Noma ilivyotikisa ZIFF 2026, Nawanda, Wendy waking'ara
Muktasari:
- Katika tamasha hilo lililoanza Juni 24 na kuhitimishwa Juni 28 mwaka huu, Tamthilia ya Noma imeibuka na ushindi mkubwa kupitia waigizaji wake pamoja na timu ya uzalishaji.
TAMTHILIA ya Noma imeendelea kuvuta hisia kubwa katika tasnia ya burudani Tanzania baada ya kung’ara kwenye Tamasha la 29 la Kimataifa la Filamu Zanzibar (ZIFF) kwa mwaka 2026.
Katika tamasha hilo lililoanza Juni 24 na kuhitimishwa Juni 28 mwaka huu, Tamthilia ya Noma imeibuka na ushindi mkubwa kupitia waigizaji wake pamoja na timu ya uzalishaji.
Zaidi ya filamu 65 zilipenya katika kushindania tuzo mbalimbali ambapo Noma imetwaa tuzo ya Tamthilia Bora ya Mwaka.
Mbali na tamthilia hiyo iliyozalishwa na Adam Kibaro ikiongozwa na Khaleed Mfundo, katika usiku huo wa tuzo, Sadam Nawanda alinyakua Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kiume kwenye Tamthilia, huku Tuzo ya Mwigizaji Bora wa Kike kwenye Tamthilia ikienda kwa Magdalena Munisi maarufu kwa jina la Wendy, wote wanatokea kwenye tamthilia hiyo ya Noma.
NOMA ILIVYOSHINDANA ZIFF 2026
Katika kipengele cha tamthilia bora, zilikuwepo kumi ambapo Noma ilishindana na Mizani (Scale) ya Kenya, Shabakadda Season 2 (Somalia), Cilaaj (Somalia), Nyota (Tanzania), Lazizi (Kenya), Kash Money Season 1 (Kenya), Single Kiasi Season 4 (Kenya), Loving Beyond (Uganda) na Adam to Eve (Kenya).
SAFARI YA NOMA
Kwa mujibu wa taarifa za uzalishaji, Noma ilianza kuonyeshwa mwanzoni mwa mwaka 2025, ikawa miongoni mwa tamthilia zilizopendwa zaidi na watazamaji katika kipindi chote ilichorushwa kupitia Chaneli ya Sinema Zetu kupitia Azam TV.
Tamthilia hiyo ilihitimisha rasmi safari yake Juni 7, 2026, hatua iliyowaacha mashabiki wengi na hisia za utamu wa hadithi kutokana na jinsi ilivyomalizika.
MASHABIKI WATAKA MWENDELEZO
Baada ya ushindi wa ZIFF, mashabiki wameendelea kuomba Noma irudi tena kama msimu wa pili.
Kupitia mitandao, kumekuwa na maoni kama: “Noma haiwezi kuisha hivi… tunahitaji episode ya pili.”
“Bado kuna stori nyingi zilikuwa hazijamalizika.”
Hali hiyo imeifanya Noma kuendelea kuwa gumzo hata baada ya kumalizika kwake rasmi.
DUDE KUBWA LINAKUJA
Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kutwaa tuzo hiyo, mzalishaji wa Noma, Adam Kibaro maarufu Adam Mo, amesema ushindi huo ni matokeo ya kazi ya pamoja ya timu nzima pamoja na sapoti ya mashabiki.
“Nashukuru sana Mwenyezi Mungu pamoja na mashabiki kwa kutupatia ushindi wa tuzo hii ya Tamthilia Bora ya mwaka 2026. Pia nataka kutoa shukrani za dhati kwa timu nzima ya Noma na wasanii wote waliofanya kazi usiku na mchana kuhakikisha tamthilia inafika hapa ilipo. Hii si tu ushindi wetu kama producer, ni ushindi wa kila mmoja aliyehusika. Nawapongeza pia Sadam Nawanda na Wendy kwa kutwaa tuzo za Muigizaji Bora wa Kiume na wa Kike, wamefanya kazi kubwa sana,” amesema.
Alipoulizwa baada ya hapo mashabiki wategemee nini kipya, alijibu: “Dude kubwa linakuja, mashabiki wakae tayari kutupokea.”
Ingawa Noma imehitimisha safari yake katika kuoneshwa kwenye runinga, lakini ushindi wa ZIFF 2026 umeifanya ibaki kwenye historia ya burudani Tanzania.