Tiger Woods, Vanessa Trump katika penzi la jioni

Muktasari:
- Kufuatia talaka yao, Woods akawa na uhusiano na mwanamichezo wa kuteleza katika barafu, Lindsey Vonn kuanzia 2013 hadi 2015 kisha akawa na mhudumu wa hoteli, Erica Herman 2017 hadi 2023 na sasa yupo na Vanessa Trump wakielekea uzeeni.
JUA linaelekea kuzama kwa gwiji wa gofu duniani, Tiger Woods, 49, na mpenzi wake mpya Vanessa Trump, 47, lakini wana matumaini ya mwanzo mpya utakaokuwa na matokeo mazuri mbele kufuatia ndoa zao za awali kupigwa na kitu kizito.
Ikumbukwe Woods aliachana na mkewe Elin Nordegren mnamo Agosti 2010. Wawili hao walikuwa pamoja tangu Novemba 2003 na walitalikiana wakiwa tayari na watoto wawili, Sam Alexis na Charlie Axel.
Kufuatia talaka yao, Woods akawa na uhusiano na mwanamichezo wa kuteleza katika barafu, Lindsey Vonn kuanzia 2013 hadi 2015 kisha akawa na mhudumu wa hoteli, Erica Herman 2017 hadi 2023 na sasa yupo na Vanessa Trump wakielekea uzeeni.
Woods baada ya kupita huku na kule hivi sasa ametua kwa Vanessa, mkwe wa zamani wa Rais wa Marekani, Donald Trump. Lakini, Vanessa Trump ni nani hasa na imefikaje hapa?
Baba yake Vanessa ni Charles Haydona ambaye alifanya kazi ya uwakili akiwa na wateja mashuhuri kama mwigizaji Marilyn Monroe, huku mama yake Bonnie Haydon akiendesha kampuni ya uwakala wa mitindo, Kay Models Agency.

Kufuatia kifo cha baba yake kilichotokea 2005, Vanessa alirithi sehemu ya utajiri kwani mzee wake alikuwa amewekeza Dola 1 milioni katika kampuni ya vyakula ya Rao's Specialty Foods Inc akimiliki wa asilimia 30.
Hivyo kufuatia kampuni hiyo kuuzwa kwa dau la Dola 415 milioni kama ilivyoripotiwa na Page Six hapo Mei 2018, Vanessa alivuta mkwanja mrefu na hivyo sio mrembo wa 'baby naomba niunge bando', hapana bali mwenyewe anajimudu.
Kabla ya kujihusisha na familia ya Trump, Vanessa alikuwa akifanya kazi kama mwigizaji na mwanamitindo tangu mwishoni mwa miaka ya 1990 kabla ya kusainiwa na wakala wa mitindo, Wilhelmina, na baadaye kufanya kazi pia na Next Model Management.
Kwa mujibu wa The New York Times, Vanessa alisoma shule binafsi ya The Dwight huko Manhattan, New York ambapo alikuwa nyota wa tenisi kisha alisomea saikolojia katika Chuo cha Marymount.

Aliigiza katika filamu ya Something's Gotta Give (2003) pamoja na tamthilia ya Bret Michaels: Life as I Know It (2010), na kubwa zaidi 2011 alitokea katika vipindi vya televisheni vya Trump, The Apprentice vilivyoruka NBC tangu 2004 hadi 2007.
Mwaka 2003 kwenye maonyesho ya mitindo, Rais Trump ndipo alimkutanisha kijana wake, Trump Jr na Vanessa. Wiki sita baadaye walikutana tena katika sherehe ya kumbukizi ya kuzaliwa ya rafiki yao na kuzungumza kwa saa moja.
Unaambiwa haikuchukua muda uhusiano ukaaanza na kufikia 2004 wakachumbiana. Vanessa alivishwa pete ya uchumba yenye dhamani ya Dola100,000 kutoka kwa sonara maarufu wa New Jersey.
Hatimaye wawili hao walifunga ndoa Novemba 12, 2005 katika hoteli ya Trump ya Palm Beach, Mar-a-Lago. Na katika ndoa hiyo walijaliwa kupata watoto watano ambao ni Kai, Donald John III, Tristan, Spencer na Chloe.

Hata hivyo, baada ya miaka 12 ya mafanikio katika ndoa na familia kwa ujumla Vanessa aliwasilisha kesi ya talaka Machi 2018, lakini inaelezwa tayari walikuwa wameshatengana kwa miezi sita kabla ya hatua hiyo.
"Siku zote tutakuwa na heshima kubwa kwa kila mmoja wetu na kwa familia. Tuna watoto wazuri watano pamoja na wanasalia kuwa kipaumbele chetu kikuu. Tunaomba gharama katika wakati huu," ilieleza taarifa yao baada ya talaka kukamilika.
Kufuatia kuachana kwao, Trump Jr alianza uhusiano na Kimberly Guilfoyle ambaye wakati huo alikuwa mtangazaji wa Fox News, na miaka miwili baadaye walichumbiana.
WOODS ATIA TIMU
Machi 13, mwaka huu, chanzo cha karibu na familia ya Trump kiliuthibitisha mtandao wa People kuwa Tiger Woods na Vanessa wamekuwa na uhusiano wa kimyakimya kwa miezi kadhaa na siku chache mbele wakathibitisha kupitia mitandao.

"Upendo umekua na maisha ni mazuri nikiwa na wewe kando yangu. Tunasonga mbele pamoja na safari yetu ya maisha. Kwa wakati huu tungethamini faragha kwa wale wote walio karibu na nyoyo zetu," aliandika Woods kupitia X akiambatanisha picha zao.
Muda mfupi baada ya uhusiano wa Vanessa na Woods kuwekwa hadharani, baba mkwe wake wa zamani, Rais Trump katika video fupi ambayo Ikulu ya White House iliiweka YouTube alisikika akisema amebariki jambo hilo.
"Nampenda Woods na ninampenda Vanessa. Yeye na mimi tuna uhusiano maalumu vivyo hivyo kwa Woods nilicheza naye gofu mara kadhaa miezi michache iliyopita, na ni mwanamichezo mzuri na mtu wa kipekee," alisema Rais Trump wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya Oval na kuongeza:
"Aliniambia kuhusu hilo (uhusiano na Vanessa) na nikasema, 'Woods, hiyo ni nzuri, hiyo ni nzuri.' Nina furaha sana kwa wote wawili."
Kufikia Mei 8, mwaka huu, Woods alirejea White House ikiwa ni ziara yake ya kwanza katika Ikulu hiyo tangu kufichua uhusiano na Vanessa miezi miwili iliyopita.

Bingwa huyo wa gofu mara 15 aliyechuma utajiri wa takribani Dola1.8 bilioni katika kipindi chote cha kazi yake, alipigwa picha akiwa na Seneta wa Indiana, Jim Banks ambaye aliposti picha hiyo katika mtandao wa X.
Ingawa sababu ya ziara hiyo ya White House haijafahamika, kulingana na mtandao wa Golf Monthly, Rais Trump alithibitisha kwamba alikutana na Woods ambaye alikuwa mchezaji namba moja wa gofu duniani mara ya kwanza 1997.