Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Rekodi Tems akishinda Grammy ya kwanza!

Muktasari:

  • Tems anayefanya vizuri na albamu yake, Born in the Wild (2024), ameshinda katika kipengele kipya ambacho ni maalum kwa muziki wa Afrika cha Best African Music Performance kupitia wimbo wake, Love Me Jeje (2024).

MWIMBAJI wa Afrobeats kutokea Nigeria, Tems, 30, ni miongoni mwa washindi walioweka rekodi katika tuzo za 67 za Grammy 2025 zilizotolewa wikiendi iliyopita huko Los Angeles, Marekani ukiwa ni ushindi wake wa kwanza mkubwa.

Tems anayefanya vizuri na albamu yake, Born in the Wild (2024), ameshinda katika kipengele kipya ambacho ni maalum kwa muziki wa Afrika cha Best African Music Performance kupitia wimbo wake, Love Me Jeje (2024).

Utakumbuka Tems alianza kuvuma Nigeria na Afrika baada ya kutoa EP yake ya pili, If Orange Was a Place (2021) yenye nyimbo kali kama ‘Free Mind’ ulioshika nafasi ya kwanza chati za Billboard U.S. Afrobeats Songs na Bubbling Under Hot 100.

Hata hivyo, ukubwa wa jina lake uliongezeka pindi aliposhirikishwa na Wizkid katika wimbo, Essence (2020) uliochaguliwa kuwania Grammy na kushinda BET 2022 kama Wimbo Bora wa Kushiririkiana, huku Tems akishinda kama Msanii Bora wa Kimataifa.

Ushindi wa Tems katika Grammy 2025 unakuja kufuatia kuwazidi kete washindani wake ambao ni Asake & Wizkid (MMS), Burna Boy (Higher), Yemi Alade (Tomorrow) na Chris Brown ft. Davido & Lojay (Sensational).

“Asante sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha katika hatua hii na kunibariki kuwa na timu hii mahiri,” alisema Tems akiwa jukwaani baada ya kukabidhiwa tuzo na kuongeza:

“Kesho ni siku ya kuzaliwa ya mama yangu, na hii ni Grammy yake ya kwanza. Nataka tu kukushukuru mama kwa sababu amefanya mengi kwa ajili yangu na kaka yangu,” alisema mkali huyo wa kibao, Me & U (2023).

Hii ni tuzo ya kwanza ya Grammy kwa Tems kushinda kupitia kazi yake binafsi!. Narudia tena, hii ni tuzo ya kwanza ya Grammy kwa Tems kushinda kupitia kazi yake binafsi, ila katika rekodi inahesabika kama tuzo yake ya pili.

Tuzo aliyoshinda 2023 katika kipengele cha Best Melodic Rap Performance, ni kutokana na kushirikishwa katika wimbo wa Future, Wait For U (2022) ambao ndio ulioshinda, hivyo kwa mujibu ataratibu naye akapewa.

Hivyo basi, kufuatia ushindi huu wa Grammy 2025, Tems ameweka rekodi kadhaa; mosi, anakuwa msanii wa kwanza wa kike Nigeria kushinda Grammy na wa pili baada ya Burna Boy kushinda 2021 kupitia albamu yake ya tano, Twice As Tall (2020).

Ikumbukwe Nigeria kuna wasanii wengi walioshinda Grammy akiwemo Femi Kuti, King Sunny Ade, Babatunde Olatunji, WizKid n.k, lakini hadi sasa ni Burna Boy na Tems pekee ndio waliofanikiwa kushinda kupitia kazi zao binafsi.

Pili, rekodi nyingine aliyoweka Tems ni kuwa msanii wa pili Afrika kushinda kipengele cha Best African Music Performance baada ya Tyla kutokea Afrika Kusini kushinda 2024 kupitia wimbo wake maarufu zaidi, Water (2023).

Mnamo Juni 2023 waandaji wa Grammy, Recording Academy ndipo walitangaza kuanzishwa kwa kipengele hicho ingawa kumekuwa na malalamiko kuwa Afrika kuna aina nyingi za muziki ambazo kuziweka zote katika kipengele kimoja sio sawa.

Kipengele hiki kinajumuisha aina nyingi za muziki Afrika kama Bongofleva, Afrobeats, Afro-fusion, Afro pop, Alte, Amapiano, Genge, Kizomba, Chimurenga, High Life, Fuji, Kwassa, Ndombolo, Mapouka, Ghanaian Drill, Afro-house, Hip Hop, Ethio Jazz n.k.

Na licha ya Tems kushinda lakini ameshindwa kufua dafu katika vipengele vingine viwili alivyokuwa anawania katika Grammy 2025 ambavyo ni Best R&B Song (Burning) na Best Global Music Album (Born in the Wild).

Je, Tems ni nani hasa? Staa huyu alizaliwa Juni 11, 1995 huko Lagos, Nigeria, muda mfupi baadaye familia yake ilihamia England maana baba yake ni raia wa huko, akiwa na umri wa miaka mitano wazazi wake waliachana, hivyo akareja Nigeria na mama yake.

Mwaka 2021 akiongea na Hot 97, alisema jamii anayotoka ni lazima kwenda shule ili kupata kazi nzuri, kauli yake ilikuja baada ya kuhitimu Chuo cha Dowen huko Monash Afrika Kusini alipopata Shahada ya Uchumi.

Aliacha kazi ya ofisini na kujikita katika muziki akivutiwa na wasanii kama Aaliyah, Destiny’s Child na Lil Wayne ingawa alianza kuimba akiwa na miaka 13 alipojiunga na kwaya na kujifunza piano na alipofikisha miaka 20 akaanza kutengeneza nyimbo zake.

Katika shoo yake, Somerset House huko London, England, Tems alisema aliamua kutengeneza nyimbo zake mwenyewe mwaka 2018 baada ya kuona hakuna mtu anayetaka kumsaidia huku akitumia jina la ‘Tems on the Beat’ kama mtayarishaji.

Hatimaye aliachia wimbo wake wa kwanza alioutengeneza, Mr. Rebel (2018) na kupata mapokezi mazuri mtandaoni, kisha zikafuata EP zake mbili, For Broken Ears (2020) na If Orange Was a Place (2021) ambazo zilipelekea Tems kufahamika na mashabiki wengi Afrika.