Prime
Nicole mbaroni kwa tuhuma za kutapeli, Kamanda Muliro afafanua

Muktasari:
- Upatu umemweka matatani mwigizaji Nicole Berry akidaiwa kuunda vikundi na kujipatia pesa kwa njia ya udanganyifu
Mwigizaji na mfanyabiashara, Joy Mbaga maarufu 'Nicole Berry' anashikiliwa na jeshi la polisi Dar es Salaam kwa tuhuma za kujipatia zaidi ya Sh100 milioni kwa njia za udanganyifu.
Akizungumza na Mwananchi leo Machi 5, 2025, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema Nicole (32) alikamatwa Machi 3, 2025 akiwa anaenda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kwa ajili ya safiri ya Lagos, Nigeria.
"Anatuhumiwa kujipatia pesa kwa njia mbalimbali za udanganyifu, kwa kutengeneza magrupu ya upatu katika mitandao kinyume na sheria. Anatengeneza watu wa uongo wa katika magrupu hayo na kuwavutia watu," amesema Muliro na kuongeza;
"Wakati mwingine wakiweka Sh100,000 baada ya mzunguko anakuonesha kuwa watu wengine 48 wapo kwenye grupu hilo, hivyo wewe unaweza kuwa wa kwanza, wa tatu au wa kumi kupokea.
"Kwa hiyo ukipiga hesabu unaona baada ya muda mfupi unaweza kupata kama milioni nne na kitu. Anatengeneza magrupu mengi tu, watu wanachangia lakini, matokeo yake ni magrupu ambayo siyo ya ukweli, kwani yana watu wengi feki."

Amesema hadi sasa kuna walalamikaji zaidi ya 18 waliojitokeza kwenye Kituo cha Polisi cha Oysterbay.
"Zaidi ya Sh100 milioni za watu zimechukuliwa katika mfumo wa udanganyifu. Watu mbalimbali wanazidi kufika kituoni wakidai na wenyewe wamechukuliwa pesa zao. Hadi sasa yupo Kituo cha Polisi cha Oysterbay," amesema Muliro na kufafanua;
"Wito wangu ni watu kuwa makini wanapotaka kufanya biashara zozote ambazo zinapitia njia hii ya mtandao, hasa magrupu ya upatu."
Wanachosema wanasheria
Kutokana na tuhuma hizo, kumekuwa na maoni tofauti kutoka kwa Wanasheria kuhusiana na adhabu anayoweza kupatiwa mwigizaji huyo endapo atapatikana na hatia.
Akizungumza kuhusiana na tukio hilo, Mwanasheria John Mallya amesema kuchezesha upatu ni kosa kisheria.
"Kosa la upataji fedha kwa njia ya udanganyifu limezungumzwa kwamba adhabu yake ni miaka saba jela na hakuna 'option' ya faini. Lakini kuna vifungu vinavyoweza kuruhusu faini ikalipishwa kwa maana mazingira ambayo kosa lilitendeka," amesema Mallya.

Mbali na John, naye Wakili Fulgence Massawe amesema kucheza na kuchezesha upatu vyote ni kosa kisheria.
"Kwa sababu bado polisi wanafanya uchunguzi ni vigumu kusema amefanya kosa gani. Labda angekuwa amesomewa mashtaka mahakamani, lakini sisi tunavyojua kwa Tanzania ni kosa la jinai kuendesha upatu. Siyo kuendesha tu hata kushiriki, Amesema Massawe ana kuongeza;
"Ndio maana hata wanaodai hela ya upatu inakuwa vigumu kwenda kushtaki kwa sababu hata wao wanakuwa ni wahalifu. Mwisho wa siku itaishia kwenye makosa ya upatu na uhujumu uchumi, adhabu zake ni miaka 20 au 30, lakini kwa sasa kusema yeye adhabu yake ni ipi ni hadi polisi wafanyie kazi."