanye ngono.
Hata hivyo, kesi inadai kuwa mara tu baada ya Doe kuingia kwenye gari, Diddy alianza kumvua nguo huku akimuahidi kumpatia kazi ikiwa wangefanya ngono ya mdomo, lakini mpigapicha huyo alionekana kupinga kufanya kitendo hicho.
“Ujumbe ulikuwa wazi pia kwamba ikiwa mlalamikaji hangetekeleza tendo hilo kwa ridhaa ya Combs, kazi aliyotaka kumpa isingekuwapo,” inaeleza sehemu ya hati ya mashtaka ikimaanisha kwamba mwanamuziki huyo alitumia mbinu ya kazi ili kushawishi kufanikisha azma yake.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka mlalamikaji anasema alitekeleza kitendo hicho. Hata hivyo, anadai hakusikia lolote kutoka kwa Diddy baada ya tukio hilo akidai Diddy 'alimchinjia baharini'.
Upande wa mashtaka unataka kesi hiyo isikilizwe na jopo la majaji ukimtuhumu mwanamuziki huyo kwa unyanyasaji wa kingono, ambapo mpigapicha huyo anadai fidia ya kuathirika kiakili, fidia maalumu, fidia ya adhabu, gharama za mahakama na nafuu nyingine yoyote ambayo mahakama hiyo itaona kwamba inafaa apewe.
Hata hivyo, kupitia mawakili wake, Diddy amekana madai hayo.
“Haijalishi ni kesi ngapi zitafunguliwa hasa zile zinazowasilishwa na watu wanaokataa kuweka majina yao nyuma ya madai hazitabadili ukweli kwamba Combs hajawahi kumshambulia kingono au kujihusisha na biashara haramu ya ngono dhidi ya mtu yeyote — mwanaume au mwanamke, mtu mzima au mtoto," taarifa ya mawakili wa Diddy imesema na kuongeza:
"Tunaishi katika ulimwengu ambapo mtu yeyote anaweza kufungua kesi kwa sababu yoyote. Kwa bahati nzuri, mfumo wa mahakama ulio wa haki na usio na upendeleo upo ili kutafuta ukweli, na Combs ana uhakika kwamba atashinda mahakamani.”
Kesi hiyo inakuja siku chache baada ya jaji mmoja kuruhusu kuendelea kwa kesi nyingine ya madai ya unyanyasaji wa kingono yenye maombi ya fidia ya Dola 30 milioni dhidi ya mwanamuziki huyo ingawa baadhi ya madai aliyafuta.
Hata hivyo iwe Diddy atashinda kesi hiyo au hii mpya bado anakabiliwa na mashtaka kadhaa ya jinai na kesi nyingine nyingi za madai. Kwa sasa anashikiliwa mahabusu akisubiri kusikilizwa kwa kesi za aina hiyo jijini New York.