Prime
Acheni mazoea! Mambo yamebadilika Ligi Kuu
Muktasari:
- Pia kuna msemo wa Kiswahili unaosema ‘Ukiwa na kawaida ya kufanya jambo kwa mfumo huohuo uliouzoea usitarajie matokeo tofauti. Matokeo tofauti huja kwa kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wako.’ Sasa basi, kitu kinachoitwa mazoea ni kibaya kwani kimewafanya wengi kuangukia pua pale wanapokuwa na matarajio makubwa ya kufanya vizuri.
KUNA methali ya Kiswahili inayosema ‘Kuti la mazoea humwangusha mgema.’ Hiyo ikiwa na maana kwamba jambo ulilozoea kulifanya na kuliona la kawaida kuna siku litakufedhehesha au kukuumiza.
Pia kuna msemo wa Kiswahili unaosema ‘Ukiwa na kawaida ya kufanya jambo kwa mfumo huohuo uliouzoea usitarajie matokeo tofauti. Matokeo tofauti huja kwa kubadilisha mfumo wa utendaji kazi wako.’ Sasa basi, kitu kinachoitwa mazoea ni kibaya kwani kimewafanya wengi kuangukia pua pale wanapokuwa na matarajio makubwa ya kufanya vizuri.
Tunapoiendea michezo ya mzunguko wa 17 katika Ligi Kuu Bara duru hili la pili, kuna mazoea fulani hayapaswi kufanyika. Kama duru la kwanza ulishuhudia timu yako ikimchapa mtu bao nne, usitarajie itakuwa hivyo tena duru la pili kwani kuna mabadiliko mengi yamefanyika, hivyo lolote linaweza kutokea.
Kupitia dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Desemba 15, 2024 na kufungwa Januari 15, 2025, timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zimelitumia vizuri dirisha hilo kuboresha vikosi.
Zipo timu zilizosajili mchezaji moja, huku zingine zikionekana kama zimefumua vikosi kwa kushusha nyota zaidi ya 15.
Mbali na kusajili wachezaji, pia baadhi ya timu zimefanya mabadiliko ya mabenchi ya ufundi ikiwemo KenGold iliyomchukua Kocha Mkuu, Vladislav Heric, raia wa Serbia. Timu hiyo imeonekana kufanya maboresho makubwa ya kikosi chake ikisajili wachezaji zaidi ya 15 wakiwemo waliowahi kucheza timu kongwe za Simba na Yanga kama Bernard Morrison, Kelvin Yondani, Zawadi Mauya na Obrey Chirwa.
Timu nyingine zenye maboresho kwenye mabenchi ya ufundi ni Fountain Gate inayonolewa na Kocha Robert Matano kutoka Kenya, Singida Black Stars ikimchukua Hamdi Miloud mwenye uraia pacha wa Algeria na Ufaransa, huku Tanzania Prisons ikimbeba kocha mzawa, Amani Josiah baada ya mzawa mwenzake Mbwana Makata kuwekwa pembeni.
Kati ya timu hizo zilizofanya mabadiliko ya benchi la ufundi katika kipindi ambacho ligi ilisimama kwa muda tangu Desemba 28, 2024 hadi kurejea kwake rasmi Februari 5, 2025, KenGold na Tanzania Prisons ndizo hazipo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo.
KenGold inaburuza mkia ikiwa na pointi 6 baada ya kucheza mechi 16, wakati Tanzania Prisons ni ya 13 ikikusanya pointi 14 katika mechi 16.
Hadi kufikia sasa, timu zote 16 shiriki zimeshuka dimbani mara 16 huku Simba ikiongoza msimamo kwa pointi 43 ikifuatiwa na Yanga (42), kisha Azam (36) na Singida Black Stars (33) ikifunga nne bora.
Timu nne za chini, inaanza KenGold yenye pointi 6, Kagera Sugar (11), Pamba Jiji (12) na Tanzania Prisons (14).
MZIGO HUU HAPA
Raundi ya 17 ya Ligi Kuu Bara inaendelea kesho Jumatano kwa kuchezwa mechi mbili.
Mapema saa 8 mchana kwenye Dimba la Ali Hassan Mwinyi, wenyeji Tabora United wataikaribisha Namungo.
Mchezo huu unaturidisha hadi Agosti 25, 2024 kwenye Dimba la Majaliwa mkoani Lindi ambapo wenyeji Namungo walikubali kichapo cha mabao 2-1. Kipigo hicho kilikuja baada ya msimu uliopita uwanjani hapo timu hizo zilipokutana Namungo ilishinda 3-2. Huku mechi ya Ali Hassan Mwinyi ikimalizika kwa sare ya 1-1.
Upinzani wa timu hizo unaonekana ni mkubwa na zinapokutana basi kila moja lazima ifunge bao.
Juma Mgunda na vijana wake wa Namungo mechi tatu za mwisho ugenini katika ligi hawajapoteza wakishinda mbili na sare moja wakati Tabora United ya Mkongomani Anicet Kiazayidi mechi tatu za mwisho nyumbani imeshinda moja, sare moja na kupoteza moja ya juzi dhidi ya Simba.
Nao mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga wanaenda kupambania kurejea kileleni wanapokwenda kucheza dhidi ya waburuza mkia KenGold ambao wana mabadiliko makubwa ya kikosi kufuatia usajili ilioufanya dirisha dogo sambamba na kushusha kocha mpya.
KenGold ile iliyokuwa ungaunga ilichapwa na Yanga bao 1-0 duru la kwanza katika mchezo ulioonekana kuwa na ushindani mkubwa.
Mabadiliko ya kikosi cha KenGold yanatoa hamu kubwa kwa mashabiki kutaka kuona wanaanzaje safari ya kujinasua kutoka mstari hatari wa kushuka daraja.
Safari hii wanakutana pale KMC Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni, uwanja ambao Yanga tangu imeanza kuutumia imeshinda mechi zote nne ikifunga jumla ya mabao 12 ikiwa na wastani wa kufunga mabao 3 kwa mechi moja. Pia imeruhusu mawili pekee katika mechi hizo nne.
KenGold kabla ya mabadiliko hayo ya kikosi, imefunga mabao 11 na kuruhusu 29.
Februari 6 ni Dodoma Jiji dhidi ya Pamba Jiji. Hii ni Dabi ya Majiji ambayo duru la kwanza ilimalizika kwa matokeo ya 0-0 kwenye Dimba la CCM Kirumba, Mwanza. Safari hii inachezwa Jamhuri, Dodoma. Itakuwa saa 1 usiku.
Kocha Melis Medo wa Kagera Sugar, ana kazi kubwa duru hili la pili kuiondoa timu yake nafasi ya 15 katika msimamo ili kubaki salama, wakati Mecky Maxime naye lazima akaze, nafasi ya tisa waliyopo sasa Dodoma Jiji na pointi 19, hazitoshi kujiona wapo salama sana.
Tanzania Prisons dhidi ya Mashujaa ni mchezo mwingine ambao unakwenda kutoa majibu ya kile kilichofanyika dirisha dogo.
Prisons ilichukua uamuzi wa kumuondoa Makata na kumpa timu Amani Josiah, kocha ambaye muda mwingi amefundisha Championship, upande wa ligi kuu itakuwa mara ya kwanza kuiongoza timu kama kocha mkuu, hapo awali amewahi kuwa msaidizi Biashara United ilipokuwa Ligi Kuu.
Duru la kwanza pale Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika matokeo yalikuwa 0-0, huku msimu uliopita kila mmoja akitamba nyumbani kwa mwenzake. Mashujaa ilianza kufungwa 2-0, kisha ikalipa kisasi cha kushinda 2-1.
Kocha Mkenya Robert Matano hakuwepo wakati Fountain Gate ikichapwa 4-0 na Simba katika duru la kwanza. Wakati huo kocha alikuwa Mohamed Muya. Simba inayofundishwa na Fadlu Davids, wakati inashinda 4-0 duru la kwanza, Fountain Gate ilikuwa na changamoto ya baadhi ya wachezaji wake kutokuwa na vibali, lakini sasa wapo full mkoko. Itakuwaje pale Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara?
Azam dhidi ya KMC ni mchezo wa mwisho utakaopigwa keshokutwa Alhamisi kwenye Dimba la Azam Complex, Dar huku duru la kwanza KMC ikilala 4-0 nyumbani.
Mechi tano za mwisho baina yao, Azam imeshinda nne mfululizo, huku KMC ikishinda moja pekee.
Kally Ongala ambaye aliwahi kuwa kocha wa Azam, anakwenda kukutana na waajiri wake wa zamani akiiongoza KMC.
Februari 7 itahitimisha mechi za mzunguko wa 17 kwa kupigwa mechi mbili. Coastal Union ya Kocha Juma Mwambusi itaikaribisha JKT Tanzania inayonolewa na Ahmad Ally. Mechi itapigwa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Duru la kwanza Coastal ikiwa chini ya kaimu kocha mkuu Joseph Lazaro, ilichapwa 2-1. Sasa wana kocha mwingine wakati JKT Tanzania inaye yuleyule.
Singida Black Stars iliyojiimarisha kwa kuwashusha nyota wenye uzoefu mkubwa kama Jonathan Sowah na Frank Assinki sambamba na kuboresha benchi la ufundi kwa kumshusha Kocha Miloud Hamdi itaikaribisha Kagera Sugar iliyotoka kupigwa 4-0 na Yanga wikiendi iliyopita.
Singida wanaonekana kuwa wababe wa Kagera baada ya duru la kwanza kuwachapa 1-0.
MAKOCHA WANASEMAJE?
Kocha Mkuu wa KenGold, Vladislav Heric anasema licha ya presha kubwa iliyopo kutokana na nafasi wanayoshika, lakini ataendelea kukisuka kikosi chake huku akiamini usajili uliofanyika dirisha dogo utaleta matokeo chanya.
“Tuna kazi kubwa ya kufanya na kuangalia ni kwa jinsi gani naitoa timu sehemu moja kwenda nyingine, jambo nzuri na la kuvutia nimeingia kipindi ambacho Ligi imesimama, hivyo imenipa nafasi ya kuangalia mapungufu yaliyopo kikosini kwetu,” anasema Heric.
Kocha wa Fountain Gate, Roberto Matano anasema kwa muda aliokaa na wachezaji amefurahishwa na jinsi wanavyofuata vyema falsafa zake huku akiamini kwamba kuna jambo zuri wanakwenda kulifanya duru la pili, wakati Kocha wa KMC, Kally Ongala akifichua kwamba wamejipanga na ushindani wa duru la pili.