Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TUONGEE KISHKAJI: Mashabiki wa Tanzania wana cha kujifunza Trace 2025

Muktasari:

  • Hawajui kuimba na live band, hawajajipanga, wanapanda jukwaani na madansa wengi na kuruka kuruka utadhani paredi. Na ubaya zaidi ni kwamba sifa hizo mbaya zinaongelewa na sisi wenyewe Watanzania huku sifa nzuri tukizipeleka kwa wasanii wa nje kama Bien kutoka Kenya na Rema wa Nigeria.
  • Kusema kweli, sifa mbaya hizi ni za kweli wasanii wengi wa Tanzania hawakufanya vizuri na wana mengi ya kujifunza kuhusu kutumbuiza live band na shoo zenye atensheni ya kimataifa kama zile.

TRACE Awards 2025 zilifanyika Zanzibar, Tanzania, wiki hii, lakini ukiingia kwenye mitandao ya kijamii kinachoongelewa ni nini? Ni kwamba wasanii wa Tanzania walitumbuiza vibaya, hovyo kabisa. Hawajui kuimba na live band, hawajajipanga, wanapanda jukwaani na madansa wengi na kuruka kuruka utadhani paredi. Na ubaya zaidi ni kwamba sifa hizo mbaya zinaongelewa na sisi wenyewe Watanzania huku sifa nzuri tukizipeleka kwa wasanii wa nje kama Bien kutoka Kenya na Rema wa Nigeria.

Kusema kweli, sifa mbaya hizi ni za kweli wasanii wengi wa Tanzania hawakufanya vizuri na wana mengi ya kujifunza kuhusu kutumbuiza live band na shoo zenye atensheni ya kimataifa kama zile. Lakini kama ambavyo wasanii Wtanzania wana mengi ya kujifunza, ndivyo ambavyo mashabiki wa Tanzania pia wanatakiwa kujifunza kuhusu kutolichafua taifa lao.

Katika tasnia ya burudani, ni muhimu kwa mashabiki wa nchi fulani kuwa mstari wa mbele kuwatetea na kuwaunga mkono wasanii wao hata pale ambapo kuna changamoto zinazohitaji kurekebishwa. Hili ni jambo ambalo mataifa kama Nigeria wamefanikiwa kulifanya kwa ustadi mkubwa, tofauti na Watanzania ambapo mara nyingi sisi wenyewe tunakuwa wa kwanza kuwashusha wasanii wetu kwa maneno makali na dhihaka mitandaoni. Tunaona SIFA.

Nigeria imefanikiwa kuifanya Afrobeat kuwa muziki wa dunia kwa sababu ya utamaduni wao wa kushikamana na kupeana moyo. Katika tuzo kubwa kama Grammy utaona jinsi Wanaigeria wanavyoungana kuwasapoti wasanii wao. Endapo msanii wao atashindwa  hawatajaa Instagram na Twitter kusema alistahili kushindwa kwa sababu hajui kuimba.

Badala yake watampongeza, watatafuta njia ya kuzungumza vizuri kuhusu msanii wao na hata kufurahia kwamba angalau aliteuliwa kushiriki mashindano hayo. Hii inajenga taswira nzuri kwa wasanii wao kimataifa na kuwaongezea heshima na fursa zaidi.

Kwa upande wa Tanzania, mara nyingi tunaonekana kutokuwa na mshikamano kama huo. Shoo ya Trace Awards 2025 ilikuwa nafasi nzuri kwa wasanii wa Tanzania kuonyesha vipaji mbele ya dunia. Ni kweli kwamba wengi walikumbwa na changamoto za kutumbuiza live band, lakini badala ya kutumia mitandao ya kijamii kama jukwaa la kuwashusha na kuwadhihaki, tunapaswa kutumia nafasi hiyo kuwajenga na kuwahamasisha wawe bora zaidi.

Kama tunataka muziki wa Tanzania uchukuliwe kwa uzito kimataifa, lazima tuanze kubadilisha namna tunavyoongea kuhusu wasanii wetu. Badala ya kukomaa kuongelea mazuri ya Rema au Bien ni bora kusema tuna mengi ya kujifunza, lakini tunashukuru kuwa tulikuwa sehemu ya tukio hilo kubwa. Hii inasaidia kujenga taswira chanya kwa wasanii wetu na kuvutia mashirika makubwa kuwekeza kwenye tasnia yetu ya muziki.

Pia, ni muhimu kuelewa kuwa tukiwaponda wasanii wetu hadharani tunawakatisha tamaa na kuharibu taswira ya tasnia kwa jumla. Waandaaji wa matukio makubwa ya kimataifa wakiona jinsi tunavyowachafua wasanii wetu wanaweza kuamua kutoleta matukio hayo nchini kwetu. Badala yake, tunapaswa kuwa sehemu ya suluhisho kwa kuwasihi waendelee kufanya mazoezi, wajifunze zaidi kuhusu utumbuizaji wa live band na kuwekeza katika uboreshaji wa vipaji.

Mwisho wa siku, maendeleo ya muziki wa Tanzania hayawezi kuwa jukumu la wasanii pekee; ni jukumu letu sote kama taifa. Tuige mfano wa mataifa mengine yanayounga mkono wasanii wao na tuache tabia ya kujidharau wenyewe. Kuwa mkosoaji ni rahisi, lakini kuchangia katika mabadiliko ya kweli kunahitaji mshikamano na mtazamo chanya.